JESHI
la Polisi mkoani Simiyu linamshikilia mwanamke na mkazi wa Kijiji cha
Usiulize wilayani Meatu kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake kwa kumvuta
korodani, kutokana na wivu wa kimapenzi.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo alisema tukio hilo lilitokea
juzi saa tisa usiku katika Kitongoji cha Mlimani Kijiji cha Usiulize
Kata ya Mwamalole.
Alisema
katika tukio hilo, wapenzi wawili Jumanne Gunda (39), mkazi wa Kijiji
cha Kinyambuli wilayani Mkalamo, akiwa amelala na mchumba wake, Mariamu
Khamis (49) mkazi wa Kijiji cha Ibaga Wilaya ya Mkalamo mkoani Singida,
kulitokea kutoelewana kati yao na kusababisha wagombane.
Katika
ugomvi huo, ambao chanzo chake ni wivu wa kimapenzi, Mariamu
anatuhumiwa kuzivuta korodani za mpenzi wake na kusababisha mishipa
muhimu kukatika na kusababisha kifo cha Jumanne papo hapo.
Kufuatia
kifo hicho, Mariamu aliburuza mwili wa mpenzi wake mpaka chooni kwa
lengo la kuutumbukiza katika shimo la choo. Hata hivyo kutokana na udogo
wa tundu la choo, alishindwa kutumbukiza mwili huo chooni na hivyo
kuamua kuutelekeza humo.
Asubuhi
kulipopambazuka, majirani wa nyumba waligundua mwili wa marehemu ukiwa
umetelekezwa chooni na kutoa taarifa Kituo cha Polisi, ambao walifika
katika eneo la tukio na kumtafuta mtuhumiwa, Mariamu.
Baada
ya Mariamu kukamatwa, anatuhumiwa kukiri kumuua mpenzi wake katika
ugomvi kati yao, uliotokea usiku walipokuwa wamelala wote wawili.
Anatuhumiwa kukiri kumvuta korodani zake na kusababisha kifo chake.