Home » » VIOJA: HAUSIGELI ATELEKEZEWA NYUMBA HUKO TANGA..

VIOJA: HAUSIGELI ATELEKEZEWA NYUMBA HUKO TANGA..

 Msaidizi wa kazi wa ndani ‘hausigeli’ aliyejitambulisha kwa jina la Nana Jackson (22), mwenyeji wa Tanga, amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kutelekezewa nyumba na bosi wake mwanamke aitwaye Nikita au mama Hassan.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 6, mwaka huu maeneo ya Minazini-Makumbusho jijini Dar.
Akizungumza na Risasi Jumamosi juzikati, hausigeli huyo alisema alifika Dar kufanya kazi za ndani kwa mwanamke huyo kwa kuunganishiwa na jirani yake wa huko Tanga.
Alisema alikaa kwa mama Hassan kwa siku tano tu ndipo siku ya sita ambayo ilikuwa Jumapili usiku wa saa nne, bosi wake alimuaga anakwenda Kibaha kwa baba yake kumpelekea mjukuu wake (Hassan) ndipo ‘akazamia kimoja’.
“Siku hiyo nilishangaa kumwona dada akitoka na mabegi na kuniambia anakwenda Kibaha mara moja na mtoto akamsalimie babu yake. Machale yalinicheza kuwa atakaa huko muda mrefu kutokana na wingi wa mizigo, nikamuomba anipe mshahara wangu kabisa.
“Hakusita, alinipa shilingi elfu hamsini (50,000) kama malipo yangu ya mwezi mzima japo nilikuwa sijamaliza mwezi toka nianze kazi kwake,”alisema Nana.
Baada ya mwanadada huyo kuondoka, Nana anasema  siku iliyofuata (Jumatatu) saa mbili asubuhi, watu asiowajua walifika nyumbani hapo wakiwa kwenye magari mawili aina ya Noah yenye ‘tinted’ kisha mmoja akaingia ndani na kuanza kupekuwa kila kona ya nyumba hiyo.
Baada ya kutokea hali hiyo wale watu wakaondoka, ghafla bosi wake naye  akampigia simu na kumtaka afungashe kila kitu kilichopo kwenye nyumba hiyo na kurudi kwao Tanga, nyumba aikabidhi kwa mmiliki wake.
Aidha, mwenye nyumba alimgomea kupokea funguo kwa madai kuwa anaogopa endapo kitu kikipotea na yeye akahusishwa, ikabidi aitwe mjumbe wa serikali ya mtaa huo, Zunda Douglas na kumfikishia taarifa za tukio zima,
ndipo alipoongozana kwa kuelekea kwa mmiliki wa nyumba hiyo kumshauri apokee funguo.
Hatimaye dada huyo alifungasha virago vyake mbele ya mapaparazi wetu huku akishuhudiwa na mjumbe, mwenye nyumba na majirani waliokuwa wakimzungumzia bosi wa hausigeli huyo kwa namna tofauti wanavyomfahamu.
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger