Home » » MAONI: Udhamini zaidi unahitajika Ligi Kuu Bara

MAONI: Udhamini zaidi unahitajika Ligi Kuu Bara



 Simba inaivaa Yanga katika Ligi Kuu ya soka Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Oktoba 20, mwaka huu.

KAZI nzuri imefanyika katika Ligi Kuu Bara ambayo sasa udhamini wake unafikia kiasi cha Sh 3.3 bilioni.
Hizi ni fedha nyingi na zinaleta matumaini kwa mashabiki wa soka, lakini pia ni kielelezo cha kazi nzuri iliyofanywa katika kushawishi wadhamini wakubali kuiunga mkono ligi hii ambayo ni mhimili muhimu wa soka la Tanzania.
Wadhamini hao ni pamoja na Kampuni ya Simu ya Vodacom Tanzania ambayo inatoa Sh 1.7 Bilioni pamoja na Azam Media ambao wanatoa kiasi cha Sh 1.68 bilioni kwa msimu.
Kutokana na udhamini huo, kila klabu ya Ligi Kuu inajipatia kiasi cha Sh 165 Milioni kwa mwaka.
Kupatikana kwa fedha hizo kunaweza kumfanya shabiki au kiongozi wa klabu ajiulize hali ingekuwaje bila ya udhamini? Je, ligi yetu ingekuwa katika mazingira gani?
Swali la aina hiyo maana yake ni kwamba udhamini uliopo sasa katika Ligi Kuu ni faraja ya kipekee kwa klabu, mashabiki, wanasoka na maendeleo ya soka la Tanzania.
Hata hivyo pamoja na ukweli huo bado viongozi wa klabu na wale wa TFF hawana sababu ya kubweteka na kuona kazi waliyoifanya inatosha na kwamba ziada haihitajiki.
Ni kutokana na hilo ndiyo maana tunawahimiza viongozi wa klabu wakishirikiana na wale wa TFF kuhakikisha kwamba udhamini katika Ligi Kuu Bara unaongezwa na kuwa mkubwa zaidi ya huu tunaojivunia sasa.
Kwamba badala ya klabu kupata Sh 165 milioni kwa msimu, ifikie zaidi ya Sh 300 milioni kwa msimu au hata zaidi.
Kuongezeka kwa ufadhili kuna maana kubwa katika maendeleo ya mpira na hivyo kuwa na msaada mkubwa katika timu yetu ya Taifa. Wachezaji watalipwa vizuri, waamuzi watalipwa vizuri, makocha watalipwa vizuri na kila anayehusika katika soka na hivyo kuleta ushindani wa kweli.
Tukitaka Ligi Kuu Bara iwe na ushindani ni lazima tuwahamasishe wanaohusika kuanzia wachezaji kwa malipo mazuri, kuwaweka katika kambi nzuri, vitu vitakavyowezekana tu pale tutakapoongeza udhamini.
Tunaamini juhudi za dhati zikifanyika udhamini unaweza kuongezeka tena kwa kiasi kikubwa tu. Bado kuna kampuni za vinywaji kama vile soda ambazo zinaweza kudhamini ligi.

-MwanaSport

0
Share



 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger