BINTI wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kilimani iliyopo Kipunguni, Dar mwenye umri wa miaka 12 (jina tunalihifadhi kwa sababu za kimaadili) amejikuta akishindwa kuendelea na masomo baada ya kupewa ujauzito na kijana wa mtaani aliyejulikana kwa jina moja la Roja.
Binti wa darasa la sita mwenye miaka 12 aliyepewa ujauzito na Roja.
Akizungumza kwa huzuni mama wa mtoto huyo, Aziza Mohammed alisema kuwa mwishoni mwa mwezi uliopita ndiyo aligundua kuwa binti yake huyo ni mjamzito na ilikuwa ni baada ya kukataa kwenda shule huku akitapika mara kwa mara.Mama huyo alisema, baada ya kuona dalili hizo aliamua kwenda kununua kifaa cha kupimia mimba lakini mwanaye huyo alikimbilia kwa mama yake mdogo, Temeke ambako waligundua kuwa ni mjamzito.
“Alipofika kwa mama yake mdogo ilibainika kuwa ana mimba, wakanipa taarifa, nikawaomba wamlete kisha tukampeleka hospitali ambako tulithibitishiwa na daktari kuwa kweli ana ujauzito wa miezi mitano,” alisema mama huyo na kuongeza:
“Nilimbana aniambie mwenye mzigo huo ambapo alimtaja kijana aitwaye Roja. Akaniambia kijana huyo ambaye ni jirani yetu amekuwa akimbaka na kumtishia kumuua ikiwa atasema.
“Kwa maelezo hayo ilibidi tumtaarifu mjumbe wa mtaa wa Kipunguni B, Bakari Issa ambaye tulikwenda naye kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Stakishari na kufungua jalada la kesi lenye namba STK/RB/18639/2013 KUMPA
MWANAFUNZI MIMBA
“Jamani naomba taasisi husika zinisaidie kwa sababu baada ya kutoa ripoti polisi nimekuwa nikuzungushwa tu...mtuhumiwa hakamatwi.”
SIMULIZI YA KUSIKITISHA
Binti aliyepata dhahama hiyo alipata kuzungumza ambapo alisimulia simulizi ya kusikitisha sana ikionesha jinsi mchezo mzima ulivyokuwa.
Alisema: “Wadogo zake Roja ndiyo walikuwa marafiki zangu...Roja alikuwa akiwatumia wao kuniita kila siku jioni na nilipoenda alikuwa akinifungia chumbani kwake na kunilazimisha kufanya naye mapenzi huku akinitishia kuwa nikisema ataniua.
“Pamoja na vitisho hivyo alikuwa akinipa shilingi elfu tatu hivyo nikawa naogopa kumwambia mama na nilipogundua nina mimba nilimtuma wifi yangu (dada wa Roja) akamwambie lakini akakataa na kusema mimba siyo ya ndugu yake, mimi sijawahi kufanya mapenzi na mwanaume mwingine zaidi yake,” alisema binti huyo.
KUTOKA KWA MWANDISHI
Tukio hili linaumiza na kusikitisha. Ni wito wetu kwa taasisi husika kufuatilia sakata hili na kumsaidia binti huyu ambaye ndoto zake zimezimwa ghafla akiwa bado mdogo.
Aidha, ni vyema wazazi wakawa makini katika kufuatilia nyendo za watoto wao kabla mambo mabaya hayajawakuta.
-Gazeti la ijumaa via Gpl