Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe amejiweka katika mazingira magumu zaidi kisiasa ndani ya chama hicho, kutokana na shaka kubwa iliyougubika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam juzi.
Zitto pamoja na viongozi wengine wawili wa
Chadema; Dk Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba walivuliwa nyadhifa zao na
Kamati Kuu ya Chadema baada ya kubainika kupanga mbinu za uasi, kupitia
waraka ambao ulikuwa ukieleza mkakati wa kufanya mabadiliko makubwa ya
kiuongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani.
Leo, uongozi wa Chadema umeitisha mkutano wa
waandishi wa habari ambao pamoja na mambo mengine, utajibu baadhi ya
hoja za utetezi ambazo zilitolewa na Zitto pamoja na Dk Kitila. Katika
mkutano wa juzi, Zitto na Dk Kitila ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu
ya Chadema, walizungumzia kuvuliwa kwao madaraka, lakini maandalizi na
uendeshaji wa mkutano huo yanazua shaka kutokana kuwahusisha watu
wanaodaiwa kuwa ni wanachama wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi
(UVCCM).
Miongoni mwao, wamo waliowahi kuwa wanachama wa
Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Habib Mchange na Mtela Mwampamba
ambao walitimuliwa kwa makosa yanayofanana na yale yalizosababisha Zitto
na wenzake kuvuliwa nyadhifa zao.
Mchange na Mwampamba pamoja na aliyekuwa Makamu
Mwenyekiti wa Bavicha, Juliana Shonza, walivuliwa uanachama wa Baraza
hilo Januari 5, mwaka huu baada ya kupatikana na hatia ya kutumia
mitandao ya kijamii kukihujumu Chadema na kuwatukana viongozi wake
wakuu. Baadaye walihamia CCM wanakoendeleza harakati zao za kisiasa.
Jana, Machange alipotafutwa, alisema: “Mimi
sikuwahi kuondoka Chadema, nilifukuzwa kihuni kama walivyowafanyia Zitto
na Kitila. Nimepeleka malalamiko yangu tangu Januari hadi leo
sijajibiwa, hivyo siwezi kusema nimeondoka.
Nataka nimuunge mkono mwathirika mwenzangu kama ilivyokuwa mimi lakini nitabakia kuwa mwanachama mwaminifu.
“Mimi ni mwanaChadema na sikuwahi kujiunga na CCM
au chama chochote, walioondoka ni Mwampamba na Shonza.” Mwampamba
alisema: “Nilijitokeza pale kuonyesha mshikamano kwa sababu mimi pia ni
mwathirika. Kwa hiyo nilitaka ulimwengu ufahamu kuwa mimi ni kati ya
wanaopinga siasa za aina hii... Chadema ni chama kinachojiandaa kuchukua
dola, sasa kama kila mwenye mawazo tofauti anaonekana mhaini itakuwaje
siku wakichukua dola? Ubaguzi huu haujalishi uko chama gani, hata kama
niko CCM, hilo halinizuii kuungana na mtu aliyepatwa na tatizo kama
langu.”
Kuwepo kwao katika mkutano wa Zitto kunaweza
kutumiwa na uongozi wa Chadema kuwa uthibitisho wa kiongozi huyo
kushiriki katika uasi na kunaweza kupuunguzia nguvu utetezi unaotolewa
na Dk Kitila kwamba hakuwa sehemu mpango wa kuuondoa uongozi wa sasa
madarakani. Zitto, Dk Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa
Arusha, Samson Mwigamba wanasubiri kukabidhiwa barua za kuvuliwa kwao
madaraka na katika siku 14 wanapaswa wawe wamewasilisha utetezi wao
wakieleza kwa nini wasifukuzwe uanachama kutokana na tuhuma
zinazowakabili.
Dk Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa alisema
jana kuwa ilikuwa lazima viongozi hao wavuliwe madaraka hasa baada ya Dk
Kitila kukiri kuhusika na waraka ambao anasema ulilenga kushinda
kupitia uchaguzi halali ndani ya chama hicho.
“Hata katika ya nchi ukihusika kutengeneza mbinu
za siri lazima ushughulikiwe.Hakuna Katiba itakayokuruhusu kufanya
mipango ya siri. Kwanza uchaguzi wa Chadema nani katangaza mpaka mipango
ianzwe kutengenezwa sasa hivi?” alihoji Dk Slaa.
-----Mwananchi
-----Mwananchi