Balozi Isaac Abraham Sepetu ambaye ni baba yake mzazi na Wema Sepetu, anatarajiwa kuzikwa Jumatano hii visiwani Zanzibar. Mwili wa marehemu utasafirishwa kesho asubuhi kuelekea visiwani humo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma, leo wameungana na watu wengi wa karibu wa familia ya Wema kuwapa pole wafiwa akiwemo mama yake, Bi. Mariam Sepetu.
Balozi Sepetu alifariki jana baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya kisukari na kiharusi na alikuwa amelazwa kwenye hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam.
Balozi Sepetu aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje mnamo miaka ya 1970 wakati wa utawala wa awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Julius KambaragE Nyerere.
Vilevile, aliwahi kuwa balozi nchini Urusi tangu mwaka 1982 wakati wa utawala huohuo wa Nyerere. Hadi anafariki, Mzee Sepetu alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Uwekezaji wa Vitega Uchumi Zanzibar.