Home » , » Mbowe Amjibu Rais Kikwete

Mbowe Amjibu Rais Kikwete


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amemjibu Rais Jakaya Kikwete kwamba asiingize utani katika masuala mazito ya taifa. Mbowe alisema Katiba ya Tanzania, itaamuriwa na wananchi wenyewe na si Chama Cha Mapinduzi (CM) ambacho kimekuwa na mkakati mkali wa kutaka kuua maoni ya wananchi.

Mbowe ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tu baada ya Rais Kikwete kudai amesikia kiongozi huyo wa upinzani akitangaza kutumia nguvu kupata Katiba mpya.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, wakati akihutubia sherehe za miaka 37 ya kuzaliwa CCM. Alisema amesikitishwa na kauli hiyo na kuwataka Watanzania kutobabaishwa.Kikwete alisema Katiba mpya itapatikana kwa hoja za kila upande kulingana na mapendekezo yake.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mbowe alisema Rais Kikwete hapaswi kuchukulia utani katika mambo mazito ya taifa.“Namuomba Rais Kikwete asichukulie utani mambo ya taifa suala la Katiba mpya. Anapaswa kuzungumza mambo ya msingi ambayo yanaleta tija.

“Siku zote Katiba ya nchi inapatikana kwa dhamira nzuri lakini tumebaini wenzetu hawa CCM hawaheshimu hoja za wananchi.“Hebu tujiulize jinsi Jaji Joseph Warioba alivyotumia fedha nyingi kukusanya maoni ya Watanzania, leo CCM hao hao wanayakataa tuwaeleweje?” alihoji Mbowe.

Alisema Jaji Warioba ametoa hoja za msingi lakini kwa sababu ya uoga wa CCM wanataka kupindisha ukweli wa mambo.“Mzee wa watu huyu amezunguka taifa zima kwa fedha za walipa kodi wa nchi hii, sasa wanataka watumie wabunge wao kukwamisha mchakato huu,”alisema Mbowe.

Alisema kama utawala wa Rais Kikwete utashindwa kuleta Katiba mpya ambayo inakidhi matakwa ya Watanzania, wao wataendelea kudai utawala mpya utakapoingia madarakani uwe ni wa Chadema au CCM.
“Nawahakikisha Watanzania, ikija Katiba mbaya tutaendelea kuidai kwa nguvu zote iwe CCM imeingia madarakani au sisi, Kikwete awe madarakani au asiwepo hatulali kamwe. “Katiba ni maridhiano ambayo yanabeba maoni ya Watanzania sasa kwa nini CCM hawataki kuyafuata?” alihoji Mbowe.

Alisema CCM haina hatimiliki ya Katiba mpya na kwamba wakati wa kufanya uamuzi mgumu wa kupindisha maoni ya Watanzania umefika.“Hawa watu hawana hatimiliki ya Katiba mpya, kwa nini wanajawa uoga kiasi hiki? Wanaogopa serikali tatu, nakwambia sitaki utani kwenye ya msingi,”alisema Mbowe.
>>mtanzania
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger