Home » » Kesho ni NYERERE DAY...Maadhimisho ya kumuenzi baba wa taifa yatafanyika mjini Dodoma Kesho..

Kesho ni NYERERE DAY...Maadhimisho ya kumuenzi baba wa taifa yatafanyika mjini Dodoma Kesho..

 
Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.Charles Magaya akiongea kuhusu maadhimisho ya Mwalimu Nyerere wakati wa kikao kazi kilichofanyika mjini Dodoma mapema leo.Kulia kwake ni Mkurugenzi Msaidizi Bw.Athanas Kolokota na Mkurugenzi Msaidizi Thomas Manyambula (kushoto).  

Na Happiness Shayo-Utumishi
Maadhimisho ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yanatarajiwa kufanyika kitaifa kesho katika viwanja vya Nyerere Square mjini Dodoma.

Hayo yalisewa na Mkurugenzi Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.Charles Magaya alipokuwa katika kikao kazi cha maandalizi ya siku hiyo mjini Dodoma.

Bw.Magaya alisema Siku ya kumuenzi Baba wa Taifa itaongozwa na mmoja wa washiriki wa Baba wa Taifa Balozi Job Lusinde.

“Maadhimisho hayo yataongozwa na mmoja wa washiriki wa Baba wa Taifa katika kupigania Uhuru wa Tanganyika Mheshimiwa Balozi Lusinde ambaye pia ni muasisi wa Chama cha TANU”alisema Bw.Magaya.

Sambamba na maadhimisho hayo Bw.Magaya alisema kuwa Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma imeandaa sinema mbalimbali za Mwalimu Nyerere zitakazoonyeshwa katika viwanja vya Nyerere Square leo kuanzia saa 12 jioni hadi saa 3 usiku.

Aidha,aliwataka wananchi wa mkoa wa Dodoma kushiriki katika maadhimisho hayo ya kumuenzi Baba wa Taifa.

Pia Bw.Magaya alitoa wito kwa viongozi wa Mkoa wa Dodoma kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye viwanja vya Nyerere Square ili kusikiliza hotuba mbalimbali kutoka kwa viongozi waliofanya kazi karibu na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Maadhimisho ya Baba wa Taifa hufanyika Oktoba 14 ya kila mwaka ambapo mada mbalimbali hutolewa na viongozi waasisi wa Taifa la Tanzania.
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger