Home » » Kivuli cha Mandela kuitesa familia yake..!

Kivuli cha Mandela kuitesa familia yake..!

VITA ya ndani ya familia ya Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, iliyoanza kupiganwa mapema mwaka huu, muda mfupi baada ya kulazwa katika Hospitali ya Med Clinic, Pretoria, huenda ikachukua sura mpya kwa makundi mawili yanayohasimiana kuanzisha upya mapambano yake nyuma ya kivuli cha Mandela.
Vita hiyo ambayo chanzo chake ni mzozo wa urithi wa utajiri mkubwa alionao Mandela, inatarajiwa pia kuigusa Serikali ya Pretoria ambayo tangu mwanzo ilionekana kutia mkono kwa kile ambacho baadhi ya wachambuzi na wafuatiliaji wa mambo wa nchini humo wamepata kukieleza kuwa ni jitihada za wakuu wa Dola inayoongozwa na Chama cha African National Congress (ANC) za kutumia kivuli cha Mandela ili kuendelea kukubalika na jamii kubwa ya watu wa Afrika Kusini.

 
Tayari mvutano baridi umekwishaibuka kuhusu mahali ambapo mwili wa Mandela unapaswa kuhifadhiwa kabla ya mazishi yake ambapo Serikali ya Pretoria imetamka kuwa utawekwa Ikulu huku familia yake ikitaka uwekwe katika makazi yake ya Johannesburg.

Nyuma ya hilo, Mandla Mandela, mjukuu mkubwa wa ukoo wa Mandela anaangaliwa kwa jicho la pembe na wengi nchini humo kama atakubaliana na matakwa ya wanaukoo wenzake ya mahali atakapozikwa babu yake kutokana na hatua yake ya awali ya kutaka kumzika kwenye makaburi yaliyo kwenye himaya yake ya uchifu iliyoko Mzove.

Wanaomuangalia kwa jicho la pembe Mandla ni pamoja na wanafamilia 16 wanaoongozwa na mtoto mkubwa wa kike wa Mandela, Makaziwe Mandela, ambao hapo awali waliunganisha nguvu pamoja kupambana naye mahakamani wakipinga hatua yake ya kubadili eneo la makaburi ya familia.

Katika kesi hiyo, Makaziwe na wenzake, walifungua kesi ya jinai katika Kituo cha Polisi cha Bityi, kilichoko jimbo la Eastern Cape, wakimtuhumu kuvamia eneo la makaburi ya familia lililo kijiji cha Qunu na kuiba miili ya wanafamilia watatu aliyokwenda kuizika upya kijiji cha Mzove.

Miili ya watoto wa Mandela ambayo Mandla alituhumiwa kuifukua kutoka Qunu na kuizika upya Mzove ni pamoja na mwili wa baba yake mzazi, Makgatho Mandela, aliyefariki mwaka 2005, Makaziwe Mandela, mtoto wa kwanza wa kike wa Mandela aliyefariki mwaka 1948 na Thembekile Mandela.

Wakati kesi hiyo ya jinai ikifunguliwa, tayari Mahakama Kuu ya Mthatha ya Jimbo la Eastern Cape iliyokuwa ikisikiliza shauri jingine lililofunguliwa awali na Makaziwe aliyeiomba imuamuru Mandla kurejesha miili ya watoto watatu wa Mandela aliyodai aliiba kutoka makaburi ya familia yaliyoko Qunu na kwenda kuizika Mzove, ilikuwa imekwishatoa hukumu ya kumtaka Mandla kuirejesha miili hiyo katika makaburi ya awali.

Wafuatiliaji wa mwenendo wa familia ya Mandela wamepata kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari vya nchini humo wakieleza kuwa chanzo cha mzozo wa wanafamilia hao ni kuwania urithi wa utajiri alionao mzee huyo baada ya kufa kwake.

Mtazamo huo ulianza kuaminiwa na wengi baada ya Mahakama Kuu ya Mthatha, kumuweka Makaziwe katika mazingira mazuri ya kusimamia mazishi ya Mzee Mandela baada ya kufa kwake, jambo ambalo lilionekana kuwapa faraja wanafamilia wanaomuunga mkono ambao waliibua madai ya ufisadi uliokuwa ukifanywa na Mandla katika shughuli ya mazishi ya Mandela.

Walimshutumu kwa kuuza haki ya kutangaza shughuli za mazishi na maziko kwa moja ya kituo cha televisheni ambacho kilimlipa mamilioni ya Rand bila idhini ya familia na waliimulika hata baadhi ya miradi aliyoianzisha kijijini kwake Mzove kupitia kivuli cha babu yake Mandela akidaiwa kutawatangazia baadhi ya wawekezaji kuwa atazikwa katika himaya yake hiyo.

Mandla ambaye amekuwa akipambana na jeshi la Makaziwe linaloundwa pia na Zindzi, Mke wa Mandela, Grace Machel na wajukuu watano ambao ni Ndaba, Mbuso, Ndikile, Tukwini na Pumla haina shaka kuwa anaweza kuibuka tena na madai yake ya kutaka kuhodhi mazishi ya Mandela.

Inaelezwa kuwa iwapo Mandla ambaye vyombo vya habari mbalimbali vya Afrika Kusini vimepata kumuelezea kuwa ni kijana mtukutu na asiyekubali kishindwa kirahisi ataibuka upya, Makaziwe na jeshi lake la wanafamilia watakuwa na kazi kubwa ya kumdhibiti.

Raia wengi wa Afrika Kusini ambao wamekuwa wakifuatilia mzozo wa wanafamilia hao wanaamini kuwa Ikulu ya Pretoria ndiyo pekee inayoweza kumdhibiti Mandla wakati huu ambao Mzee Mandela aliyekuwa akimpenda sana mjukuu wake huyo akiwa amenyamaza milele.

Imani hiyo imejengeka kwa wengi kutokana na taarifa za awali zilizoeleza kuwa baada ya Mzee Mandela kukata kauli na kuwalazimu wanaye kurejea Afrika ya Kusini, Ikulu ya Pretoria ilitumia fursa hiyo kufanya nao mazungumzo na kuwaeleza namna ambavyo Mandla amekuwa akitumia uhuru aliopewa ndani ya familia kufanya mambo yasiyokubalika.

Kwamba jambo kubwa ambalo Makaziwe na wenziwe walitakiwa kulifanyia kazi haraka ni mahali atakakozikwa Mzee Mandela baada ya kufariki kwa sababu mahali alipoelekeza palibadilishwa na Mandla hivyo kulikuwa na hofu ya kuibuka mvutano ndani ya wanafamilia wenyewe jambo ambalo iwapo lingetokea lingeitia aibu familia na taifa zima la Afrika Kusini.

Hata hivyo, zipo taarifa zilizodai kuwa Serikali ya Pretoria ilikuwa ikipata wakati mgumu kutoka kwa Mandla ambaye alikuwa akiiweka kando katika mambo mengi yaliyokuwa yakimuhusu Mandela bila kujali kuwa kivuli chake kilikuwa muhimu kwa ustawi wa ANC.

Ukweli kwamba Mandla alikuwa mrithi wa uchifu wa Mandela ulizifanya Mamlaka za Afrika za Kusini kushindwa kumdhibiti na hilo liliwezeka zaidi kwa sababu alikuwa akisikilizwa sana na Mandela mwenyewe kiasi kwamba na hata watu walio karibu na Mandela walikuwa makini na Mandla ili kuepusha mgogoro ambao ungeweza kumuumiza Mzee huyo.

Vyovyote iwavyo, wakati ikiwa imekwishatangazwa na serikali ya Pretoria kuwa Mandela atazikwa kijijini kwake Qunu Desemba 15, macho na masikio ya wengi bado yanasikiliza na kuangalia kile kinachoweza kutoa ndani ya familia hiyo kabla na hata baada ya mazishi yake
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger