ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni, amenyang’anywa gari aina ya Toyota Mark 11 GX 110 alilopewa na uongozi wa timu hiyo akiwa anakinoa kikosi hicho.
Kocha huyo hivi karibuni alisimamishwa na uongozi wa timu hiyo yeye na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, kabla ya yeye mwenyewe kutangaza kujiuzulu kuendelea kukinoa kikosi hicho.
Tetesi zilizopo hivi sasa ni kwamba, gari hilo anatarajiwa kupewa kocha mpya wa timu hiyo, Zdravok Logarusic, raia wa Croatia, aliyetua jijini Dar es Salaam jana asubuhi.
Kocha huyo anatarajiwa kukabidhi gari wakati wowote kuanzia hivi sasa, mara baada ya kukamilisha baadhi ya vitu, ikiwemo kusaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo.
Uongozi huo utampa kocha huyo gari hilo kwa ajili ya matumizi ya timu na binafsi katika mizunguko yake mbalimbali nchini.
Gari hilo analotarajiwa kupewa, awali lilikuwa likitumiwa na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Milovan Cirkovic, raia wa Serbia, kabla hajatimuliwa.
Alipotafutwa Kibadeni kuzungumzia hilo, alisema: “Nimeshakabidhi kila kitu kwa Simba, sitaki kuzungumza masuala yoyote ya timu hiyo kwa sasa.”