Showing posts with label SIASA. Show all posts
Showing posts with label SIASA. Show all posts

"Siyo vibaya kwa wanaotaka kuwania urais kutangaza nia mapema, kwa sababu inawapa nafasi wananchi kuwapima"....Hii ni kauli ya January Makamba baada ya kuhojiwa na kamati ya maadili jana



Kamati ndogo ya Maadili ya CCM imeendelea kuwahoji wanachama wake walioonyesha nia ya kuwania urais, jana ilikuwa zamu ya mawaziri watatu. 
 
Waliotarajiwa  kuhojiwa jana ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.

 Makamba alikuwa wa kwanza kufika mbele ya kamati hiyo jana asubuhi, huku Wassira akifuatia. Hata hivyo, Membe hakuonekana.
 
Hata hivyo, kanuni za uongozi wa maadili za CCM kifungu cha 7 (i) kinaeleza kuwa wanachama wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi katika muhula unaofuata, yaani ubunge, uwakilishi, udiwani na nafasi nyingine katika chama wanaweza kutangaza nia zao, lakini hawaruhusiwi kufanya kampeni kabla ya muda uliowekwa rasmi, muda wa kampeni unaanza baada ya majina ya wagombea kuteuliwa na kikao kinachohusika.
 
Makamba
Baada ya kuhojiwa Makamba, alisema siyo vibaya kwa wanaotaka kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kutangaza nia mapema, kwa sababu inawapa nafasi wananchi kuwapima.
 
Mbali na hilo Makamba alisema siyo dhambi kwa mtu kuonyesha nia, bali ni dhambi kwa mtu kutoa fedha kwa nia ya kutaka uongozi na kuvitaka vyombo vya dola kuchukua hatua za kisheria kwa watu wa aina hiyo.
 
Kikao hicho kinachoongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula, juzi kiliwahoji mawaziri wakuu wa zamani Edward Lowassa na Fredrick Sumaye pamoja na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
 
“Ipo faida ya kuwajua mapema wanaotaka uongozi kuliko kuwajua mwishoni, kwa sababu mnapata faida ya kuwachambua na kuwauliza maswali, mbaya ni mtu kutoa pesa ama kutumia pesa.
 
“Hata katika maoni yangu na ushauri (ndani ya kikao hicho cha maadili), nimesema kwamba hilo ndilo kubwa na la msingi, kwa sababu linawaweka pembeni watu wenye vipaji vya uongozi kama huna fedha basi huwezi kuwa kiongozi,” alisema Makamba.
 
Alisisitiza matumizi ya fedha katika kutafuta uongozi yanakatazwa kwa mujibu wa kanuni za chama chao na sheria za nchi na kwamba ushahidi unapopatikana chama kifanye kazi yake na Serikali ichukue hatua dhidi yao.
 
Makamba alisema ipo sheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ambazo zote zinakataza matumizi ya fedha.
 
“Kwa hiyo hawa wanaotajwa wanatumia fedha vilevile vyombo vya dola viwachukulie hatua, siyo tu kwenye chama,” alisema Makamba.

Makamba alisema kuwa mazungumzo yao ndani ya kikao hicho yalikwenda vizuri, akidai yeye hakuitwa kwa ajili ya kugawa fedha kwa wananchi na wala hakukuwa na shitaka lolote, isipokuwa ilikuwa ni kutoa ushauri na kukumbushana kuhusiana na misingi muhimu ya chama chao ya namna ya kupata uongozi.
 
“Kwa hiyo nilipata fursa nzuri ya mimi kutoa ushauri wangu kuhusiana na namna ambavyo tunaweza kuyafanya mambo haya vizuri zaidi, na namna ambayo tunaweza kutafuta uongozi kwa namna nzuri zaidi badala ya kukigawa,”alisema.
 
Makamba alisema kuwa mazungumzo yao yalikuwa mazuri sana na kwamba hakukuwa na jambo baya, wala hakuwa ameshitakiwa bali walikuwa katika majadiliano ya kawaida ya ndani ya chama na kuwa aliitwa kutokana na kutajwatajwa na wanachama.
 
Wassira
Kwa upande wake Wassira alisema hana mpango wa kutangaza kugombea urais leo wala kesho, lakini muda ukifika ataamua.
 
Alisema: “Kutamani nafasi ya urais siyo dhambi.”
Wassira alisema yeye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hawezi kutoboa mtumbwi ndani ya chama, halafu waangamie wote.
 
Alisema hajafanya vurugu zozote ndania ya chama na kwamba katika kikao cha jana aliitwa kwa ajili ya kujitathimini na kuangalia mustakbali wa chama katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
 
Ripoti ya kamati hiyo ya maadili ya chama huenda ikawasilishwa kwenye mkutano Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), unaotarajiwa kufanyika leo mjini Dodoma.
 
Akizungumzia suala hilo mwishoni mwa wiki iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Philip Mangula alisema mwanachama yeyote wa chama hicho hatakiwi kutoa michango, misaada, zawadi kwa mtu au katika shughuli yoyote bila kupata ridhaa ya uongozi.
 
“Kufanya jambo hilo ni kwenda kinyume na kanuni za chama. Ndani ya chama kila ngazi ina Kamati ya Maadili, wote ambao wameanza kwenda kinyume na kanuni za chama watahojiwa katika kamati hizo,” alisema Mangula na kuongeza:
 
“Hairuhusiwi kuwasafirisha wajumbe, kuwapa malazi, chakula, vinywaji na ukifanya hivyo utakuwa unakwenda kinyume na utaratibu uliowekwa na Kamati ya Sheria, Katiba na Kampeni.”

Akihutubia kilele cha maadhimisho ya miaka 37 tangu kuzaliwa kwa chama hicho, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete aliziagiza Kamati za Maadili na Usalama, kuwachukulia hatua stahiki viongozi na wanachama wake wanaomwaga fedha ili kupata uongozi.
 
Kadhalika, Rais Kikwete alipozungumza na wajumbe wa Halmashauri ya CCM ya Mkoa wa Mbeya, alisema kuanza kwa kampeni kabla ya wakati wake ni moja ya mambo yanayosikitisha na kwamba suala hilo limekabidhiwa kwa Mangula kwa hatua zaidi za kinidhamu.

>>Gazeti  la Mwananchi.

DUDE NAE ATANGAZA NIA YA KUGOMBEA UBUNGE 2015

WIMBI la wasanii kuingia kwenye siasa limeendelea kushika kasi ambapo awamu hii msanii wa maigizo na filamu Bongo, Kulwa Kikumba ‘Dude’ ametangaza kugombea ubunge kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

‘Akistorisha’ na paparazi wetu, Dude alisema kutokana na sanaa kutotoa masilahi ipasavyo, ameamua kuingia kwenye ulingo
DUDE
WIMBI la wasanii kuingia kwenye siasa limeendelea kushika kasi ambapo awamu hii msanii wa maigizo na filamu Bongo, Kulwa Kikumba ‘Dude’ ametangaza kugombea ubunge kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

‘Akistorisha’ na paparazi wetu, Dude alisema kutokana na sanaa kutotoa masilahi ipasavyo, ameamua kuingia kwenye ulingo wa siasa ambapo anatarajia ‘kunyakua’ Jimbo la Tabora Mjini ambalo kwa sasa linaongozwa na Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage.
“Natarajia kugombea ubunge nyumbani kwetu Tabora mjini, niko tayari kuchuana na Rage na kwa sasa  nipo katika maandalizi ikiwemo kuwa karibu na wananchi kwani  wananikubali sana, hivyo natarajia ushindi tu,” alisema Dude.

Chadema watoa fomu mrithi wa Dk Mgimwa.

CDM
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza kutoa fomu za uchaguzi mdogo Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa huku kikijinadi kuibuka na ushindi kwenye uchaguzi huo utakaofanyika Machi 16.
Uchaguzi huo unafanyika ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Dk William Mgimwa aliyefariki dunia Januari Mosi, mwaka huu Hospitali ya Kloof Medi-Clinic nchini Afrika Kusini alikokwenda kwa matibabu ya figo.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa Chadema, Kigaila Benson alisema fomu zimenza kutolewa kuanza Februari 5 na kazi hiyo itasitishwa Februari 9, saa 10:00 jioni.
Benson alisema upigaji kura za maoni utafanyika Februari 10 mwaka huu, siku itakayofuata Kamati ya Utendaji ya Jimbo itapitia maoni yaliyotolewa na kura za maoni kisha itapeleka Kamati Kuu ya Chama yenye jukumu la kumteua mgombea.
CDM
“Febriari 12 mwaka huu, Kamati Kuu itakutana na siku hiyo tutamtangaza mtu ambaye atapeperusha bendera ya chama chetu, siku tutakayozindua kampeni na bajeti nzima itakayotumika,” alisema.
Mwananchi

HATIMAYE CCM MKOA WA SHINYANGA YALAANI VURUGU ZA CHADEMA KATIKA KAMPENI ZA UCHAGUZI KAHAMA.

CCM
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Khamis M. Mgeja akimpa pole Afisa Mtendaji wa kata ya Ubagwe katika halmashauri ya wilaya ya Ushetu Alphonce John Kimario aliyejeruhiwa kwa kushambuliwa na mapanga na watu aliowataja kuwa ni wafuasi wa CHADEMA, kupitia vurugu zilizotokea juzi saa moja usiku katika kata ya Ubagwe muda mfupi baada ya kumalizika kwa kampeni za kumnadi mgombea wao Bw. Hamisi Majogolo, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Itabola A.
kizungumza na waandishi wa habari Afisa huyo Mtendaji wa kata ya Ubagwe, Alphonce John Kimario amesimulia kuwa sanjari na kuumia vibaya machoni hasa jicho lake la kulia pia analalamika juu ya maumivu makali anayo yasikia mgongoni mara baada ya kupigwa na nondo ambapo kwa hivi sasa upande wa kulia sanjari na bega lake umekufa ganzi. 
Ndugu Alphonce Kimario (Afisa Mtendaji wa kata ya Ubagwe) ambaye amepigwa nondo, amepigwa mapanga kwenye paji la uso kiasi cha kushonwa nyuzi kadhaa na kutobolewa jicho moja amekimbizwa hospitali ya Rufaa Bugando kutokana na hali yeke kuwa mbaya zaidi.
Tabitha Shuli ambaye ni Afisa Muuguzi Idara ya Macho Hospitali ya Rufaa Bugando mkoani Mwanza akimhudumia Ndugu Alphonce Kimario.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Khamis M. Mgeja akiongozana na makada wengine wa CCM mkoa wa Mwanza kuelekea ward nyingine kuwaona majeruhi wengine walio lazwa katika hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza mara baada ya kushambuliwa kwa mapanga pamoja na kuharibiwa mali zao mara baada ya kumaliza kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wilayani Kahama mkoani Shinyanga..
Dereva wa gari la CCM wilaya ya Kahama Charles Peter akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwaajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa mapanga wakati wa kampeni za udiwani wilayani humo.
Majeruhi wengine  kama Masoud Melimeli (katibu Mwenezi wa Wilaya) amebaki katika uangalizi wa Hospitali ya Wilaya akiwa na majeruhi wengine kama Ramadhani Salum (Umoja wa Vijana) na Mussa Daudi (Katibu Uchumi Kata ya Nyihogo) ambaye alilazwa katika Hospitali ya wilaya ya Kahama na mara baada ya kuzidiwa leo asubuhi amepakiwa katika AMBULANCE kuwahishwa Bugando kwa ajili ya matibabu zaidi. Ikitajwa kuwa yeye alipigwa nondo ya kifuani.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Khamis M. Mgeja akimpa pole Sebastian Masonga (Katibu UVCCM Kata ya Majengo) aliyepigwa nondo na hatimaye kuvunjwa mkono wa kushoto, kuliani ni mwenyeji wa msafara huo ulio tembelea hospitali hiyo, Katibu wa CCM mkoa wa Mwanza Mama Joyce Masunga.
Sebastian Masonga ambaye ni Katibu UVCCM Kata ya Majengo akisimulia juu ya tukio zima la kuvamiwa. 
Pamoja na kulaani vurugu hizo Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mjumbe wa Halm

Kipigo chatokea kati ya CCM na CHADEMA wilayani Njombe


KIKOSI cha ulinzi cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Njombe, mkoani Iringa kimewashushia kipigo wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kumvunja taya mwanachama, Ally Kalonga.
Licha ya kushusha kipigo hicho, Mkuu wa Polisi wilayani Njombe, Lucy Mwakafirwa, amelaumiwa kuwakumbatia watuhumiwa makada wa CCM, huku akiwasweka ndani wanachama wa CHADEMA.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio, mwananchi ambaye hakupenda jina lake litajwe, alisema kikosi cha CCM cha ‘Green Guards’ kilitoa kipigo kwa wafuasi wa CHADEMA baada ya kubaini mpango wao wa kutaka kugawa fedha kwa wapiga kura utabainika.
CCM na CHADEMA wako katika kampeni za udiwani wa Kata ya Njombe Mjini unaotarajiwa kufanyika Februari 9,  sambamba na kata nyingine 27 nchini kote.
“Siku ya leo (jana) tulikuwa na mikutano ya kampeni za udiwani wa Kata ya Njombe Mjini, mikutano ilifanyika salama huku vyama vyote vikimaliza salama,” alisema.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, baada ya kukamilika kwa kampeni hizo viongozi wa CCM wilayani hapo wakiongozwa na mbunge wa chama hicho (jina linahifadhiwa), walielekea katika Kijiji cha Matalawe.
Mwananchi huyo alisema baada ya kufika Matalawe, walikusanya baadhi ya wananchi na kuwaweka katika chumba kimoja na kuanza kugawa fedha.
“Baadhi ya Wana CHADEMA waliokuwepo pale, hawakupendezwa na jambo hilo, hivyo waliamua kupiga simu kwa viongozi wao kuwajulisha mchezo huo mchafu na viongozi hao walichukua gari kuja eneo hilo,” alisema. Alisema kabla ya kufika walikutana na  kundi la vijana wa CCM waliokuwa wametanda barabarani.
Alisema vijana hao wa CCM waliwaamuru Wana CHADEMA hao wasimame, kisha walichomoa funguo za gari lao lililokuwa likiendeshwa na Ally Muhagama.
“Green Guards walisimamisha gari  la vijana wa CHADEMA, wakamnyang’anya funguo dereva, wakamshusha chini na kuanza kumpiga. Wakati wakiendelea kumpiga, ghafla alitokea mtu mmoja aliyevaa kiraia na kujitambulisha kuwa askari na kuomba wamuachie mtu huyo.
“Kutokana na kauli hiyo mbunge aliyekuwa na vijana wa CCM alimuomba raia huyo  atoe kitambulisho lakini hakuwa nacho, ndipo naye alipogeuziwa kibao na kuanza kupigwa na baadaye walifungiwa kwenye ofisi ya CCM ya eneo hilo,” alisema mtoa habari wetu.
Alisema vijana wa CHADEMA waliojificha baada ya kuona wenzao wakipata kipigo hicho walijaribu kukimbia lakini Green Guards waliwakamata na kuwapa kipigo huku mmoja wao akivunjwa taya na hali yake si nzuri.
“Hata hivyo wananchi walilazimika kupiga simu polisi ambapo walifika na kuwaamuru Wana CCM hao na mbunge wao wawatoe na kuelekea kituo cha polisi,” alisema.
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, wakiwa polisi, mbunge huyo na viongozi wa wilaya walifika kituoni na kwenda moja kwa moja katika ofisi ya OCD Mwakafirwa.
Mwananchi huyo alisema baada ya dakika chache ilitolewa amri ya kuwasweka ndani wanachama hao wa CHADEMA walioumizwa, huku baadhi yao wakiendelea kuvuja damu.
Gazeti hili lililazimika kumtafuta Mwakafirwa ambaye hakukubali wala kukataa kuwepo kwa vurugu hizo huku akimtaka mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi (ACP) Ramadhan Mungi, kwa taarifa zaidi.
Kwa upande wake Kamanda Mungi alisema hajapata taarifa kamili na kwamba anafuatilia kujua ukweli na undani wa tukio hilo.
>> tanzania daima

Mbowe Amjibu Rais Kikwete


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amemjibu Rais Jakaya Kikwete kwamba asiingize utani katika masuala mazito ya taifa. Mbowe alisema Katiba ya Tanzania, itaamuriwa na wananchi wenyewe na si Chama Cha Mapinduzi (CM) ambacho kimekuwa na mkakati mkali wa kutaka kuua maoni ya wananchi.

Mbowe ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tu baada ya Rais Kikwete kudai amesikia kiongozi huyo wa upinzani akitangaza kutumia nguvu kupata Katiba mpya.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, wakati akihutubia sherehe za miaka 37 ya kuzaliwa CCM. Alisema amesikitishwa na kauli hiyo na kuwataka Watanzania kutobabaishwa.Kikwete alisema Katiba mpya itapatikana kwa hoja za kila upande kulingana na mapendekezo yake.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mbowe alisema Rais Kikwete hapaswi kuchukulia utani katika mambo mazito ya taifa.“Namuomba Rais Kikwete asichukulie utani mambo ya taifa suala la Katiba mpya. Anapaswa kuzungumza mambo ya msingi ambayo yanaleta tija.

“Siku zote Katiba ya nchi inapatikana kwa dhamira nzuri lakini tumebaini wenzetu hawa CCM hawaheshimu hoja za wananchi.“Hebu tujiulize jinsi Jaji Joseph Warioba alivyotumia fedha nyingi kukusanya maoni ya Watanzania, leo CCM hao hao wanayakataa tuwaeleweje?” alihoji Mbowe.

Alisema Jaji Warioba ametoa hoja za msingi lakini kwa sababu ya uoga wa CCM wanataka kupindisha ukweli wa mambo.“Mzee wa watu huyu amezunguka taifa zima kwa fedha za walipa kodi wa nchi hii, sasa wanataka watumie wabunge wao kukwamisha mchakato huu,”alisema Mbowe.

Alisema kama utawala wa Rais Kikwete utashindwa kuleta Katiba mpya ambayo inakidhi matakwa ya Watanzania, wao wataendelea kudai utawala mpya utakapoingia madarakani uwe ni wa Chadema au CCM.
“Nawahakikisha Watanzania, ikija Katiba mbaya tutaendelea kuidai kwa nguvu zote iwe CCM imeingia madarakani au sisi, Kikwete awe madarakani au asiwepo hatulali kamwe. “Katiba ni maridhiano ambayo yanabeba maoni ya Watanzania sasa kwa nini CCM hawataki kuyafuata?” alihoji Mbowe.

Alisema CCM haina hatimiliki ya Katiba mpya na kwamba wakati wa kufanya uamuzi mgumu wa kupindisha maoni ya Watanzania umefika.“Hawa watu hawana hatimiliki ya Katiba mpya, kwa nini wanajawa uoga kiasi hiki? Wanaogopa serikali tatu, nakwambia sitaki utani kwenye ya msingi,”alisema Mbowe.
>>mtanzania

CHADEMA yatoa ufafanuzi kuhusu tuhuma za ufisadi zilizoelekezwa kwa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe



Kama mojawapo ya mikakati ya baadhi ya watu wanaotaka kuhamisha mjadala wa makosa yanayowaandama ya utovu wa maadili na usaliti dhidi ya chama, hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe amezushiwa tuhuma zisizokuwa na ukweli wowote zikilenga kumchafua kwa nafasi yake ya uongozi na kuipaka matope taasisi anayoiongoza.
 
Tuhuma hizo ni pamoja na;
1. Kwamba Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa mwaka 2005 eti alichukua fedha kutoka kwa Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono kiasi cha sh.Milioni 40 ili Mwenyekiti Mbowe asifanye kampeni katika jimbo hilo.

2. Mwaka 2008, eti Mbunge Mkono alimpatia Mwenyekiti wa Chama Taifa, sh. Milioni 20 kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Tarime, kisha akazitoa kwenye chama kama mkopo na akalipwa.

3. Mwaka 2010, wakati wa uchaguzi mkuu Mbunge Mkono eti alimpatia Mwenyekiti wa Chama Taifa sh. Milioni 200 kwa ajili ya kampeni za mgombea urais.
 
4. Mwaka huo huo wakati wa uchaguzi mkuu, eti Mwenyekiti wa Chama Taifa, alipokea sh. Milioni 100 kutoka kwa Rostam Aziz kwa ajili ya kampeni.
 
Idara ya Habari ya CHADEMA, inapenda kutaarifu umma yafuatayo;
 
1. Hakuna ukweli hata mmoja katika tuhuma hizo. Ni uongo na uzushi uliopangiliwa kama moja ya mikakati ya watu wenye malengo ya kutaka kuilaghai jamii kwamba viongozi wa CHADEMA hawana tofauti na wale wa CCM na kwamba chama hiki kikuu cha upinzani kinachobeba matumaini ya Watanzania katika kupigania haki zao na kupinga kila aina ya ufisadi, kionekane hakina tofauti na chama kilichoko madarakani, ambacho kimepoteza ushawishi kwa wananchi.

 

2. Matokeo ya uongo huo ni kutaka kuisaidia CCM na kugeuza mjadala.
 

3. Idara ya Habari ya CHADEMA inapenda kuuambia umma wa Watanzania wote, hususan wanachama, wapenzi, mashabiki wa CHADEMA na wapenda mabadiliko nchini kwamba,Mwenyekiti wa Chama Taifa, ameshawasiliana na mawakili walifanyie kazi suala hili kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.
 

4. Kwa uhakika tunapenda kuiambia jamii ya Watanzania wote, hususan wanachama, wapenzi, mashabiki wa CHADEMA na wapenda mabadiliko wote nchini, kwamba; Chama wala Mwenyekiti wa Chama Taifa, mahali popote na wakati wowote, hajawahi kupokea msaada wa fedha hizo kutoka kwa waliotajwa kwa malengo yaliyosemwa.
 

5. Tungependa kuwaambia waliozusha tuhuma hizo, ni vyema kama wanapenda kutunza heshima kidogo waliyobakiza katika jamii kutokana na kuelemewa na mzigo wa tuhuma za utovu wa maadili na usaliti dhidi ya CHADEMA, badala ya kugeuka kuwa mabingwa wa kupika uongo, wajibu masuala ya msingi yanayowaandamana kuhusu mikakati yao ya kuhujumu CHADEMA na viongozi wake, ambayo iwapo chama kisingeibaini na kuchukua hatua za kinidhamu, ingesababisha kuua ndoto na matumaini ya Watanzania kufanya mabadiliko ya kimfumo na kiutawala, kwa kuiondoa CCM madarakani.
 

6. Taarifa kuhusu baadhi ya tuhuma katika mkakati huo ambazo zimemlenga Mwenyekiti wa Chama Taifa, kwa kuhusisha shughuli zake binafsi za uwekezaji, zitajibiwa kupitia taasisi husika.


Imetolewa leo Dar es Salaam na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari- CHADEMA

Kauli ya UVCCM kuhusu baadhi ya wana CCM wanaojinadi kugombea nafasi za uongozi



Kwa kipindi kirefu sasa vijana ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tumeshuhudia na kusikia kauli na vitendo vya baadhi ya wanachama wa CCM vinavyoashilia ukiukwaji wa makusudi wa maadili, miiko na kanuni za Chama.

CCM katika uhai wake wa miaka 37 baada ya kuunganisha TANU na ASP, imeendelea kukua na kushamiri kutokana na misingi imara ya kikatiba tuliyojiwekea tangu mwaka 1977, ambayo wana CCM wote kwa utashi na hiari tumeienzi na kuifuata.Asiyetaka, ni ruksa kuondoka na kutuachia chama chetu.

Ni kwa njia hii tumeweza kuimarisha mshikamano ndani ya Chama Cha Mapinduzi na kutuwezesha kushinda katika 
chaguzi mbali mbali, hivyo kuendelea kutoa uongozi katika ngazi zote za utawala nchini. 

Hivyo basi, kitendo chochote kile chenye mwelekeo wa kubomoa mshikamano ndani ya Chama, ni kitendo cha kutudhoofisha, hivyo kutuengua katika uongozi wa nchi. HILI KWA VIJANA WA CCM, HALIKUBALIKI.

Tunasema hivyo kwa sababu kuanzia mwaka huu tunaingia kwenye mchakato wa chaguzi mbali mbali zitakazohitimishwa mwakani na uchaguzi mkuu, mchakato unaohitaji mshikamano wa hali ya juu ndani ya chama. Bila ya tunu hiyo, chama kitatetereka na hatma yake ni vurugu, mipasuko na utekelezaji mbovu wa ilani ya chama ambayo ni silaha yetu kuu ya kukonga nyoyo za Watanzania.

CCM iliyotulea sisi vijana inatutaka kipindi kama hiki kuhakikisha kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM inatekelezwa kikamilifu, hivyo penye mapungufu parekebishwe na penye mafanikio pashangiliwe. 

Na bahati yetu nzuri ni kuwa Serikali ya Rais Kikwete imefanya mengi mazuri yenye kumgusa kila Mtanzania mwenye nia njema na nchi yake. 

Lakini tunachokiona sasa ni kitu tofauti kabisa na malezi na makuzi yetu ndani ya Chama kwani tayari baadhi ya wana CCM, bila woga wala aibu, wameshajitangaza kuwa wagombea wa Urais, Ubunge, Udiwani na nafasi zingine za kupigiwa kura na wameanza kwa kampeni za kishindo za rushwa na vishawishi mbalimbali nje kabisa ya taratibu, kanuni na maadili ya chama. 

Kinachotishia kutoweka kabisa kwa mshikamano ndani ya Chama ni makundi ya mashabiki yanayoundwa na "wagombea" hawa wasio rasmi yanayopita nchi nzima kushawishi (kwa fedha na rushwa zingine) makundi mbalimbali ya kijamii, ya kijasiriamali ili kuungwa mkono. 

Ilani ya CCM ya 2010 imewekwa pembeni, kinachonadiwa ni "Ilani" binafsi za kumwaga pesa nchi nzima, kusambaza elimu kama njugu, bila kuelezea vyanzo vya mapato vya serikali zao za kusadikika.

Huu ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi, maadili, miiko na taratibu ndani ya Chama; ni fedheha kubwa kwa Chama na Serikali yake ambayo iko wima kuhakikisha kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2010 inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa 
 
CCM ina taratibu zake za kupata uongozi na wote tunazijua, kufanya kinyume na taratibu hizo ni uasi, upungufu wa busara, na ukosefu wa sifa ya uongozi.

Hivyo vijana wa CCM tunamuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Taifa Mh. Dr Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa CCM Ndugu Philip Mangula, na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama, Ndugu Nape Nnauye na viongozi mbalimbali wa Chama waliokemea tabia hii mpya na hatarishi ndani ya chama chetu ya kuhaha kupata uongozi nje ya taratibu na kutumia vishawishi vyenye sura ya rushwa vinavyokitia doa Chama.

Kwa kuwa dhamira ya miiko, maadili na kanuni za Chama ni kutuunganisha wana CCM wote kuwa kitu kimoja , dalili zozote nje ya tunu hizo ni usaliti, uasi ambao hauna budi kupigwa vita kwa nguvu zetu zote hasa sisi vijana. 

Hapa hatutakiwi kumwangalia nyani usoni. Gharama ya kuendelea kuvumilia kauli na vitendo hivi vipya na hatarishi katika historia ya Chama chetu, ni majuto. 

Waswahili hunena bandu bandu humaliza gogo, na bandu bandu hii iliyoanza tusiivumilie, itatuweka pabaya. 

Wana CCM wote tunaamini kuwa hakuna mtu yeyote aliye juu au mkubwa kuliko chama, hivyo uasi ulioanza kuota mizizi ndani ya chama hauna budi kung'olewa mara moja tena bila ganzi, bila huruma. 

Kamati ya Maadili ya CCM ina wajibu wa kutafsiri hasira ya wana CCM na Viongozi wao kwa vitendo. UVCCM inahimiza kuwa wale wote walioanza kampeni za uraisi, ubunge, udiwani na nafasi nyingine zozote kwa vitendo na kauli za kukiuka taratibu, hivyo kukikejeli Chama, kukejeli uongozi wa nchi uliopo na kuleta nyufa katika chama chetu, waonyeshwe mlango wa kutokea.

Tusipoziba ufa huu sasa, tujiandae kujenga ukuta mwakani kwa gharama kubwa ya kupindukia.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Paul Makonda
MKUU WA IDARA YA UHAMASISHAJI NA
CHIPUKIZI TAIFA

Zitto Kabwe auanika Ufisadi wa Freeman Mbowe... Adai Tundu Lissu ni kifaranga, hivyo anamtaka mama kifaranga....Amegusia pia kifo cha Chacha Wangwe



====Huu  ni  ujumbe  wa  Zitto Kabwe  kujibu  mapigo  ya  Tundu Lissu===
**
Lissu anasema nimepewa magari 2 na Mzee Mkono. Anasema kaambiwa na Mkono. Naamini Mkono alimwambia pia mwaka 2005 alimpa Freeman Aikaeli Mbowe tshs 40m ili Mbowe asifanye kampeni Musoma vijijini. 

 Nadhani alimwambia pia mwaka 2008 (baada ya orodha ya mafisadi kutangazwa 2007) Mkono alimpa Freeman tshs 20m za uchaguzi wa Tarime na Freeman akasema kwenye chama ametoa mkopo na akalipwa.

 Nadhani alimwambia pia kuwa Mwaka 2010 Mkono alimpa Mbowe tshs 200m za kampeni ya Slaa. Pia hakusahau kumwambia kuwa Rostam Aziz alimpa Mbowe tshs 100m za kampeni. Lissu anajua kuwa gazeti la Tanzania Daima limeanzishwa na fedha za chama kutoka Conservative party?

Nimefanya internship yangu kwa Mkono and Company Advocates kuhusu masuala ya mikataba. Mzee Mkono ni Mzee wangu na alisaini petition ya kumtoa Waziri Mkuu Pinda.

Lissu awaambie waliyemtuma wamwambie ukweli wote. Lissu ajue yeye ni kifaranga tu, Mimi namtaka mama wa kifaranga ajitokeze. Aeleze aliingia deal gani na Kinana na Sumaye mwaka 2005 kufuatia deni lake NSSF. Aweke wazi mkataba kati yake na NHC kuhusu nyumba ya Umma ilipo Club Bilicanas.

They must know I am not a push over. Chacha died, I won't.

Mtu ambaye hawezi kuheshimu mke wake aliyemzalia watoto hawezi kunyooshea mtu kidole kuhusu maadili.

Hatimaye Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba wavuliwa uanachama wa CHADEMA...!!

 
Dk.Kitila Mkumbo aliyetimuliwa uanachama Chadema.
Samson Mwigamba ambaye naye amevuliwa uanachama wa Chadema.
 
KAMATI Kuu ya Chadema iliyokutana Januari 3-4, 2014 katika Ukumbi wa Mbezi Garden, jijini Dar es Salaam imeamua kuwavua uanachama Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba kuanzia jana.
 
Maamuzi hayo ni baada ya kunasa mawasiliano mbalimbali ya Zitto Kabwe na washirika wake akiwemo anayejulikana kwa jina la Chadema Mpya.
 
Akizungumza na wanahabari leo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willbroad Slaa amesema malengo ya waraka wa mabadiliko waliokutwa nao wahusika hayakuwa ya kisiasa tu bali yalikuwa na lengo la kuimaliza chadema na kuwabomoa viongozi wa chama.
 
Ameongeza kuwa, chama kinawatangazia wanachama wote na wapenzi wote kutokushiriki mikutano ama shughuli zozote za kisiasa zitakazoandaliwa na Zitto Kabwe na washirika wake kwa jina la Chadema.

CHADEMA watwangana ngumi tena.....Awamu hii ni ndani ya kikao kilichokuwa kikiendeshwa na Freeman Mbowe


 
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Shaaban Mwamba, juzi usiku alipata kipigo kutoka kwa maofisa wa  kikundi cha ulinzi cha chama hicho waliokuwa katika eneo ambalo mkutano wa Kamati Kuu ulifanyika, baada ya kutuhumiwa alikuwa akiwasiliana na wafuasi wa Zitto.
 
Taarifa kutoka kwa mjumbe mmoja ambaye hakupenda jina lake litajwe, ilisema kuwa mtu huyo alikuwa akichunguzwa na maofisa wa ulinzi wa chama hicho muda mrefu, kutokana na nyendo alizokuwa akizionyesha zilizotia shaka.
 
Mwandishi wa habari hizi ambaye alikuwa katika eneo hilo, alishuhudia kiongozi huyo akibebwa juu juu na maofisa hao, huku akiulizwa aliyekuwa akiwasiliana naye ni nani, kabla ya vijana wengine wa chama kumkamata na kumweka chini ya ulinzi, wakimtaka atoe ufafanuzi wa alichokuwa anakifanya.
 
Baada ya mahojiano ya muda mfupi, kiongozi huyo alionekana akiinuka na kwenda  kunawa kwenye bomba la maji, huku akitokwa damu mdomoni.
 
Taarifa zilizopatikana baadaye zilidai kuwa kiongozi huyo alikuwa akiwasiliana na mama yake Zitto na Katibu wa Zitto, Dk Alex na kwamba pia simu yake ilikutwa na ujumbe mfupi aliokuwa amewaandikia watu hao.
 
Mwandishi wetu alijaribu kumtafuta kiongozi huyo ili kueleza sababu ya kupigwa kwake, lakini hakupatikana eneo la mkutano kwa madai kuwa alikwenda hospitali kupata huduma ya kwanza, lakini hakurudi.

Wakati hatima ya  Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe  ikisubiriwa kujulikana hapo kesho baada ya Mahakama kutoa hukumu yake, inadaiwa kuwa baadhi wa wabunge, viongozi na wazee wa Chadema, wanataka suala hilo liishe mapema.
 
Habari ambazo zilipatikana  jana zilisema kuwa baadhi ya viongozi hao walitaka Zitto aende Halmashauri Kuu ya Chadema na kuomba msamaha ili mambo yaishe.
 
“Walimfuata Kitila (Dk Kitila Mkumbo) wakamwambia amshawishi Zitto ili mambo yaishe nje ya mahakama, wanataka aende kwenye Halmashauri Kuu kuomba radhi. Kitila akawaambia kuomba radhi kwa kosa gani?” kiilisema chanzo hicho.

Hata hivyo, Zitto aliiambia Mwananchi jana kuwa kumekuwa na jitihada  mbalimbali za wazee kutaka kukiepusha chama hicho na migogoro na kuwa amekuwa tayari kwa suala hilo. “Wazee walikuwa na wajibu wa kuhakikisha hatufiki hapa tulipofika. Sijui kama fursa hiyo bado ipo,” alisema Zitto.
 
Kuhusu uamuzi wake wa kwenda mahakamani alisema: “Nimekwenda mahakamani kutaka haki itendeke. Chama cha kidemokrasia kinanyima vipi mwanachama fursa ya kukata rufaa?

“Nisingekwenda mahakamani kama ningeona haki ikitendeka. Tatizo kubwa la chama chetu sasa kinaongozwa na mawazo ya kihuni na yeyote mwenye mawazo ya kujenga anaonekana msaliti.

>>Mwananchi

CCM yatoa onyo kwa wanachama wake walioanza kupiga kampeni za chini chini kabla ya muda



Chama cha mapinduzi CCM kimetoa onyo kwa baadhi ya wanachama wake wanaoanza kufanya kampeni za chini kwa chini kabla ya muda kutangazwa na kuwataka kuacha mara moja.
 

Akibainisha hayo Jijini Dar es salaam Makamu mwenyekiti wa chama hicho Tanzania bara Philip mangula amesema ibara ya 33 kifungu kidogo cha kanuni za CCM kinakataza mtu yoyote kufanya kampeni za aina yoyote kabla ya tume ya uchaguzi kutangaza.
 

Amesema suala la baadhi ya wanasiasa hususani wanachama wa chama chake kuanza kufanya kampeni kabla ya wakati ni ishara ya viongozi hao kuonesha kuwa na uchu wa madaraka na kuitaka jamii iwaangalie kwa jicho pana.


Aidha katika mkutano wake na waandishi wa habari uliyokuwa unatoa tathimini ya mwaka ya tawi la ccm ofisi ndogo ya chama hicho mangula amesema suala hilo si la kulikalia kimya kwani hata nchi ambazo zinapigana sasa zilianza na chokochoko za namna hiyo.
 

Mangula ambaye muda mwingi alikuwa akizungumza kwa kunukuu baadhi ya vifungu vya sheria na kanuni ya chama hicho anatoa msimamo wa chama chake kwa mtu yoyote atakayeikiuka ama kwenda kinyume na maadili ya msaafu wa chama hicho.
 

Mangula alimalizia kwa kusema kuwa malalamiko mengi yalitolewa katika uchaguzi mkuu uliyopita na tayari baadhi yameshaghulikiwa na akaongeza kwamba tume ya udhibiti na nidhamu imepanga kuwaita baadhi ya watu ambao wanaonekana kuanzisha makundi yanayoweza kukivuruga chama hicho.

Majibu ya Mh.zitto Kabwe kwa kamati kuu ya Chadema, juu ya mashtaka 11 dhidi yake

 
Our Ref: ZZK/12/13 10.12. 2013.
Mh. Katibu MKuu, Chama Cha Demokrasia Na Mendeleo HSE NO 170,
UFIPA STREET, KINONDONI
S. L. P 31191
Dar es Salaam – Tanzania.


YAH: MASHATAKA YA UKIUKWAJI WA KATIBA, KANUNI NA MWONGOZO WA CHAMA.

Rejea barua yako ya tarehe 26 Novemba 2013 yenye kumbukumbu no C/HQ/ADM/KK/08/31 Iliyoelezea maamuzi yaliyofikiwa na kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha tarehe 20-22 Novemba 2013, kiliazimia kwamba niachishwe nafasi zote za uongozi ninazoshikilia katika chama na kwamba Kamati Kuu iliazimia kwamba hatua zaidi za kinidhamu za kuachishwa ama kufukuzwa uanachama zichukuliwe dhidi yangu kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji za 6.5.2(d), ningependa kuwasilisha majibu ya mashtaka hayo kama ifuatavyo;

1.0 MAELEZO YA AWALI;Napenda kuwasilisha utetezi wangu huku nikiwa napinga utaratibu uliotumika kuandaa na kunifikishia mashtaka husika (Defence Under Protest) kwa sababu zifuatazo;

1.1. Hatua za kinidhamu ambazo kimsingi ni adhabu zimeshachukuliwa na Kamati Kuu kwa mashtaka haya haya ambayo nimepatiwa. Kama barua yako inavyosema na nanukuu maneno yako “Kamati Kuu kwa kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa Kanuni ya 6.5.2(d) ya Kanuni za Uendeshaji Shughuli za Chama (‘Kanuni za Uendeshaji’), iliazimia kwamba muachishwe nafasi zote za uongozi mnazoshikilia katika Chama…” (msisitizo ni wangu).Mheshimiwa Katibu Mkuu;Ni wazi kabisa kwamba adhabu ya kuachishwa nafasi zote za uongozi imeshatekelezwa. Kamati Kuu imeshanitia hatiani kwa makosa haya haya ambayo sasa hivi natakiwa nijitetee. Binafsi siamini kwamba kwa utaratibu huu haki itatendeka na inaonekana kutendeka. Ni vigumu sana kusema kwamba haki yangu ya msingi ya kusikilizwa na kujitetea imelindwa wakati tayari adhabu imeshatolewa na chombo kile kile ninachotakiwa kujitetea mbele yake.

1.2. Kama kiongozi ambaye nimeadhibiwa na Kamati Kuu ninayo haki ya kukata rufaa Baraza Kuu dhidi ya haya yafuatayo;
1.2.1. utaratibu uliotumika na Kamati Kuu kunivua nyadhifa zote za uongozi.
1.2.2. sababu zilizotumika kunivua nyadhifa zote za uongozi.

Mheshimiwa Katibu Mkuu;

Katiba ya Chama pamoja na Kanuni za Uendeshaji zinatoa HAKI hii ya msingi na UTARATIBU kwa maneno haya;

Ibara 6.3.6(d) ya Katiba ya Chama;“Kiongozi aliyechukuliwa hatua za kinidhamu na mamlaka yake ya nidhamu anayo haki ya kukata rufaa ngazi ya juu ya ile mamlaka yake ya nidhamu na uamuzi wa ngazi hiyo utakuwa wa mwisho”.

Ibara 6.3.6(e) ya Katiba ya Chama;“Rufaa yoyote lazima ifanyike katika muda wa siku thelathini tangu tarehe ya kupokea rasmi kwa maandishi maamuzi ya mamlaka iliyotoa adhabu”.Mheshimiwa Katibu Mkuu;Kanuni za Uendeshaji zinatoa UTARATIBU ambao unatakiwa ufuatwe ili kiongozi aliyeadhibiwa aweze kutumia HAKI yake ya kukata rufani kwa maneno haya;Kanuni ya 6.5.8 ya Kanuni za Uendeshaji;“Kiongozi aliyeadhibiwa atapewa taarifa ya msingi wa maamuzi ya mamlaka ya nidhamu ili kumuwezesha kuamua kukata rufani au la”

Kanuni ya 6.5.9 ya Kanuni za Uendeshaji;“Mwadhibiwa atakayeamua kukata rufani atatakiwa kufanya hivyo katika muda wa siku thelathini baada ya kuarifiwa uamuzi wa adhabuKanuni ya 6.5.10 ya Kanuni za Uendeshaji;“Baada ya kutoa uamuzi kikao husika kinalazimika kuandaa taarifa kamili ya mwenendo wa shauri na kuwasilisha ngazi ya juu. Taarifa hiyo lazima ifike katika muda wa siku kumi na nne baada ya kikao cha mamuzi
 
Mheshimiwa Katibu Mkuu;
Mpaka tarehe 01/12/2013 siku ambayo nimepokea barua yako ya mashtaka dhidi yangu sijapokea taarifa ya msingi wa maamuzi ya mamlaka ya nidhamu na pia taarifa kamili ya mwenendo wa shauri langu haujawasilishwa Baraza Kuu. Wakati hayo yote hayajafanyika natakiwa kutoa utetezi wangu wa maandishi kwa mujibu wa Kanuni ya 6.5.2(a) ikisomwa pamoja na Kanuni ya 6.5.6 ya Kanuni za Uendeshaji kwa makosa yaleyale ambayo tayari nimeshaadhibiwa na Kamati Kuu. Ni wazi kabisa kwamba barua yako ya mashtaka ni muendelezo wa hatua au maazimio ya Kamati Kuu kama ilivyoandikwa “Aidha Kamati Kuu iliazimia kwamba hatua zaidi za kinidhamu za kuachishwa ama kufukuzwa uanachama zichukuliwe….”

Mheshimiwa Katibu Mkuu;

Utaratibu uliotumika na Kamati Kuu sio wa HAKI na ni ukiukaji wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji. Nalazimika kutoa utetezi wangu nikiwa napinga (under protest) kwa sababu kwa Chama ambacho kinasifika kwa kupigania misingi ya utawala bora na utawala wa sheria ni lazima kiheshimu haki za wanachama na viongozi wake pamoja na kufuata utaratibu kilichojiwekea wakati wa kuchukua hatua za kinidhamu.1.3. Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu kwa nyakati mbalimbali wametoa matamko kwamba tumefukuzwa uongozi na hatua zaidi zitachukuliwa dhidi yetu kabla hata ya ofisi yako kutoa Mashtaka dhidi yetu. Mheshimiwa Tundu Lissu na Mheshimiwa John Mnyika walitoa matamko hayo wakati wakiongea na Waandishi wa Habari.

Mheshimiwa Katibu Mkuu;

Kitendo cha wajumbe hao kutoa misimamo kwa niaba ya Chama au Kamati Kuu ni ukiukwaji wa haki yangu ya msingi ya kusikilizwa. Ni wazi kabisa kwamba tayari hukumu dhidi yangu imeshapitishwa kabla sijasikilizwa. Sina imani na wajumbe ambao tayari wameonyesha waziwazi misimamo yao kuhusu tuhuma dhidi yangu.
Mheshimiwa Katibu Mkuu;

Kutokana na hayo yote ambayo nimeyataja hapo juu naomba ofisi yako isitishe utekelazaji wa maamuzi au maazimio ya Kamati Kuu mpaka pale ambapo nitakuwa nimepatiwa taarifa ya msingi wa maamuzi ya Kamati Kuu na kuweza kukata rufaa ngazi ya juu kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji. Hatua zozote za Kamati Kuu zitaendelea kukiuka Katiba na Kanuni za Uendeshaji.

Bila kuathiri hayo niliyoyasema;

1 UTETEZI WANGU DHIDI YA MASHTAKAMheshimiwa Katibu Mkuu;Kwa ujumla nakanusha na kukataa kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwangu kuhusu kinachoelezwa kwamba niliandaa mkakati wa mabadiliko 2013, mimi binafsi sijawahi kushiriki, kuhusika kuandaa au kufahamu kwa namna yoyote ile kinachoitwa waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 kama ulivyoainisha kwenye barua yako.

KOSA LA KWANZA

Kukashifu Chama kiongozi au mwanachama yeyote wa chama kinyume na masharti ya 10.1(xii) ya Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa waraka ulioitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013. 
 
2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kumkashifu Mwenyekiti wa Chama Taifa kwa njia yoyote ile.

3. Kuhusu kutoa kashfa kwa Katibu Katibu Mkuu wa Chama na Mbunge wa Arusha Mjini Mh. Godbles Lema kama ulivyoainisha kwenye barua yako mimi binafsi sijawahi kutoa kashfa hizo na wala kuhusika kwa namna yoyote ile kwenye maandalizi ya mkakati huo wa mabadiliko.

KOSA LA PILI

Kutokuwa wakweli na wawazi wakati wote na kushirikiana na vikundi vya majungu na wadanganyifu (rumour mongers) Kinyume na Kanuni ya Uendeshaji 10.1 (vii) ya Kanuni za Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana nilianzisha mtandao wa siri ulioitwa “Mtandao wa Ushindi’ ili kuniwezesha mimi kutwaa madaraka ya Mwenyekiti wa Chama Taifa kwa njia zilizo kinyume na Katiba, Kanuni za Uendeshaji na Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili ya Wabunge wa CHADEMA na Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali 2012.

2. Nakanusha kuanzisha, kushiriki uanzishwaji au kuufahamu unaoitwa mtandao wa ushindi kama ilivyoelezwa na barua yako.
 
3. Siku zote nimekuwa mkweli muwazi kwa yale ninayoyaamini na katika kutekeleza majukumu yangu kama kiongozi na mwanachama mtiifu wa CHADEMA. Pia sijashirikiana na kikundi chochote cha majungu au wadanganyifu kama iliyoainishwa kwenye barua yako.
KOSA LA TATU

Kutoa tuhuma juu ya viongozi wenzenu pasipo kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa kwenye Kanuni kinyume na Kanuni ya 10.1(x) ya Kanuni za Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana nilitoa tuhuma nzito na za uongo dhidi ya viongozi wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa na Katibu Mkuu pasipo kupitia vikao halali na bila kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa na Kanuni za Uendeshaji.
 
2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kwamba nilitoa tuhuma nzito na za uongo dhidi ya viongozi wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa n Katibu Mkuu pasipo kupitia vikao halali na bila kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa na Kanuni za Uendeshaji.

KOSA LA NNE

Kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana ndani ya chama na miongoni mwa jamii kisiasa au kijamii na Kanuni ya 10.1(iv) ya Kanuni za Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba nimejihusisha katika kuanzisha, kushiriki uanzishwaji au kufahamu kikundi chochote chenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda ambacho kina makusudi ya kubaguana ndani ya chama na miongoni mwa jamii kisiasa au kijamii kwa kutumia waraka unaosemekana kuandaliwa nami.

2. Mimi binafsi sio mdini, mkabila au mkanda na sijawahi kujihusisha na kikundi au mtu yeyote mwenye tabia hizo.

KOSA LA TANO

Kujihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake na kinyume na Kanuni ya 10.1 (x) ya Kanuni za Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba nimejihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake.

2. Mimi binafsi sikifahamu kikundi chochote ambacho nashutumiwa kujihusisha nacho.
KOSA LA SITA

Kutekeleza mpango wa kusudio la kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Chama Taifa bila kutangaza kusudio la kugombea nafasi hiyo kinyume na kifungu cha 2(g) cha Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali 2012.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba nimetekeleza au kuhusika katika utekelezaji wa mpango wa kusudio la kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa bila kutangaza kusudio la kugombea nafasi hiyo.

2. Sijatangaza sehemu yeyote kwamba nitagombea nafasi hiyo na pia vile vile sijatekeleza mpango wowote kama ilivyoelezwa kwenye barua yako.
KOSA LA SABA

Kutengeneza makundi au mitandao ya kuwania uongozi ndani ya chama kwa nia ya kujihakikisha ushindi kinyume nakifungu cha 2(d) cha mwongozo wa kuwania uongozi.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba nimejihusisha katika kutengeneza, kuanzisha, kushiriki uanzishwaji au kufahamu kikundi chochote kwa ajili ya kuniwezesha kuwania uongozi ndani ya chama na kujihakikishia ushindi kutwaa Uenyekiti wa Chama Taifa kinyume na taratibu.

KOSA LA NANE

Kuwachafua viongozi na wanachama wengine wenye kusudio/nia ya kutaka kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Chama Taifa kinyume nakifungu cha 2(e) cha Mwongozo wa Kuwania Uongozi.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa waraka ulioitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013. 

2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kumkashifu Mwenyekiti wa Chama Taifa, kiongozi mwenzangu au mwanachama yeyote Yule.

KOSA LA TISA

Kujihusisha na upinzani dhidi ya Chama na makundi ya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa Uchaguzi wa Chama kinyume na Kanuni ya 10.3(4) ya Kanuni za Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa mkakati wa kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa Uchaguzi wa Chama kwa kuwachafua viongozi wakuu wa Chama yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa na Katibu Mkuu kwa tuhuma nzito za uongo na kunipamba mimi.

2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote.

KOSA LA KUMI

Kukashifu Chama au Kiongozi wa Chama nje ya Bunge kinyume na Kanuni 2(b) ikisomwa pamoja na Kanuni 3(b) ya Kanuni za Mwenendo na Maadili ya Wabunge.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana kwa kuandaa na kutumia waraka uitwao Mkakati wa Mabadiliko 2013 nilitengeneza mtandao haramu ndani ya Chama na nilitoa kashfa, matusi na uzushi dhidi ya Chama na viongozi wake wakuu kwa lengo la kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama.

2. ambao ulikashifu Chama na/au viongozi wake wakuu nikiwa Mbunge wa CHADEMA na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni. 

3. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kwamba nimekashifu Chama au viongozi wake wakuu nikiwa Mbunge wa CHADEMA na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwa njia yoyote ile.

KOSA LA KUMI NA MOJA

Kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama kinyume na Kanuni ya 3(f) ya Kanuni za mwenendo na maadili ya Wabunge.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Mimi kama kiongozi wa Kitaifa sijawahi kutengeneza mtandao haramu ndani ya Chama wala kutoa lugha ya matusi na uzushi dhidi ya Chama na viongozi wake wakuu kwa lengo la kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama.

HITIMISHO:

Mheshimiwa Katibu Mkuu;
a) Nakanusha kila tuhuma mojamoja na kwa ujumla wake dhidi yangu. Mashtaka yote dhidi yangu sio kweli na sijavunja Katiba au Kanuni za Chama.
 
b) Naiomba Kamati Kuu ijiridhishe kwa kiasi kinachostahili kuhusu mashtaka yote niliyoshtakiwa nayo kwa kuangalia ushahidi wote uliotolewa au utakaotolewa dhidi yangu.
 
c) Utetezi wangu umetolewa bila kupewa nakala ya Waraka unaosemekana nimeuandaa ilhali kukiwa na maelezo kwamba kuna waraka ‘feki’ na waraka ‘original’ ambao umetumika na Kamati Kuu kufikia maamuzi yake.
 
d) Ndugu Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba kwa maneno yao wenyewe wametamka kwamba hawakunishirikisa na sikushiriki kwenye uandaaji wa waraka ambao ndio msingi wa mashtaka haya. Kamati Kuu inao ushahidi huo.

Wako katika ujenzi wa Chama,
.............................. ......................
Mh. Zitto Zuberi Kabwe (MB).

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger