Home » » Gazeti la Mtanzania litakuwa mtaani tena kuanzia ijumaa ya wiki hii baada ya serikali kulifunga kwa siku 90

Gazeti la Mtanzania litakuwa mtaani tena kuanzia ijumaa ya wiki hii baada ya serikali kulifunga kwa siku 90



GAZETI la Mtanzania ambalo serikali ililifungia kuchapishwa kwa muda wa siku 90 kwa kile ilichokieleza kuwa ni kuandika habari za uchochezi sasa litaanza tena kuchapishwa na kusambazwa nchini Ijumaa ya Disemba 27, 2013. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, kwa gazeti hili, uamuzi huo mpya umefikiwa katika mkutano wa dharura wa menejimenti ulioitishwa kujadili maoni na mapendekezo ya wasomaji yaliyotaka kuwapo kwa mabadiliko ya siku ya kurudi mtaani kwa gazeti hilo.
 

Kibanda alisema, awali menejimenti ya New Habari, ambayo pia inachapisha magazeti ya Rai, The African, Bingwa na Dimba ilipanga Gazeti la Mtanzania lirudi sokoni Desemba 25 baada ya kumaliza kifungo chake na maandalizi yote yalikuwa yamekamilika ikiwa ni pamoja na kutoa matangazo katika vyombo mbalimbali vya habari.

Alisema, tangu matangazo hayo yalipoanza kusikika katika vyombo vya habari, wadau wa habari na wasomaji wamekuwa wakituma maombi kwa wingi wakitaka kuwepo kwa mabadiliko ya siku hiyo kwa sababu inaangukia kwenye mapumziko ya sikukuu ya Krismas hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kukosa nakala za gazeti hilo.

“Nimeshangazwa na mwitikio wa wasomaji na wadau wa habari baada ya kutolewa kwa tangazo la kurudi mtaani kwa Gazeti la Mtanzania. Chumba cha bahari za Mtanzania na ofisini kwangu mimi mwenyewe simu zimekuwa zikimiminika zikiwa na ujumbe wa kushauri tubadilishe siku ya kurudi upya sokoni.

“Wengi wanasema siku ya Krismas siyo nzuri kwao kwa sababu watakuwa wamepumzika nyumbani na familia zao hivyo wanaweza kukosa nakala za gazeti letu. Wanatamani kusoma tena habari motomoto na makala zenye kufikirisha kama walivyoeleza wao. Wanachosisitiza ni kwamba gazeti lizinduliwe upya siku ya kawaida ya kazi.

Kwa sababu ya wingi wa maombi, menejimenti tulilazimika kukutana kwa dharura na tukaafiki maombi ya wasomaji wetu. Ingawa kuna hasara kubwa kwa sababu maandalizi yote ya kurudi mtaani kesho yalikuwa yamekamilika hatuna jinsi, tutaibeba, sasa tutakuwa sokoni Ijumaa ya Disemba 27,” alisema Kibanda.

Akizungumzia sura na muundo mpya wa gazeti hilo, Kibanda alisema dhamira ya timu ya wahariri na waandishi wa habari anaowaongoza ni kurudi sokoni upya kwa kuwapatia wasomaji wao habari bora zaidi walizozikosa kwa muda wa miezi mitatu.

Alisisitiza kuwa kauli mbiu ya Gazeti la Mtanzania ni Fikra yakinifu, na kwanza itawaongoza wafanyakazi wote wa kampuni hiyo kuwapatia wasomaji habari na makala bora zaidi.

Alisema Gazeti la Mtanzania sasa litabeba maoni ya wasomi, wanaharakati na wadau wa habari yatakayothibitisha fikra yakinifu ni zaidi ya kuwa na mawazo duni.

Gazeti la MTANZANIA lilifungiwa kwa madai ya kuchapisha habari na makala za uchochezi, katika toleo la Machi 20, Juni 12 na Septemba 18, mwaka huu.

Habari na Makala zilizolalamikiwa na serikali ni zilizobebwa na vichwa vya habari vilivyosomeka ‘Urais wa damu,’ ‘Serikali yanuka damu’ na ‘Mapinduzi hayaepukiki.’

Mbali ya MTANZANIA, Serikali pia ililifungia gazeti la Mwananchi kwa siku 14.

Kwa mujibu wa tangazo la serikali la kufungia magazeti hayo, ni mwenendo wake wa kuandika habari na makala za uchochezi na uhasama kwa nia ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vya dola, jambo ambalo linaweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger