Chama cha mapinduzi CCM kimetoa onyo kwa baadhi ya wanachama wake wanaoanza kufanya kampeni za chini kwa chini kabla ya muda kutangazwa na kuwataka kuacha mara moja.
Akibainisha hayo Jijini Dar es salaam Makamu mwenyekiti wa chama hicho Tanzania bara Philip mangula amesema ibara ya 33 kifungu kidogo cha kanuni za CCM kinakataza mtu yoyote kufanya kampeni za aina yoyote kabla ya tume ya uchaguzi kutangaza.
Amesema suala la baadhi ya wanasiasa hususani wanachama wa chama chake kuanza kufanya kampeni kabla ya wakati ni ishara ya viongozi hao kuonesha kuwa na uchu wa madaraka na kuitaka jamii iwaangalie kwa jicho pana.
Aidha katika mkutano wake na waandishi wa habari uliyokuwa unatoa tathimini ya mwaka ya tawi la ccm ofisi ndogo ya chama hicho mangula amesema suala hilo si la kulikalia kimya kwani hata nchi ambazo zinapigana sasa zilianza na chokochoko za namna hiyo.
Mangula ambaye muda mwingi alikuwa akizungumza kwa kunukuu baadhi ya vifungu vya sheria na kanuni ya chama hicho anatoa msimamo wa chama chake kwa mtu yoyote atakayeikiuka ama kwenda kinyume na maadili ya msaafu wa chama hicho.
Mangula alimalizia kwa kusema kuwa malalamiko mengi yalitolewa katika uchaguzi mkuu uliyopita na tayari baadhi yameshaghulikiwa na akaongeza kwamba tume ya udhibiti na nidhamu imepanga kuwaita baadhi ya watu ambao wanaonekana kuanzisha makundi yanayoweza kukivuruga chama hicho.