Home » » Wanakwaya wa kanisa katoliki wapigwa bomu jijini Arusha , sita wajeruhiwa, mmoja hali yake ni mbaya

Wanakwaya wa kanisa katoliki wapigwa bomu jijini Arusha , sita wajeruhiwa, mmoja hali yake ni mbaya



WANAKWAYA sita wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Kalory Rwanga, Usa River, mkoani hapa, wamelazwa katika Hospitali ya Misheni na ya Tengeru, Arumeru baada ya kujeruhiwa kwa bomu.
 
Walikutwa na masahibu hayo juzi muda mfupi baada ya kutoka kanisani kwenye Mkesha wa Mwaka Mpya saa 6.30 usiku, meta 100 kutoka Kanisa hilo, eneo la Kisangani.
 
Mganga Msaidizi wa hospitali hiyo, iliyoko chini ya Kanisa Katoliki, Fredrick Mathew, alithibitisha jana kupokewa majeruhi watano, huku wawili wakiwa na hali mbaya na wengine wakiendelea vizuri.
 
Alitaja majeruhi hao kuwa ni Theresia Lesitare (33), Philipo Ambrose (22), Alphonce Nyigo (19), Mary Merikiory (40) na Anna Mathew (19) wote wakazi wa Lake Tatu, Usa River.
 
Majeruhi mwingine ambaye hali yake si nzuri, Annet Baltazar (16) amelazwa katika Hospitali ya Tengeru. Alisema majeruhi hao waliumia miguuni kwa kuchanwa na mlipuko huo na baadhi ya vipande vya bomu, vilitolewa kwenye miili yao na baadhi yao kushonwa kwa nyuzi kadhaa.
 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kupata taarifa za tukio hilo na kueleza, kwamba uchunguzi wa tukio umeanza mara moja na atatoa taarifa ukikamilika.
 
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Merikiory, alisema baada ya kutoka kanisani akiwa na wanakwaya wenzake, waliondoka kuelekea nyumbani, Lake Tatu.
 
Alisema wakiwa barabarani, waliona gari aina ya Toyota Land Cruiser likienda kwa kasi na lilipowakaribia, walisikia mlipuko na wakajikuta wamelala kando ya barabara huku baadhi yao wakivuja damu miguuni na tumboni.
 
Aliongeza kuwa gari hilo, halikusimama na lilipofika mbele waliokuwamo walifyatua mabomu ya kutoa machozi, kutawanya makundi ya watu mbalimbali waliokuwa wakionekana barabarani.
 
Alisema waliomba msaada kwa Paroko wa Kanisa hilo, Patrick Njau, ambaye alitoa gari na kuwapeleka Hospitali ya Misheni na wengine wakipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Tengeru kwa matibabu zaidi.
 
Askofu alia
Akizungumza huku akitokwa machozi baada ya kutembelea majeruhi, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Josephat Lebulu alisema ameshangazwa na tukio hilo. Alisisitiza kuwa Kanisa Katoliki, limechoka kuandamwa na matukio ya aina hiyo.
 
“Waumini wanakosa gani hadi watupiwe bomu, kwa nini polisi wako kimya hadi leo wasiseme? Kuna siri gani? Kwa nini kila siku ni Wakatoliki tu ndio wanapigwa mabomu, tunataka haki itendeke, watu wametoka kanisani usiku, wamekosa nini? Usalama uko wapi?” Alihoji.
 
Aliendelea: “Tumekosa nini, kupigwa mabomu kila siku hapa Arusha? Tumeshuhudia Olasiti, tukashuhudia Soweto sasa ni hapa Usa,” alisema. “Na kwa hili Kanisa hatutakubali hata kidogo, tunataka wahusika wawajibishwe na walioficha uovu huu wawajibishwe la sivyo viongozi walioficha uovu huu wawajibishwe, Mungu atasimama kwa ajili yetu,” alisema.
 
Mei mwaka jana, bomu lililorushwa liliua watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 60 kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Parokia ya Olasiti, mjini Arusha.
 
Waumini walikuwa wamejumuika katika misa ya uzinduzi wa Kanisa hilo. Misa hiyo ilikuwa ikiongozwa na Balozi wa Vatican nchini na Mwakilishi wa Papa Francis, Askofu Francisco Padila kwa kushirikiana na Askofu Lebulu.

>>Habari leo
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger