JESHI la Polisi mkoani hapa kwa kushirikiana na wakazi wa Kijiji cha Maili kumi wilayani Korogwe wamefanikiwa kuwakamata watu saba kwa tuhuma za kuhusika na kuweka mabomu yaliyokuwa yameandaliwa tayari kwa kulipuka kwenye nyumba mbili tofauti za ibada.
Pamoja na mabomu hayo, watuhumiwa hao ambao majina yao yanahifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi wanatuhumiwa kuhusika na kukutwa na vifaa mbalimbali vya kutengenezea milipuko ya mabomu hayo pamoja na silaha za jadi ambazo pia zilikuwa zimefichwa katika nyumba hizo za ibada katika Kijiji cha Maili kumi wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Watu hao walikamatwa wakiwa na chupa 10 ambapo tano zilikuwa na petrol zikiwa na tambi zake ndani, gololi 103 ambazo hutumiwa kwa milipuko, galoni kubwa mbili zilizokuwa na lita nne za petrol, majambia, mishale yenye sumu, soksi za kuzuia uso (mask) upinde, daftari lenye mafunzo ya kijeshi kuhusu namna kufungua na kufunga silaha.
Vifaa vingine ni mapanga, visu, mifuko ya sandarusi, manati, vifuniko 12 vya maji, kofia nne na vitambaa vya kufunga kichwani pamoja na tende walizokuwa wakitumia kwa chakula.
Akizungumza ofisini kwake leo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga Constantine Massawe alisema kuwa watu hao walikamatwa Disemba 17 mwaka huu majira ya saa 2.00 usiku huko wilayani Korogwe.
Kamanda Massawe alisema kuwa Askari Polisi wakiwa kaika kizuizi cha Maili Kumi wilaya ya Korogwe waliwatilia shaka vijana watatu wa kiume waliokuwa wamebeba vifurishi na walipotaka wasimame walikimbilia msituni na ndipo mmoja alipokamatwa na Askari hao.
“sasa baada ya kukamatwa huyu mmoja na ndipo alipopekuliwa na kukutwa na vifaa hivyo kwenye begi lake na ndipo msako wa kuwatafuta hawa wengine ulipoanza,” alisema Kamanda huyo.
Hata hivyo alisema kuwa alisema kuwa katika msako huo ambao ulifanywa na Polisi kwa kushirikiana na wananchi wa eneo la Maili Kumi ndipo walipobaini kuwepo kwa vifaa vingine katika nyumba mbili tofauti za ibada zilizopo Kijijini hapo.
Alisema watuhumiwa hao baada ya mwenzao kukamatwa walikimbia kujificha kwenye nyumba hizo za ibada ndipo wakazi wa maeneo hayo walipowatilia mashaka na kutoa taarifa kwa Polisi.
“Baada ya kukimbizwa wakaona mahali salama kwao ni kwenye nyumba za ibada lakini wananchi wa eneo lile waliwatilia shaka na kuamua kutoa taarifa ndipo yalipokutwa hayo mabomu ambayo yalikuwa yameshaandaliwa kulipuka kwani kulikuwa na petrol na tambi ndani ya chupa hizo na zile gololi hutumika kama silaha zinapolipuka,” alifafanua Kamanda Massawe.
Hata hivyo kwa mujibu wa Kamanda huyo ni kwamba baada ya mahojiano ya Polisi na watuhumiwa hao walibaini kuwa ni miongoni mwa wale waliokimbi katika oparesheni ya kuwasaka wahalifu iliyofanyika mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu huko wilayani Kilindi.
“Hawa ni miongoni mwa wale waliosababisha machafuko wilayani Kilindi ambapo Mgambo aliuawa sasa wengine walikimbia na inaonekana nao hawa wapo katika mtandao huo,” alisema.
Kamanda Massawe alitoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Tanga kutoa taarifa mara moja kwa Polisi mara wanapobaini kuwepo kwa watu ambao wanawatilia mashaka kwenye maeneo yao.