Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema atasaini muswaada tata unaopinga ushoga na kuwa sheria kamili.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni onyo kwa wanaotetea vitendo vya mahusiano ya jinsia moja kuwa watashughulikiwa vikali nchini humo.
Mwezi
 uliopita kiongozi huyo alipanga kuachana na muswaada huo ambao umekuwa 
ukikosolewa vikali na wahisani kutoka mataifa ya Magharibi na 
wanaharakati wa haki za binaadamu tangu ulipowasilishwa mwaka 2009. 
Mapenzi ya jinsia moja ni mwiko katika mataifa ya Afrika na kinyume cha 
sheria kwa mataifa 37.
 
Wasiwasi wa mashoga wa Afrika
Wanaharakati
 wa haki za binaadamu wanasema Waafrika wachache waliojitangaza kuwa 
mashoga, wanahofu ya kufungwa, kukabiliwa na vurugu na kupoteza ajira 
zao.
Wakati
 wa mkutano wake na chama tawala nchini Uganda NRM kundi la wanasayasi 
liliwasilisha utafiti wao kuhusu mapenzi ya jinsia moja kwa rais 
Museveni. Msemaji wa mkutano huo, wa NRA Anite Evelyn katika taarifa 
yake alisema kuwa "Museveni alitangaza atasaini muswaada huo kwa vile 
swali lile la iwapo mtu anaweza kuzaliwa shoga au hapana limejibiwa".
Uchunguzi wa mawaziri
Katika
 taarifa yake kamati ya mawaziri iliyokuwa ikilifanyia uchunguzi suala 
hilo ilisema Ijumaa (14.02.2014) hakuna vinasaba vya mapenzi ya jinsia 
moja na kwa hivyo si ugonjwa lakini ni tabia isiyo ya kawaida ambapo mtu
 anaweza kujifunza tu kwa kupitia uzoefu katika maisha.
Katika
 mkutano na chama tawala cha NRM, Mshauri wa Rais katika masuala ya 
Kisayansi, Dokta Richard Tushemereirwe alimwambia kwamba "mapenzi ya 
jinsia moja yana athari kubwa kwa afya za watu kwa hivyo si jambo la 
kuachwa liendelee hata kidogo".
Muswaada
 wa kupinga uhusiano wa jinsia moja uliwasilishwa bungeni mwaka 2009, 
ambapo awali ulikuwa ukipendekeza adhabu ya kifo kwa wanaoshiriki 
vitendo vya ngono kwa watu wa jinisia moja, lakini ukafanyiwa 
marekebisho kwa kuweka adhabu ya vifungo vya awamu gerezani na maisha 
kwa kile kilichotajwa kuwa mapenzi ya jinsia moja ya kuchochewa.
Rais
 Museveni alisisitiza kuwa , wahamasishaji, wanaojionesha na wote 
wanaoshiriki vitendo vya ngono kwa watu wa jinsia moja kwa sababu za 
ukaidi wa kutumwa , hawatavumiliwa na watakabiliwa vikali.
Chanzo, dw.de/swahili
 
 
 
 
 
 
 
