Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema hatishwi na mchakato wa kumng’oa katika nafasi yake ambao umeanzishwa na Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalla kutokana na tuhuma za kukiuka kanuni za Bunge.
Kadhalika Spika Makinda amepuuza hoja za Dk
Kigwangalla akisema kuwa yeye hajavunja kanuni yoyote, lakini akaweka
bayana kuwa mbunge huyo wa Nzega ana haki kwa mujibu wa Kanuni za Bunge
kuendelea na kile anachokifanya.
“Kanuni si zinamruhusu, utaratibu upo kwenye
kanuni za Bunge kwa hiyo aendelee na mchakato lakini mimi ninachosema
sitetereki maana hakuna kanuni yoyote ambayo nimeivunja,” alisema
Makinda katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake jana.
Wakati Spika akitoa kauli hiyo, jana, Dk
Kigwangalla alianza harakati zake za kukusanya saini za wabunge,
akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya kutokuwa na imani naye kwa madai
kwamba amekuwa akikiuka kanuni.
Miongoni mwa madai ya Dk Kigwangalla ni hatua ya
Makinda kufanya uteuzi wa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge
kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, tofauti na kanuni
zinazotaja wenyeviti kuchaguliwa na wajumbe wa kamati.
Hoja nyingine ni kamati hiyo ya bajeti kulipwa
posho ya Sh430,000 wakati wajumbe wa kamati nyingine wamekuwa wakipewa
Sh130,000 pamoja na kumteua Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba
kuingia katika kamati hiyo ya bajeti wakati mbunge huyo ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Miundombinu.
Jana Dk Kigwangalla aliwasilisha hoja yake kwa
Katibu wa Bunge na kuongeza madai mapya yakiwamo ya kuagiza kwa mabavu
majedwali ya mabadiliko ya sheria kwenda kwenye kamati ya bajeti,
kuvunja masharti ya kanuni ya 48 inayotoa maelekezo ya namna ya
kuwasilisha na kujadili jambo la dharura na kutumia madaraka yake vibaya
kwa kuvunja masharti ya Sheria ya The National Assembly
(Administration) Act (Cap.115) ya mwaka 2008.
(Administration) Act (Cap.115) ya mwaka 2008.
Makinda akijibu hoja hizo jana alisema alifanya
uteuzi wa Chenge kuongoza Kamati ya Bajeti kwa sababu kamati hiyo ni
mpya na haikuwapo katika kamati za awali, hivyo ni wazo ambalo
lilitokana na mawazo ya Bunge la sasa.
“Tulikuwa tunafikiria jinsi Bunge linavyoweza
kuisadia Serikali ipate vyanzo vipya vya mapato. Kwa hiyo tumehitimisha
wazo hili kwa kuamua kuwa na Kamati ya Bajeti. Kamati hii haikuwapo na
wala utaratibu wake wa kikanuni haukuwapo.
Niliamua na kanuni zinanipa uwezo huo kwamba niteue mtu ambaye ninaamini anaweza kuisimamia katika hatua za mwanzo ili tuone uzoefu utatufikisha wapi,” alisema Makinda na kuongeza:
Niliamua na kanuni zinanipa uwezo huo kwamba niteue mtu ambaye ninaamini anaweza kuisimamia katika hatua za mwanzo ili tuone uzoefu utatufikisha wapi,” alisema Makinda na kuongeza:
“Kamati hii hata Serikali ilikuwa haikubaliani na
sisi, lakini katika muda mfupi wa utendaji wake umefanya kazi kubwa na
kama tusingekuwa na Mzee Chenge ambaye ni mzoefu na anafahamu vizuri
utendaji wa Serikali basi tungeshindwa na mimi siko tayari kuanzisha
kitu halafu nikashindwa”.
Kuhusu posho, Spika aliungana na kauli ya Katibu
wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kwamba si wakati wote Kamati ya Bajeti
imekuwa ikipewa malipo zaidi, bali ni pale tu wanapofanya kazi nje ya
siku na saa za kazi tena kwa kibali chake.
“Lazima walete maombi na waeleze kwa nini
wanapaswa kufanya kazi kwa muda wa ziada au siku za mapumziko na mimi
nikisharidhia basi wanalipwa mara mbili ya viwango vya kawaida na hiyo
ni kwa mujibu wa taratibu na Kanuni zetu,” alisema
Kadhalika alizungumzia suala la wabunge wengine kuteuliwa
kuingia kwenye kamati ambazo si zao ambapo alisema, suala hilo pia ni la
kawaida kwani hata katika mjadala unaoendelea wa Kamati ya Katiba,
Sheria na Utawala ameongeza wajumbe wa ziada.
“Ninafanya hivyo kupanua wigo wa mjadala na mara
nyingi kwa mfano kwenye kamati yetu ya Katiba nimeongeza wabunge wenye
uelewa wa masuala ya sheria ili watusadie kufanya uchambuzi, maana
unaweza kukuta kwenye kamati, watu wenye utaalamu kuhusu suala husika ni
wachache. Kwa hiyo siyo kosa kwa mujibu wa Kanuni zetu,” alisema
Makinda.
Ukusanyaji saini
Kwa upande wake Dk. Kingwangalla jana alikuwa
akiendelea na ukusanyaji wa saini za wabunge huku akisema kuwa
amewasilisha kwa Katibu wa Bunge kusudio la kupeleka bungeni hoja yake.
Ukusanyaji wa saini ulifanywa kwa kupitia fomu
maalumu na kutoa taarifa kwamba wabunge wa CUF na NCCR-Mageuzi, wote
wameshasaini katika fomu hizo.
Akizungumza jana katika viwanja vya Bunge, Dk
Kigwangallah, alisema wabunge wa Chadema, walimweleza kuwa watafanya
hivyo baada ya kukutana katika kikao cha pamoja.
Hata hivyo Kiongozi wa Upinzani Bungeni ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikiri kusikia taarifa hizo
lakini akasema walikuwa bado hawajaketi kama kambi ili kuwa na msimamo
wa pamoja kuhusu suala hilo.
Jana asubuhi wakati wa kipindi cha maswali na
majibu, Dk. Kingwangalla alionekana akipita katika baadhi ya meza za
wabunge akiwashawishi kusaini fomu za kumuunga mkono.
Hadi jana mchana wabunge wa CCM, na CUF wapatao 30 tayari walikuwa wamesaini fomu hizo, wakimuunga mkono mbunge huyo.
Alipoulizwa ulazima wa kukusanya saini za wabunge
wakati kanuni hazimtaki kufanya hivyo alisema, hilo linamwezesha kujua
nguvu aliyonayo katika kumuunga mkono kuhusiana na suala hilo.
Hoja zake
Katika taarifa ya kusudio lake ambalo Mwananchi imebahatika
kuliona, Dk. Kingwangalla alisema uteuzi wa Serukamba ni kinyume na
masharti ya kanuni ya 116(3) na (4).
Alisema Juni 27, 2013, wakati wa kutunga sheria ya
fedha, Spika aliagiza kwa mabavu kuwa wabunge wote wenye majedwali ya
mabadiliko waende kwenye kamati ya bajeti.
“Uamuzi huu wa Spika ni wa kidikteta na unapingana
na masharti ya kanuni ya 88 ya kanuni za kudumu za Bunge ambapo kwa
ufupi ni kwamba majedwali ya mabadiliko hujadiliwa bungeni wakati wa
kamati ya Bunge zima na huamuliwa kukubaliwa ama kukataliwa na Bunge
zima na si kamati yoyote ya Bunge,” alisema.
Alisema hatua hiyo ya kuipa mamlaka makubwa kamati
hiyo ni kuondoa mantiki ya uwepo wa Bunge lilopewa mamlaka ya kutunga
sheria zote za nchi na Katiba ibara ya 63 (3) ( c) na (d ).
Pia alisema Spika Makinda amekuwa wa kwanza
kuvunja masharti ya kanuni anazopaswa kuzitilia nguvu kama
anavyoelekezwa na kanuni ya 5 (2). Amevunja pia kanuni na hivyo
anastahili kuhukumiwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa masharti ya kanuni
hizi ili kukidhi masharti ya Ibara ya 84 (7) (d) ya katiba ya kumwondoa
madarakani.
Alitoa mfano wa hoja ya dharura iliyotolewa wakati
MV Skagit ilipozama Julai 18, 2012 na siku zilipowasilishwa hoja mbili
zinazohusiana na mauaji ya kwenye vurugu zinazohusu migogoro baina ya
jamii za wakulima na wafugaji na wanyang’anyi wa mali na unyanyasaji wa
wafugaji unaofanywa kwenye operesheni tokomeza ujangili.
Katika kuhitimisha taarifa hiyo, Dk Kingwangalla
alisema: “Ni maoni yangu binafsi na ya wabunge wengi wanaoniunga mkono
kuwa Spika wa Bunge Anne Makinda apumzishwe kazi kwa tuhuma nilizozitaja
hapo juu.”
-Mwananchi
-Mwananchi