Home » » CHADEMA watwangana ngumi tena.....Awamu hii ni ndani ya kikao kilichokuwa kikiendeshwa na Freeman Mbowe

CHADEMA watwangana ngumi tena.....Awamu hii ni ndani ya kikao kilichokuwa kikiendeshwa na Freeman Mbowe


 
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Shaaban Mwamba, juzi usiku alipata kipigo kutoka kwa maofisa wa  kikundi cha ulinzi cha chama hicho waliokuwa katika eneo ambalo mkutano wa Kamati Kuu ulifanyika, baada ya kutuhumiwa alikuwa akiwasiliana na wafuasi wa Zitto.
 
Taarifa kutoka kwa mjumbe mmoja ambaye hakupenda jina lake litajwe, ilisema kuwa mtu huyo alikuwa akichunguzwa na maofisa wa ulinzi wa chama hicho muda mrefu, kutokana na nyendo alizokuwa akizionyesha zilizotia shaka.
 
Mwandishi wa habari hizi ambaye alikuwa katika eneo hilo, alishuhudia kiongozi huyo akibebwa juu juu na maofisa hao, huku akiulizwa aliyekuwa akiwasiliana naye ni nani, kabla ya vijana wengine wa chama kumkamata na kumweka chini ya ulinzi, wakimtaka atoe ufafanuzi wa alichokuwa anakifanya.
 
Baada ya mahojiano ya muda mfupi, kiongozi huyo alionekana akiinuka na kwenda  kunawa kwenye bomba la maji, huku akitokwa damu mdomoni.
 
Taarifa zilizopatikana baadaye zilidai kuwa kiongozi huyo alikuwa akiwasiliana na mama yake Zitto na Katibu wa Zitto, Dk Alex na kwamba pia simu yake ilikutwa na ujumbe mfupi aliokuwa amewaandikia watu hao.
 
Mwandishi wetu alijaribu kumtafuta kiongozi huyo ili kueleza sababu ya kupigwa kwake, lakini hakupatikana eneo la mkutano kwa madai kuwa alikwenda hospitali kupata huduma ya kwanza, lakini hakurudi.

Wakati hatima ya  Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe  ikisubiriwa kujulikana hapo kesho baada ya Mahakama kutoa hukumu yake, inadaiwa kuwa baadhi wa wabunge, viongozi na wazee wa Chadema, wanataka suala hilo liishe mapema.
 
Habari ambazo zilipatikana  jana zilisema kuwa baadhi ya viongozi hao walitaka Zitto aende Halmashauri Kuu ya Chadema na kuomba msamaha ili mambo yaishe.
 
“Walimfuata Kitila (Dk Kitila Mkumbo) wakamwambia amshawishi Zitto ili mambo yaishe nje ya mahakama, wanataka aende kwenye Halmashauri Kuu kuomba radhi. Kitila akawaambia kuomba radhi kwa kosa gani?” kiilisema chanzo hicho.

Hata hivyo, Zitto aliiambia Mwananchi jana kuwa kumekuwa na jitihada  mbalimbali za wazee kutaka kukiepusha chama hicho na migogoro na kuwa amekuwa tayari kwa suala hilo. “Wazee walikuwa na wajibu wa kuhakikisha hatufiki hapa tulipofika. Sijui kama fursa hiyo bado ipo,” alisema Zitto.
 
Kuhusu uamuzi wake wa kwenda mahakamani alisema: “Nimekwenda mahakamani kutaka haki itendeke. Chama cha kidemokrasia kinanyima vipi mwanachama fursa ya kukata rufaa?

“Nisingekwenda mahakamani kama ningeona haki ikitendeka. Tatizo kubwa la chama chetu sasa kinaongozwa na mawazo ya kihuni na yeyote mwenye mawazo ya kujenga anaonekana msaliti.

>>Mwananchi
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger