MWENYEKITI
wa IPP , Reginald Mengi, ametunukiwa Tuzo ya Mafanikio ya Maisha katika
Kusaidia Jamii kwa mwaka 2013 katika eneo la ukanda wa nchi za Afrika
Mashariki.
Tuzo
hiyo ijulikanayo kama East Africa Philanthropy Awards 2013, inatolewa
na Shirikisho la Taasisi Zinazofadhili Maendeleo ya Jamii katika Afrika
Mashariki (EAAG) lenye makao yake makuu nchini Kenya. Tuzo hiyo
alikabidhiwa na Balozi wa Norway Nchini, Ingunn Klepsvik katika hafla
iliyofanyika juzi usiku jijini Dar es Salaam.
Mtendaji
Mkuu wa EAAG, Nicar Sabula alisema shirika lao lilianzishwa mwaka 2003
na linaunganishwa na mashirika yanayofadhili maendeleo ya jamii katika
Ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Akizungumzia tuzo hiyo, alisema ilizinduliwa mwaka 2011 huko Arusha wakati wa mkutano mkuu wa shirika hilo.
Alisema
tuzo hiyo inalenga kuwatambua, kuwathamini kampuni, mashirika au watu
wa aina mbalimbali, ambao wamekuwa wanatoa misaada kwa jamii katika eneo
la Afrika Mashariki.
"Ni
tuzo kwa watu ambao wametoa muda, fedha, taarifa bidhaa na huduma na
sauti zao zikasaidia kuboresha maisha au kundi fulani la watu," alisema Sabula.
Aliongeza
kuwa ili mtu au shirika liweze kuwa na sifa za kupewa tuzo hiyo ni
lazima hatua yake ya msaada, iwe ya viwango vya juu ambayo inaweza
kuwavutia wengine.
Tuzo hiyo ilizinduliwa mwaka jana huko Entebe nchini Uganda, ikiwa ni miongoni mwa tuzo nane zinazotolewa na asasi hiyo.
Alisema
jumla ya watu 60 walipendekezwa kupewa tuzo hiyo kwa mwaka huu kutoka
nchi zote za Afrika Mashariki. Kati ya hao, watu 15 walipenya katika
mchujo wa awali, ambao ulifanywa na watu mashuhuri kutoka katika asasi
zisizo za kiserikali.
"Kati
ya hao, watu wanane walikidhi vigezo vya kupewa tuzo hizo na Mengi
akiwa ni mmojawapo ya watu ambao walishinda Tuzo ya Mafanikio ya Maisha
katika kusaidia jamii (Lifetime Achievement in Philanthropy Award).
Mwenyekiti
wa EAAG, Tom Were alisema Afrika Mashariki ili isiendelee kutegemea
misaada kutoka nje ya bara hili, inategemea kuzalisha akina Mengi wengi
ili waweze kujitokeza kusaidia jamii inayowazunguka.
Alimwelezea
Mengi kuwa ni mtu ambaye amejitoa katika maeneo mengi kusaidia jamii na
kupata mafanikio, ndio maana amechaguliwa kutunukiwa tuzo hiyo.