SIKU moja baada ya binti anayedaiwa kubakwa na kutishiwa kuuawa na Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), kufungua jalada polisi dhidi yake, inadaiwa mbunge huyo ametoweka nchini...
Vyanzo
mbalimbali vilivyo karibu na mbunge huyo, vinadai kuwa amesafiri juzi
kwenda nchini Sweden kwa masuala ya kikazi, na kwamba atakuwepo huko kwa
muda usiopungua mwezi mmoja.
Chanzo
kingine kimedokeza kuwa mbunge huyo alidai ametumwa kazi na kigogo
mmoja serikalini na atakuwepo nchini Sweden miezi miwili hadi mitatu.
Hata
hivyo haijajulikana kazi anayokwenda kuifanya Kapuya ingawa kuna
taarifa safari hiyo imelenga kumtuliza na upepo mbaya wa kuandamwa na
tuhuma za ubakaji ambazo zipo polisi hivi sasa.
Wakati
Profesa Kapuya anakimbilia nje ya nchi, tayari alishafunguliwa jalada
namba OB/RB/21124/13 katika Kituo cha Polisi Oysterbay, jijini Dar es
Salaam juzi.
Mtoa
taarifa wetu anasema muda mchache baada ya Kapuya kushindwa kumshawishi
binti huyo asimfungulie kesi ya ubakaji, wala kuogopa vitisho vya
kuuawa, au kupokea pesa kiasi chochote aondoke nchini, Kapuya mwenyewe
alipanga safari ya dharura na kwenda nje ya nchi.
Tanzania
Daima lilifanya juhudi za kuwasiliana na ofisi ya Bunge kujua kama
wana taarifa zozote za kuondoka kwa mbunge huyo kwenda nje ya nchi na
kujua ni sababu zipi hasa zimempeleka huko, lakini simu ya Naibu Spika
wa Bunge, Job Ndugai ilikuwa inaita bila kupokelewa.
Katibu
wa Bunge, Thomas Kashilila naye hakupatikana baada ya simu yake kuita
bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu (sms)
hakuujibu.
Hata
hivyo, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa Kamati ya Bunge ya
Kudumu ya Miundombinu ambayo Kapuya ni mjumbe wake haina safari ya
Sweden.
Tangu
Tanzania Daima lianze kuandika tuhuma hizi nzito, kumekuwapo na
kusuasua kwa mtuhumiwa huyo kutiwa hatiani na Jeshi la Polisi.
Harakati
za kufungua jalada dhidi ya Kapuya zilianza juzi jioni na kuendelea
hadi jana ambapo polisi walitumia zaidi ya saa 12 kumhoji binti huyo
anayedaiwa kubakwa ili kupata ukweli wa sakata hilo.
Akiwa
polisi, binti huyo alikutana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi ya
Oysterbay (OCD) na OC-CID wake na kutoa maelezo ya awali kabla ya
viongozi hao kumruhusu ayaweke malalamiko yake katika maandishi kwa
ajili ya kufunguliwa mashitaka.
Polisi wanena
Akizungumza
na Tanzania Daima Jumapili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni,
Camilius Wambura, alisema watamtafuta Kapuya nchi yoyote atakayokwenda
iwapo tuhuma dhidi yake zitathibitika.
Alisema
Jeshi la Polisi lina mtandao mkubwa ndani na nje ya nchi, hivyo si
rahisi kwa mtuhumiwa yeyote kuukwepa mkono wa sheria endapo itahitajika
kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Sisi
tunashirikiana na polisi wa nchi mbalimbali duniani, ndiyo maana
inakuwa rahisi kwa mtuhumiwa aliyetoroka nchi fulani kukamatwa nyingine
na kurejeshwa kwao.
“Nataka
niwaondoe hofu wale wote wanaodhani polisi haiwezi kumkamata mtu
akikimbia nchini, tuna mkono mrefu sana na hatufanyi kazi kinyume na
taratibu zetu,” alisema.
Kamanda
Wambura pia alikiri polisi kufungua jalada la Kapuya huku akiweka wazi
kuwa kinachofanyika hivi sasa ni uchunguzi wa tuhuma zake.
Alisema
miongoni mwa maeneo wanayoyafanyia uchunguzi ni kubaini kama ujumbe
ulio katika simu ya binti anayedai kubakwa na kutishiwa maisha unatoka
katika simu ya mbunge huyo.
“Tumefungua
jalada, lipo kwa ajili ya uchunguzi na tukibaini kuwa ni nani anahusika
na tuhuma hizo tutamsaka na kumkamata popote alipo,” alisema Wambura.
Source: Tanzania Daima