Haruni Kayombo.
Katika mahojiano na gazeti hili akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, Kayombo alisema bado hajui hatima ya maisha yake kutokana na mateso anayoyapata usiku na mchana huku akitoa simulizi ya majonzi namna gonjwa hilo lilivyomtokea.
Alisema awali akiwa na umri wa miaka 11 alilazwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya lakini baadaye wazazi wake walifariki dunia na hakupata kuwajua ndugu zake jambo ambalo anaona hakuna haja ya kuwa binadamu huku akionekana mwenye mateso makubwa.
“Sioni faida ya kuwa binadamu, niliugua kama utani, ilifika wakati nikajua kitu cha kawaida, nilishangaa kuona linazidi kuongezeka nilijua utakuwa ugonjwa wa muda mfupi, lakini nikashangaa usiku na mchana mateso yanazidi.
“Ni tatizo ambalo hata mimi mwenyewe sijui chanzo chake, lilianza kama kauvimbe ka kawaida, sikutambua mapema na sikuwa na hela kwenda kwenye kituo cha afya kwa matibabu zaidi.
“Nilijipa moyo kuwa ipo siku nitakuwa sawa lakini kwa mpaka sasa nimeshakata tamaa, sina baba wala mama, hapa kweli kuna haja ya mimi kuitwa binadamu? Sina kazi na sikubahatika kusoma ni nani atakayeokoa maisha yangu?
“Maisha haya ni Mungu tu anayeweza kuniokoa, inaniuma sana! Ningekuwa na ndugu wangeweza kunisaidia japo hata pesa ya matumizi. Eee... Mola okoa maisha yangu (analia). Napenda kuishi kama binadamu wengine lakini kwa hali hii sina amani kabisa.
“Zamani wakati tatizo linaanza nilikuwa na tabia ya kusali mara kwa mara lakini nimefika hatua ya kukata tamaa na kuona hakuna haja.
“Namuomba rais aje anitembelee ajionee mateso ninayoyapata usiku na mchana, nimepangiwa kwenda kufanyiwa operesheni India lakini sijui lini na itakuwaje!” alisimua Kayombo na kumaliza na kilio tena.
Kama utakuwa umeguswa na tatizo la Haruni Kayombo basi usisite kutoa mchango wako kwenye namba yake ya simu, mtumie kwa njia ya M-PESA ama wasiliana naye moja kwa moja akiwa ndani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa namba +255764548607.