Home » » Majibu ya Mh.zitto Kabwe kwa kamati kuu ya Chadema, juu ya mashtaka 11 dhidi yake

Majibu ya Mh.zitto Kabwe kwa kamati kuu ya Chadema, juu ya mashtaka 11 dhidi yake

 
Our Ref: ZZK/12/13 10.12. 2013.
Mh. Katibu MKuu, Chama Cha Demokrasia Na Mendeleo HSE NO 170,
UFIPA STREET, KINONDONI
S. L. P 31191
Dar es Salaam – Tanzania.


YAH: MASHATAKA YA UKIUKWAJI WA KATIBA, KANUNI NA MWONGOZO WA CHAMA.

Rejea barua yako ya tarehe 26 Novemba 2013 yenye kumbukumbu no C/HQ/ADM/KK/08/31 Iliyoelezea maamuzi yaliyofikiwa na kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha tarehe 20-22 Novemba 2013, kiliazimia kwamba niachishwe nafasi zote za uongozi ninazoshikilia katika chama na kwamba Kamati Kuu iliazimia kwamba hatua zaidi za kinidhamu za kuachishwa ama kufukuzwa uanachama zichukuliwe dhidi yangu kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji za 6.5.2(d), ningependa kuwasilisha majibu ya mashtaka hayo kama ifuatavyo;

1.0 MAELEZO YA AWALI;Napenda kuwasilisha utetezi wangu huku nikiwa napinga utaratibu uliotumika kuandaa na kunifikishia mashtaka husika (Defence Under Protest) kwa sababu zifuatazo;

1.1. Hatua za kinidhamu ambazo kimsingi ni adhabu zimeshachukuliwa na Kamati Kuu kwa mashtaka haya haya ambayo nimepatiwa. Kama barua yako inavyosema na nanukuu maneno yako “Kamati Kuu kwa kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa Kanuni ya 6.5.2(d) ya Kanuni za Uendeshaji Shughuli za Chama (‘Kanuni za Uendeshaji’), iliazimia kwamba muachishwe nafasi zote za uongozi mnazoshikilia katika Chama…” (msisitizo ni wangu).Mheshimiwa Katibu Mkuu;Ni wazi kabisa kwamba adhabu ya kuachishwa nafasi zote za uongozi imeshatekelezwa. Kamati Kuu imeshanitia hatiani kwa makosa haya haya ambayo sasa hivi natakiwa nijitetee. Binafsi siamini kwamba kwa utaratibu huu haki itatendeka na inaonekana kutendeka. Ni vigumu sana kusema kwamba haki yangu ya msingi ya kusikilizwa na kujitetea imelindwa wakati tayari adhabu imeshatolewa na chombo kile kile ninachotakiwa kujitetea mbele yake.

1.2. Kama kiongozi ambaye nimeadhibiwa na Kamati Kuu ninayo haki ya kukata rufaa Baraza Kuu dhidi ya haya yafuatayo;
1.2.1. utaratibu uliotumika na Kamati Kuu kunivua nyadhifa zote za uongozi.
1.2.2. sababu zilizotumika kunivua nyadhifa zote za uongozi.

Mheshimiwa Katibu Mkuu;

Katiba ya Chama pamoja na Kanuni za Uendeshaji zinatoa HAKI hii ya msingi na UTARATIBU kwa maneno haya;

Ibara 6.3.6(d) ya Katiba ya Chama;“Kiongozi aliyechukuliwa hatua za kinidhamu na mamlaka yake ya nidhamu anayo haki ya kukata rufaa ngazi ya juu ya ile mamlaka yake ya nidhamu na uamuzi wa ngazi hiyo utakuwa wa mwisho”.

Ibara 6.3.6(e) ya Katiba ya Chama;“Rufaa yoyote lazima ifanyike katika muda wa siku thelathini tangu tarehe ya kupokea rasmi kwa maandishi maamuzi ya mamlaka iliyotoa adhabu”.Mheshimiwa Katibu Mkuu;Kanuni za Uendeshaji zinatoa UTARATIBU ambao unatakiwa ufuatwe ili kiongozi aliyeadhibiwa aweze kutumia HAKI yake ya kukata rufani kwa maneno haya;Kanuni ya 6.5.8 ya Kanuni za Uendeshaji;“Kiongozi aliyeadhibiwa atapewa taarifa ya msingi wa maamuzi ya mamlaka ya nidhamu ili kumuwezesha kuamua kukata rufani au la”

Kanuni ya 6.5.9 ya Kanuni za Uendeshaji;“Mwadhibiwa atakayeamua kukata rufani atatakiwa kufanya hivyo katika muda wa siku thelathini baada ya kuarifiwa uamuzi wa adhabuKanuni ya 6.5.10 ya Kanuni za Uendeshaji;“Baada ya kutoa uamuzi kikao husika kinalazimika kuandaa taarifa kamili ya mwenendo wa shauri na kuwasilisha ngazi ya juu. Taarifa hiyo lazima ifike katika muda wa siku kumi na nne baada ya kikao cha mamuzi
 
Mheshimiwa Katibu Mkuu;
Mpaka tarehe 01/12/2013 siku ambayo nimepokea barua yako ya mashtaka dhidi yangu sijapokea taarifa ya msingi wa maamuzi ya mamlaka ya nidhamu na pia taarifa kamili ya mwenendo wa shauri langu haujawasilishwa Baraza Kuu. Wakati hayo yote hayajafanyika natakiwa kutoa utetezi wangu wa maandishi kwa mujibu wa Kanuni ya 6.5.2(a) ikisomwa pamoja na Kanuni ya 6.5.6 ya Kanuni za Uendeshaji kwa makosa yaleyale ambayo tayari nimeshaadhibiwa na Kamati Kuu. Ni wazi kabisa kwamba barua yako ya mashtaka ni muendelezo wa hatua au maazimio ya Kamati Kuu kama ilivyoandikwa “Aidha Kamati Kuu iliazimia kwamba hatua zaidi za kinidhamu za kuachishwa ama kufukuzwa uanachama zichukuliwe….”

Mheshimiwa Katibu Mkuu;

Utaratibu uliotumika na Kamati Kuu sio wa HAKI na ni ukiukaji wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji. Nalazimika kutoa utetezi wangu nikiwa napinga (under protest) kwa sababu kwa Chama ambacho kinasifika kwa kupigania misingi ya utawala bora na utawala wa sheria ni lazima kiheshimu haki za wanachama na viongozi wake pamoja na kufuata utaratibu kilichojiwekea wakati wa kuchukua hatua za kinidhamu.1.3. Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu kwa nyakati mbalimbali wametoa matamko kwamba tumefukuzwa uongozi na hatua zaidi zitachukuliwa dhidi yetu kabla hata ya ofisi yako kutoa Mashtaka dhidi yetu. Mheshimiwa Tundu Lissu na Mheshimiwa John Mnyika walitoa matamko hayo wakati wakiongea na Waandishi wa Habari.

Mheshimiwa Katibu Mkuu;

Kitendo cha wajumbe hao kutoa misimamo kwa niaba ya Chama au Kamati Kuu ni ukiukwaji wa haki yangu ya msingi ya kusikilizwa. Ni wazi kabisa kwamba tayari hukumu dhidi yangu imeshapitishwa kabla sijasikilizwa. Sina imani na wajumbe ambao tayari wameonyesha waziwazi misimamo yao kuhusu tuhuma dhidi yangu.
Mheshimiwa Katibu Mkuu;

Kutokana na hayo yote ambayo nimeyataja hapo juu naomba ofisi yako isitishe utekelazaji wa maamuzi au maazimio ya Kamati Kuu mpaka pale ambapo nitakuwa nimepatiwa taarifa ya msingi wa maamuzi ya Kamati Kuu na kuweza kukata rufaa ngazi ya juu kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji. Hatua zozote za Kamati Kuu zitaendelea kukiuka Katiba na Kanuni za Uendeshaji.

Bila kuathiri hayo niliyoyasema;

1 UTETEZI WANGU DHIDI YA MASHTAKAMheshimiwa Katibu Mkuu;Kwa ujumla nakanusha na kukataa kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwangu kuhusu kinachoelezwa kwamba niliandaa mkakati wa mabadiliko 2013, mimi binafsi sijawahi kushiriki, kuhusika kuandaa au kufahamu kwa namna yoyote ile kinachoitwa waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 kama ulivyoainisha kwenye barua yako.

KOSA LA KWANZA

Kukashifu Chama kiongozi au mwanachama yeyote wa chama kinyume na masharti ya 10.1(xii) ya Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa waraka ulioitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013. 
 
2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kumkashifu Mwenyekiti wa Chama Taifa kwa njia yoyote ile.

3. Kuhusu kutoa kashfa kwa Katibu Katibu Mkuu wa Chama na Mbunge wa Arusha Mjini Mh. Godbles Lema kama ulivyoainisha kwenye barua yako mimi binafsi sijawahi kutoa kashfa hizo na wala kuhusika kwa namna yoyote ile kwenye maandalizi ya mkakati huo wa mabadiliko.

KOSA LA PILI

Kutokuwa wakweli na wawazi wakati wote na kushirikiana na vikundi vya majungu na wadanganyifu (rumour mongers) Kinyume na Kanuni ya Uendeshaji 10.1 (vii) ya Kanuni za Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana nilianzisha mtandao wa siri ulioitwa “Mtandao wa Ushindi’ ili kuniwezesha mimi kutwaa madaraka ya Mwenyekiti wa Chama Taifa kwa njia zilizo kinyume na Katiba, Kanuni za Uendeshaji na Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili ya Wabunge wa CHADEMA na Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali 2012.

2. Nakanusha kuanzisha, kushiriki uanzishwaji au kuufahamu unaoitwa mtandao wa ushindi kama ilivyoelezwa na barua yako.
 
3. Siku zote nimekuwa mkweli muwazi kwa yale ninayoyaamini na katika kutekeleza majukumu yangu kama kiongozi na mwanachama mtiifu wa CHADEMA. Pia sijashirikiana na kikundi chochote cha majungu au wadanganyifu kama iliyoainishwa kwenye barua yako.
KOSA LA TATU

Kutoa tuhuma juu ya viongozi wenzenu pasipo kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa kwenye Kanuni kinyume na Kanuni ya 10.1(x) ya Kanuni za Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana nilitoa tuhuma nzito na za uongo dhidi ya viongozi wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa na Katibu Mkuu pasipo kupitia vikao halali na bila kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa na Kanuni za Uendeshaji.
 
2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kwamba nilitoa tuhuma nzito na za uongo dhidi ya viongozi wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa n Katibu Mkuu pasipo kupitia vikao halali na bila kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa na Kanuni za Uendeshaji.

KOSA LA NNE

Kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana ndani ya chama na miongoni mwa jamii kisiasa au kijamii na Kanuni ya 10.1(iv) ya Kanuni za Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba nimejihusisha katika kuanzisha, kushiriki uanzishwaji au kufahamu kikundi chochote chenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda ambacho kina makusudi ya kubaguana ndani ya chama na miongoni mwa jamii kisiasa au kijamii kwa kutumia waraka unaosemekana kuandaliwa nami.

2. Mimi binafsi sio mdini, mkabila au mkanda na sijawahi kujihusisha na kikundi au mtu yeyote mwenye tabia hizo.

KOSA LA TANO

Kujihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake na kinyume na Kanuni ya 10.1 (x) ya Kanuni za Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba nimejihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake.

2. Mimi binafsi sikifahamu kikundi chochote ambacho nashutumiwa kujihusisha nacho.
KOSA LA SITA

Kutekeleza mpango wa kusudio la kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Chama Taifa bila kutangaza kusudio la kugombea nafasi hiyo kinyume na kifungu cha 2(g) cha Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali 2012.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba nimetekeleza au kuhusika katika utekelezaji wa mpango wa kusudio la kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa bila kutangaza kusudio la kugombea nafasi hiyo.

2. Sijatangaza sehemu yeyote kwamba nitagombea nafasi hiyo na pia vile vile sijatekeleza mpango wowote kama ilivyoelezwa kwenye barua yako.
KOSA LA SABA

Kutengeneza makundi au mitandao ya kuwania uongozi ndani ya chama kwa nia ya kujihakikisha ushindi kinyume nakifungu cha 2(d) cha mwongozo wa kuwania uongozi.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba nimejihusisha katika kutengeneza, kuanzisha, kushiriki uanzishwaji au kufahamu kikundi chochote kwa ajili ya kuniwezesha kuwania uongozi ndani ya chama na kujihakikishia ushindi kutwaa Uenyekiti wa Chama Taifa kinyume na taratibu.

KOSA LA NANE

Kuwachafua viongozi na wanachama wengine wenye kusudio/nia ya kutaka kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Chama Taifa kinyume nakifungu cha 2(e) cha Mwongozo wa Kuwania Uongozi.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa waraka ulioitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013. 

2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kumkashifu Mwenyekiti wa Chama Taifa, kiongozi mwenzangu au mwanachama yeyote Yule.

KOSA LA TISA

Kujihusisha na upinzani dhidi ya Chama na makundi ya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa Uchaguzi wa Chama kinyume na Kanuni ya 10.3(4) ya Kanuni za Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa mkakati wa kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa Uchaguzi wa Chama kwa kuwachafua viongozi wakuu wa Chama yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa na Katibu Mkuu kwa tuhuma nzito za uongo na kunipamba mimi.

2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote.

KOSA LA KUMI

Kukashifu Chama au Kiongozi wa Chama nje ya Bunge kinyume na Kanuni 2(b) ikisomwa pamoja na Kanuni 3(b) ya Kanuni za Mwenendo na Maadili ya Wabunge.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana kwa kuandaa na kutumia waraka uitwao Mkakati wa Mabadiliko 2013 nilitengeneza mtandao haramu ndani ya Chama na nilitoa kashfa, matusi na uzushi dhidi ya Chama na viongozi wake wakuu kwa lengo la kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama.

2. ambao ulikashifu Chama na/au viongozi wake wakuu nikiwa Mbunge wa CHADEMA na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni. 

3. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kwamba nimekashifu Chama au viongozi wake wakuu nikiwa Mbunge wa CHADEMA na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwa njia yoyote ile.

KOSA LA KUMI NA MOJA

Kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama kinyume na Kanuni ya 3(f) ya Kanuni za mwenendo na maadili ya Wabunge.Mheshimiwa Katibu Mkuu;

1. Mimi kama kiongozi wa Kitaifa sijawahi kutengeneza mtandao haramu ndani ya Chama wala kutoa lugha ya matusi na uzushi dhidi ya Chama na viongozi wake wakuu kwa lengo la kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama.

HITIMISHO:

Mheshimiwa Katibu Mkuu;
a) Nakanusha kila tuhuma mojamoja na kwa ujumla wake dhidi yangu. Mashtaka yote dhidi yangu sio kweli na sijavunja Katiba au Kanuni za Chama.
 
b) Naiomba Kamati Kuu ijiridhishe kwa kiasi kinachostahili kuhusu mashtaka yote niliyoshtakiwa nayo kwa kuangalia ushahidi wote uliotolewa au utakaotolewa dhidi yangu.
 
c) Utetezi wangu umetolewa bila kupewa nakala ya Waraka unaosemekana nimeuandaa ilhali kukiwa na maelezo kwamba kuna waraka ‘feki’ na waraka ‘original’ ambao umetumika na Kamati Kuu kufikia maamuzi yake.
 
d) Ndugu Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba kwa maneno yao wenyewe wametamka kwamba hawakunishirikisa na sikushiriki kwenye uandaaji wa waraka ambao ndio msingi wa mashtaka haya. Kamati Kuu inao ushahidi huo.

Wako katika ujenzi wa Chama,
.............................. ......................
Mh. Zitto Zuberi Kabwe (MB).

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger