Serikali imeondoa kodi ya kadi za simu iliyopitishwa na wabunge katika Mkutano wa 13 wa Bunge ambayo ililalamikiwa na wadau na watumiaji wa simu nchini.
Hata hivyo, kodi hiyo imerejeshwa kwa staili
nyingine baada ya kuongezwa katika tozo la kodi ya manunuzi iliyokuwepo
kutoka asilimia 14.5 ya awali hadi asilimia 17.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Naibu Waziri wa Fedha
Saada Mkuya Salumu, bungeni juzi wakati akisoma Muswada wa Sheria ya
Manunuzi wa mwaka 2013, ambao uliingizwa bungeni kwa hati ya dharura.
Muswada huo ulipelekwa bungeni kwa hati ya dharura
baada ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia upitishwe na Bunge kabla ya kuwa
sheria kutokana na malalamiko yaliyokuwa yametanda kila kona.
Katika muswada huo ambao ulichukua muda mfupi na
kuchangiwa na wabunge wachache, Serikali imesema kuwa kilio cha
Watanzania kilisikika na Serikali haikuona haja ya kuendelea na kodi
hiyo, badala yake ikaamua kutafuta njia nyingine.
“Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kutafuta njia
nyingine ya kukusanya mapato hayo ambayo yalilengwa kupatikana kwa zaidi
ya Sh170 bilioni ambayo yangepelekwa katika huduma za umeme na maji,
hata hivyo tumepata njia mbadala,” alisema Mkuya.
Alitaja njia hiyo ni kukusanya katika mitandao ya
kimawasiliano yote ambayo awali hawakuwa wameilenga na kwamba kupitia
njia hizo, wanaweza kupata kiasi cha Sh140 bilioni huku kiasi cha Sh30
zikitarajia kutolewa na kampuni za mawasiliano.
Katika maelezo yake, alisema kuwa kampuni za simu
nchini yalikubali kutoa kiasi cha Sh30 bilioni ili kuisaidia Serikali
katika kufidia pengo ambalo lingepatikana kwani tayari bajeti
ilishapangwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Andrew
Chenge alisema kuwa Kamati ilikutana juzi mjini Dodoma kwa dharura na
kukubaliana jinsi ya kurekebisha kodi na kutafuta njia nyingine ambayo
ni kutoza kuongeza kodi katika manunuzi.
Kwa upande wake msemaji wa Kambi ya Upinzani kaika
Wizara hiyo Christina Lissu, alilaumu mpango huo kwa madai kuwa hakuna
kitu kilichoondolewa na badala yake kilichofanyika ni kiinimacho kwa
Watanzania.
-Mwananchi
-Mwananchi