Home » , » MMHHH...!!! DAKTARI MWENYE MATATIZO YA AKILI ATIBU WATU NA KUFUNDISHA MASUALA YA TIBA...

MMHHH...!!! DAKTARI MWENYE MATATIZO YA AKILI ATIBU WATU NA KUFUNDISHA MASUALA YA TIBA...

MMHHH...!!! DAKTARI MWENYE MATATIZO YA AKILI ATIBU WATU NA KUFUNDISHA MASUALA YA TIBA...

Huwezi kuamini lakini huu ndio ukweli, kwamba watu kadhaa wamekuwa wakimiminika kupata msaada wa tiba, ushauri wa kitabibu na wengine masomo ya udaktari kwa mtu ambaye imethibitika kwamba hivi sasa ana matatizo ya akili.
Huyu si mwingine bali ni Mark Paulo Kishiwa ambaye kitaaluma ni daktari, aliyewahi kufanya kazi Hospitali za Kasulu, mkoani Kigoma na Bugando mkoani Mwanza, lakini sasa mvua na jua humwishia akiwa maeneo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Ukimwona mara kadhaa utamkuta akiimba nyimbo zisizo rahisi kuzielewa kutokana na hali anayonekana kuwa nayo ya matatizo ya akili, lakini anapokuwa sawa, hugeuka kuwa msaada kwa wengi; madaktari wa MNH ambao huomba ushauri kwake, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba Muhimbili (MUHAS) na wagonjwa ambao hutaka ushauri pia.
Dk Kishiwa anasema: “Naikumbuka Aprili 26, 1981, ilikuwa Jumatatu ya Pasaka, ndipo nilianza kuugua. Nilijikuta nikifanya vitu visivyo vya kawaida.
Nilimwaga maji ovyo ndani, nilimwaga nguo na vitu mbalimbali, kila kitu kilikuwa ovyo. Baada ya muda niligundua kufanya vitu siyo vya kawaida…Hivyo ndivyo nilivyoanza kuchanganyikiwa na hali hii imenitokea mara kwa mara.”
Aliongeza: “Yaliponitokea hayo, nilikuwa nikifanya kazi mkoani Kigoma katika hospitali iliyopo wilayani Kasulu (hakuitaja jina) ndipo kilikuwa kituo changu cha kazi.”
Pamoja na Dk Kishiwa kuwa na matatizo ya akili, imethibitika kuwa baadhi ya madaktari wa MNH wamekuwa wakikimbilia kwake kupata ushauri, lakini kubwa ni lile la kufundisha masomo ya ziada kwa baadhi ya wanafunzi MUHAS.
Pia amekuwa akifuatwa na watu wanaomfahamu hasa wanawake wakimwomba ushauri hata kuwaandikia dawa kutokana na maradhi waliyonayo. Mwandishi wa habari hii ni mmoja wa waliopata ushauri wa kitabibu kutoka kwa Dk Kishiwa.
Tiba na ushauri
Uchunguzi wa wiki kadhaa katika eneo la MNH, nyumbani kwake Chamazi na hata katika familia yake, umethibitisha kwamba Dk Kishiwa licha ya kuwa mgonjwa wa akili bado ni msaada mkubwa kwa watu wengi.
Gazeti hili lilishuhudia daktari huyo akimwelekeza mmoja wa madaktari wa MNH namna ya kumsaidia mgonjwa wake. Kwa mujibu wa mazungumzo yao, hali ya mgonjwa husika ilimchanganya daktari huyo, hivyo kutaka kupata msaada kwa Dk Kishiwa.
Uchunguzi pia ulibaini kuwa wakati fulani, Dk Kishiwa anakuwa katika hali ya kawaida na kuweza kutoa ushauri, hata kutibu kwa kuwaandikia dawa wagonjwa akiwa eneo hilo la Muhimbili.
Jioni moja gazeti hili lilishuhudia wanawake wawili waliobeba watoto mgongoni wakiwa na Dk Kishiwa, aliyekuwa akiwaandikia kitu kwenye karatasi. Baada ya tukio hilo mwandishi aliwauliza iwapo wanamfahamu, na walijibu; “Tunamfahamu, ni daktari alikuwa akituandikia dawa.”
Hata hivyo, uchunguzi ulibaini kuwa mambo yanapobadilika, Dk Kishiwa huwa mkali asiyetaka kuwa karibu na mtu au kuzungumza naye, huku akifanya vioja vinavyothibitisha hali yake ya matatizo ya akili. Hali hiyo ilimlazimisha mwandishi kuendelea kumfuatilia kwa siku kadhaa katika eneo hilo la MNH na kufanikiwa kuzungumza naye.
Kwa mujibu wa watu wanaomfahamu hasa madereva teksi wa eneo hilo, walisema Dk Kishiwa hushinda hapo na kwamba pamoja na kuwepo kwa wafanyabiasha na madereva wengi, daktari huyo humsikiliza dereva mmoja anayepatana naye na mara nyingi hutekeleza anayomweleza.
Kwa msaada wa dereva huyo, Dk Kishiwa anaeleza historia ya maisha yake kuwa alizaliwa Desemba 25, 1954, alipata elimu katika Shule ya Msingi Tumbi mkoani Tabora hadi darasa la nane na kuendelea na masomo kupitia shule kadhaa ikiwemo Sekondari ya Busonga na Sekondari ya St Mary’s ya Tabora.kwamba katika elimu ya sekondari alipata daraja A kwa masomo yote 11.
“Sikuwahi kufeli, nilipata daraja A katika masomo yote 11 niliyosoma yakiwemo kemia, baolojia, hisabati na civics. Baada ya hapo nilijiunga na jeshi kwa mujibu wa sheria kwa miezi sita katika kambi ya Mafinga,” anasema Kishiwa bila kutaja miaka aliyosoma.
Anakumbuka kuwa 1974 ndipo alijiunga na Chuo cha Tiba Muhimbili, ambapo alisoma kwa miaka mitano na kumaliza 1979, bila kufeli somo hata moja na baada ya hapo alipangwa kwenda Hospitali ya Bugando, Mwanza kikiwa ni kituo chake cha kazi cha kwanza.
Anasema alikaa Bugando kwa mwaka mmoja tu na mwaka uliofuata akapelekwa Wilaya ya Kasulu, Kigoma kama Mganga Mfawidhi na huko ndipo lilipoanzia tatizo alilonalo hadi sasa.
Kuugua akili
Anaeleza kuwa tangu Aprili 26, 1981 alipopatwa na tatizo la akili, amekuwa akipelekwa hospitali mara kadhaa na tatizo hilo kutulia, lakini bado hali haikuwa nzuri ingawa bado aliendelea kufanya kazi.
Anasema kuugua kwake kunahusishwa na imani za kishirikina, jambo ambalo si kweli na hajui nani aliyezusha.
Dk Kishiwa anasimulia kuwa baada hali yake kuwa nzuri hakuendelea kukaa Kigoma bali alirudishwa Bugando, Mwanza na anadai kwamba kati ya 1986 na 1994 alifanya kazi Muhimbili, lakini alisimamishwa kwa sababu ambazo hadi leo hazifahamu.
“Nililipwa Sh3.4 milioni ambazo nilizitumia kununua shamba eneo la Chamazi na kujenga nyumba ninayoishi sasa,” anabainisha.
Anaendelea kueleza kuwa licha ya kufanya kazi Muhimbili, pia aliwahi kufanya katika Hospitali ya Vikuruti na Chamazi wilayani Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo alikuwa akilipwa posho na Wizara ya Afya.
“Nilipokuwa nikifanya kazi Vikuruti, nilitakiwa nipewe maharage na unga na vitu muhimu bure, lakini nilipewa mara moja tu,”analalamika Kishiwa.
Kauli ya MHN
Hata hivyo, Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Aminiel Eligaesha, anasema Kishiwa hakuwahi kufanya kazi katika hospitali hiyo licha ya kusikia kuwa aliwahi kuwa daktari.
“Kwenye kumbukumbu za hapa Muhimbili hakuna daktari kama huyo ingawa kuna habari kuwa aliwahi kuwa daktari na kuna maprofesa ambao alisoma nao darasa moja. Niliwahi kusikia kuwa anawafundisha masomo ya ziada wanafunzi wa MUHAS,”anasema Eligaesha.
Profesa Victor Mwafongo MNH anathibitisha kwamba alisoma darasa moja na Dk Kishiwa, lakini hakuwahi kufanya naye kazi hospitalini hapo.
Anasema kuwa alipotezana na Kishiwa kwa muda na hakufuatilia alipo, lakini baadaye alipata taarifa kuwa ana matatizo ya akili na kufikishwa MNH kwa ajili ya matibabu.
“Namafahamu Kishiwa na nimesoma naye katika Chuo Kikuu cha Muhimbili, lakini sikuwahi kufanya naye kazi hapa Muhimbili. Kwa sasa humwona mara nyingi akizunguka hapa MNH, hukutana na kuzungumza naye kwa kuwa ananikumbuka vizuri na mimi namkumbuka,”anasema Mwafongo.
Anafafanua kuwa anachofahamu kuhusu Kishiwa ni kwamba anapata tiba hospitalini hapo inayomsaidia hata kuwa kama alivyo sasa.
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger