WATEJA katika mikoa inayopata umeme kwenye gridi ya Taifa wanatarajiwa kupata adha ya upungufu wa umeme kwa siku 11 kuanzia leo, kutokana na upungufu wa gesi kutoka katika Kisiwa cha Songosongo kilichopo wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi.
Hali
hiyo imetajwa inatokana na kuwapo kwa matengenezo ya kiufundi kwenye
visima vya gesi unaofanywa na Kampuni ya Pan African Energy Tanzania
Limited (PAT).
Meneja
Uhusiano wa TANESCO, Badra Masoud aliyasema hayo Dar es Salaam jana,
akisema upungufu huo utatokea kati ya Novemba 16 hadi Novemba 26, mwaka
huu na itahusisha maeneo yaliyopo katika mikoa iliyounganishwa katika
gridi ya Taifa.
“Tumepata
barua kutoka kwa kampuni ya Pan African inayotuuzia gesi, wakisema
inafanya matengenezo hayo kuboresha upatikanaji wa gesi ya kutosha
kwenye visima hivyo. Uongozi unaomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza
kwa baadhi ya maeneo yatakayokuwa yakikosa umeme,” alisema.
Kwa
mujibu wa Masoud, kutokana na matengenezo hayo mikoa iliyounganishwa
katika gridi ya Taifa itaathirika kwa kukosa umeme kwa baadhi ya maeneo
na kwa nyakati tofauti na kuongeza huduma ya umeme ni muhimu kwa kila
Mtanzania kwa ajili ya kujiinua kiuchumi na kipato, lakini matengenezo
hayo ni muhimu kwani itaboresha upatikanaji wa gesi kwa ufanisi zaidi.
Aliitaja mikoa na maeneo yatakayokumbwa na upungufu wa umeme kuwa ni Dar
es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Dodoma, Morogoro,
Singida, Mwanza, Mara, Mbeya, Iringa, Tabora, Shinyanga, Manyara na
Zanzibar.
Masoud
alisema gesi imekuwa ikiwawezesha kutoa Megawati 100 katika kituo cha
Ubungo 1, Megawati 100 katika kituo cha Ubungo 2, kituo cha Tegeta
Megawati 45 wakati Kampuni ya Songas imekuwa ikitoa Megawati 182 na
kuongeza kutokana na matengenezo hayo kutakuwa na upungufu wa Megawati
kati ya 150 na 200 na kwamba uzalishaji wa umeme kutumia mafuta na maji
utaendelea.
Alisisitiza
kuwa upungufu huo wa umeme sio mgawo ila ni kupitisha matengenezo ya
kiufundi ya Kampuni ya Pan African ambayo alidai kuwa ilishaiomba
Tanesco miezi miwili iliyopita ikitaka kufanya matengenezo hayo ambayo
hayaepukiki na yenye lengo la kuleta ufanisi zaidi.
Masoud
alitoa wito kwa wananchi kuwa wavumilivu siku hizo 11 wakati
matengenezo yakifanyika na kuwa lengo ni kuboresha upatikanaji wa gesi
ya kutosha kwa ajili ya kuzalisha umeme wa kutosha na kutoa huduma
inayoridhisha ya nishati ya umeme kwa wateja wake.
-Habari Leo
-Habari Leo