Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha amesema licha ya kuvuliwa uwaziri ataendelea kuwa kiongozi wa kisiasa na kukitumikia chama chake na wananchi bila ya kuvunjika moyo.
Nahodha, ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa ametoa kauli hiyo siku chache baada ya kuondolewa kwenye Baraza la Mawaziri na Rais Jakaya Kikwete
kutokana na matatizo yaliyotokea katika utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza Ujangili.
Akihutubia wanachama wa CCM waliomlaki na
kumsikiliza kwenye Ofisi ya chama hicho Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja
jana, Nahodha alisema yaliyomtokea ni mambo ya kawaida katika medani za
utumishi wa umma.
“Pamoja na hayo yaliyotokea, nitaendelea
kulitumikia taifa, chama changu na wananchi kwa uaminifu, juhudi na
uwezo wangu wote,” alisema Nahodha, ambaye pia ni Mwakilishi wa
Mwanakerekwe.
Alisema amewajibika serikalini kutokana na matakwa
ya wajibu katika utendaji wa pamoja na kusema kitendo hicho ni mfano wa
ajali inayoweza kumkuta mtu yeyote katika safari ya maisha.
“Sina kinyongo wala muhali, yaliyotokea ni mambo
ya kawaida katika medani za uongozi, wajibu na dhati yangu ni kuwa mtii
kwa Serikali zote. Pia kuitumikia CCM na kushirikiana na wananchi
wenzangu. Binadamu hawezi kujiepusha na mitihani, ”alisema Nahodha.
Alisema alikabidhiwa dhamana na viongozi wake ili
kulitumikia taifa na kutimiza wajibu ipasavyo katika nyadhifa mbalimbali
na yaliyomtokea ameyapokea kwa mikono miwili na hana kinyongo.
Mawaziri walioenguliwa pamoja na Nahodha ni Dk
Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Dk Mathayo David (Mifugo na Maendeleo
ya Uvuvi) na Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii).
Mapinduzi ya Zanzibar
Akizungumzia Mapinduzi ya Zanzibar, Nahodha
alisema ni ufunguo uliofungua milango ya fursa kwa wananchi wanyonge
waliokandamizwa na ukoloni huku akisifu uongozi kwa miaka minane wa Rais
wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Mzee Abeid Amani Karume.
Alisema kiongozi huyo licha ya kuongoza Mapinduzi
ya Januari 12, 1964, aliifanyia mema Zanzibar na watu wake katika
kuwaletea maendeleo na kwamba atakumbukwa na vizazi vyote hadi mwisho wa
dunia.
“Kufanya Mapinduzi haikuwa kazi nyepesi. Waliofanya walikuwa ni
majasiri na wazalendo. Juhudi zao ni matunda haya leo baada ya miaka 50
kupita nchi ikiwa katika utulivu na amani,” alisema Nahodha, ambaye
alikuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar kuanzia mwaka 2000 hadi 2010.
“Uongozi wa Mzee Karume ni mfano wa aina yake,
mwaka 1964 hadi 1972 aliiletea mabadiliko makubwa Zanzibar. Alijenga
viwanda, makazi bora, elimu bila malipo, barabara na kuimarisha huduma
za jamii,” alisema Nahodha.
“Nasikia kuna watu hawataki kulisikia neno
Mapinduzi, hao ni wapuuzi na wapuuzeni. Mapinduzi na Muungano ni uti
wetu wa mgongo, Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Karume waliona mbali,
tusibeze mitazamo yao kwa tamaa za madaraka,” alisema.
Kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Nahodha
alisema angependa ubaki katika mfumo na Serikali mbili na kusema pamoja
na uzuri wake, zipo changamoto na kasoro zinazohitaji kurekebishwa na
kuwa na muungano wenye nguvu za kiuchumi.
Alisema kazi ya kurekebisha makosa ni nyepesi
lakini wazo la kuvunja Muungano lina gharama kubwa kuliko inavyofikiriwa
na baadhi ya watu wanaotaka uvunjike.
“Sina uwezo wa kuwachagulia watu kitu
wanachokipenda na kukitamani. Imani yangu ni kwamba nje ya Muungano
hatutabaki salama kama ilivyo sasa. Muungano wetu umekuwa kinga na nguzo
kwa nchi zetu mbili na usalama na wake,” alisema Nahodha.
Aliitolea mfano Sudan Kusini ambayo ilitaka ipewe
mamlaka yake kamili akisema hivi sasa imejikuta ikiwa katika machafuko
na vita ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na kuibuka kwa mgawanyiko wa
kijamii unaotishia mustakabali wa Taifa hilo.
“Itazameni Sudan Kusini, tusipokuwa waangalifu na
makini yanaweza kutukuta. Angalia vita ya Somalia inaitesa Kenya na
kutukosesha amani, tusikubali kugawanywa na viongozi ambao wanawaza
madaraka.”
>>Mwananchi
>>Mwananchi