Home » » MLIMANI CITY YASITISHA UKAGUZI WA MAGARI NA WATU KWA MADAI KWAMBA UNAPUNGUZA WATEJA

MLIMANI CITY YASITISHA UKAGUZI WA MAGARI NA WATU KWA MADAI KWAMBA UNAPUNGUZA WATEJA



Siku chache baada ya kuanzisha ukaguzi wa magari na watu wanaoingia katika maduka ya Mlimani City, ukaguzi huo sasa umesitishwa.
  

Hatua hiyo ilifuatia tishio la ugaidi baada ya duka la Westgate la Nairobi nchini Kenya kushambuliwa na kikundi cha Al-shabab na kusababisha mauaji ya watu 68 na wengi kujeruhiwa.
 

Mbali na Mlimani City lililopo Barabara ya Sam Nujoma, jijini Dar es Salaam, maduka mengine makubwa kama vile Quality Plaza lililopo Barabara ya Nyerere nalo lilianzisha ukaguzi kwa wateja wake.
 
Hata hivyo uchunguzi wa  hivi karibuni umebainisha kuondolewa kwa ukaguzi uliokuwa ukifanywa kwa wateja na magari yanayoingia dukani hapo, kwa madai kuwa unapunguza wateja.
 
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, askari wa kike wa kampuni ya Omega Nitro inayolinda duka hilo, alisema kuwa hatua hiyo ilikuja Oktoba 16 mwaka huu.
 
“Nakumbuka Jumatano baada ya kumaliza ‘shift’ niliacha ukaguzi ukiendelea, lakini niliporudi Ijumaa nikaambiwa umesitishwa mara moja,” alisema na kuongeza:
 
 
“Kwa kweli ukaguzi wenyewe ulikuwa mgumu kwani hatukuwa na vifaa vya kutosha na wateja ni wengi,” alisema na kuongeza: “Katika ukaguzi tulikuta watu wengi na silaha hasa bastola wakimiliki kihalali.”
 
 
Jitihada za kuupata uongozi wa Mlimani City hazikufanikiwa kwa kile kilichoelezwa kuwa yuko likizo. Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema hana taarifa ya kusitishwa kwa ukaguzi, lakini akasisitiza kuwa hilo ni suala lao binafsi.
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger