Home » » Waziri Magufuli asalimu amri....Mabasi yaruhusiwa kutopita mizani wakati mazungumzo ya AMANI yakiendelea...

Waziri Magufuli asalimu amri....Mabasi yaruhusiwa kutopita mizani wakati mazungumzo ya AMANI yakiendelea...



MGOMO mkubwa wa mabasi ya abiria umeitikisa nchi na kuilazimisha serikali kusitisha kwa muda amri yake ya kuwatoza asilimia tano wasafirishaji wanaozidisha uzito.

Idadi kubwa ya mabasi ya abiria yanayofanya safari ndani na nje ya nchi yaligoma jana katika miji mingi ya nchi na kusababisha taharuki kubwa kwa abiria waliokuwa wamekata tiketi kwa ajili ya safari.
  
Idadi kubwa ya abiria walipata wakati mgumu katika kituo kikuu cha mabasi jijini Dar es Salaam, Arusha na Moshi huku wasijue la kufanya.

Wafanyakazi wa mabasi mengi walikuwa wamesimama wakidai kuwa wamekatazwa na waajiri wao kuendelea na safari hadi watakapopewa maelekezo mengine.

Sakata hilo liliwalazimu viongozi wa Jeshi la Polisi kuwasili katika vituo hivyo na kuanza kuwasiliana na Wizara ya Ujenzi ambayo ilichukua muda mrefu kupata ufumbuzi.
  
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, alidai kuwa mgomo huo haukuwa halali kwa sababu wamiliki hao wa mabasi walikwisha kuingia mkataba na abiria kwa kuwauzia tiketi za kusafiria kwa siku ya jana, hivyo hawakupaswa kuwanyima haki yao ya kusafiri.
Mpinga alisema kitendo cha kutowasafirisha abiria hao ni sawa na kuvunja sheria.

Hata hivyo, baada ya Kamanda huyo kukutana na viongozi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), aliwataka wamiliki hao, hususan madereva kuwapeleka abiria hao kama tiketi zao zilivyokuwa zinaelekeza, huku akiagiza Sumatra kuwakamata wale wote watakaopinga kufanya hivyo na kuwanyang’anya leseni zao na hatua nyingine zichukuliwe dhidi yao.
  
Hata hivyo, amri hiyo iliongeza hasira, na kuzuka mvutano mkubwa uliozidisha taharuki miongoni mwa abiria.
Hali hiyo iliwafanya viongozi hao kuwasiliana tena na mamlaka za juu, na ndipo ilipokubaliwa kuyaruhusu mabasi yote kuondoka kwa masharti ya kutopimwa katika mizani.
  
Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa Taboa, Severine Ngallo, alisema makubaliano yaliyofikiwa ya kusafirisha abiria yalikuwa ya muda, wakisubiri matokeo ya kikao ambacho kingefanyika jana kwa kuwakutanisha na viongozi wa serikali.

“Nawashauri abiria wasikate tiketi katika kipindi hiki kwani kuna uwezekano mgomo huo ukaendelea tena leo na siku nyingine endapo madai yetu ya kuondolewa tozo hiyo yatakataliwa,” alisema Ngallo.
  
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo, alisema wizara imekubali kukutana na wasafirishaji hao, lakini akakana kuwapo kwa makubaliano ya mabasi kupita katika mizani bila ya kupimwa.

Jijini Arusha, mabasi yote yaligoma kuondoka kituo kikubwa cha mabasi kwa zaidi ya saa tatu, katika mwendelezo wa mgomo huo.
  
Hali hiyo ilimlazimu  Kamanda wa  Polisi mkoani humo, Liberatus Sabasi, kuingilia kati na kuwataka madereva hao kutumia busara ya kuendelea kuwasafirisha abiria wao ambao walikuwa tayari wameshawakatia tiketi.

Alisema kuwa kila abiria anapopanga safari yake ana kusudi lake, hivyo kuvunja safari kwa sababu za mgomo si busara.
  
Madereva hao walikubali kuendelea na safari kama kawaida majira ya saa mbili asubuhi huku wakidai kuwa hawajui mahali pa kuwapeleka abiria hao kwani mgomo wao ni wa nchi nzima.
  
Mjini Moshi, mabasi yote yalisitisha safari zake kwa zaidi ya saa tano na kuasabisha hali ya taharuki kwa wasafiri katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi.
  
Hali ilikuwa mbaya zaidi katika kituo hicho kutokana na  idadi kubwa ya wasafiri waliokuwa wakisafiri kuelekea jijini Dar es Salaam na mikoa ya Mashariki kukwama huku wengi wao wakilazimika kusitisha safari na kurejea majumbani licha ya kuwa na tiketi kwa ajili ya safari.
  
Baadhi ya wasafiri walilaumu kauli ya Waziri John Magufuli, kuwaambia wasafirishaji kuegesha magari yao majumbani na si katika barabara.
  
Walisema kauli hiyo ilichochea hasira na si ya kistaarabu, kwa kuwa imeongeza msuguano kati ya wasafirishaji na serikali.
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger