HATUA
ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia kutengua uteuzi wa mawaziri wanne, sasa
ina kila dalili za kumpa nafasi ya kuchukua uamuzi wenye mwelekeo mpya
ndani ya muda mfupi ujao kuanzia sasa...
Ni
katika mwelekeo huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye naye alitakiwa
na wabunge kujiuzulu, licha ya juzi kutokuwa tayari kulizungumzia jambo
hilo wakati akitangaza uamuzi wa Rais kutengua uteuzi wa mawaziri hao
wanne, anaaminika kutangaza uamuzi huo huku hatma yake ya kuondoka
madarakani ikiwa imezungukwa na wingu la shaka.
Ingawa
hadi sasa Pinda mwenyewe amekwishasema yuko tayari kung’oka na kwamba
atafurahi kama uamuzi huo utachukuliwa dhidi yake, lakini hatua
iliyochukuliwa na Rais Jakaya Kikwete sasa inadhihirisha kuwepo kwa
dalili za kutaka kumnusuru kiongozi huyo dhidi ya shinikizo la wabunge,
ambao mara kwa mara wamekuwa wakimtaka ang’oke, wakimtuhumu kwa uzembe.
Baadhi
ya wadadisi na wafuatiliaji wa mambo waliochambua uamuzi huu wa sasa wa
Rais Kikwete, wanaeleza kuwa huenda kiongozi huyo akawa anatumia staili
ile ile aliyoitumia mwaka mmoja uliopita kumnusuru Pinda.
Wanaeleza
kuwa, mwaka 2012, Kikwete alilazimika kufanya mabadiliko ya Baraza la
Mawaziri kwa kuwaweka kando mawaziri nane ambao wabunge walikuwa
wakishinikiza wang’olewe pamoja na Pinda, baada ya kukasirishwa na
ripoti ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG),
iliyowatuhumu mawaziri hao kwa ubadhirifu.
Hata
hivyo, baada ya kufanya mabadiliko hayo, yaliyoshuhudia mawaziri wa
Nishati na Madini, William Ngeleja, Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige,
Afya Hadji Mponda, Viwanda na Biashara Cyril Chami, Uchukuzi, Omari
Nundu na wengine, Rais Kikwete hakumuondoa Pinda na tishio la wabunge
kutaka kumuondoa kwa kura ya kutokuwa na imani naye nalo lilififishwa na
hatua hiyo.
Wakati
wadadisi na wachambuzi wa mambo wakiwa na mtizamo huo, zipo taarifa
zinazoeleza kuwa ugumu wa Rais Kikwete kuchukua hatua ya kumuondoa Pinda
unatokana na hatua yake ya kutaka kuinusuru serikali na mzigo wa
gharama za kuwalea mawaziri wakuu pindi wanapoondoka kwenye nyadhifa
zao.
Hatari
hiyo ya serikali kubaki na mzigo mkubwa wa viongozi wakuu wastaafu,
ndiyo inayotajwa wakati fulani mwaka 1994 kumlazimisha Rais Ali Hassan
Mwinyi kumrudisha kwenye nafasi ya uwaziri mkuu, Cleopa Msuya, aliyepata
kuhudumu kwenye nafasi kama hiyo wakati wa utawala wa Mwalimu Julius
Nyerere.
Hadi
sasa Tanzania ina mawaziri wakuu wastaafu watano, ambao ni John
Malecela, Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba, Frederick Sumaye na Edward
Lowassa.
Hata
hivyo, taarifa ambazo RAI Jumapili limezipata zinaeleza kuwa, Pinda
binafsi yuko tayari kukabidhi madaraka, ingawa uamuzi huo haijulikani
utachukuliwa namna gani na Rais Kikwete pindi atakaporejea Alhamisi wiki
hii, akitokea Marekani, alikokuwa kwenye matibabu.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo zilizolifikia gazeti hili, tayari Pinda
amemueleza Rais Kikwete juu ya azma yake hiyo, huku nyingine zikieleza
kuwa amekwishamuandikia barua ya kujiuzulu.
Ingawa
si Pinda wala Ikulu waliopatikana kuthibitisha taarifa hizo hadi
tunakwenda mitamboni usiku wa kuamkia leo, ni wazi kwamba, hatua ya sasa
ya Rais Kikwete inakuja kama mbinu ya serikali yake kutaka kujisafisha
kupitia mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri, ili kukwepa lawama ambazo
zimekuwa zikielekezwa mara kwa mara na jamii dhidi ya serikali yake
kuhusu vitendo mbalimbali vya ubadhirifu na ukiukwaji wa haki za
binadamu.
Tayari mawaziri wawili majina yao yameanza kutajwa kurithi nafasi ya Pinda, ikiwa ataondoka katika nafasi hiyo.
Mawaziri hao ni Waziri wa Miundombinu, Dk. John Magufuli na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira.
Aidha
kitendo hicho cha Rais kuamua kutengua uteuzi wa mawaziri wa aina ya
Emanuel Nchimbi wa Mambo ya Ndani, Balozi Khamis Kagasheki wa Maliasili
na Utalii, na David Mathayo wa Kilimo kwa tuhuma zilizotokana na
Operesheni Tokomeza, inatajwa kuliweka njia panda Baraza zima la
Mawaziri, hususan wale wanaotajwa kuwa ni mawaziri mizigo.
Taarifa
zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa uamuzi huo wa Rais Kikwete
umewashtua mawaziri karibu wote, huku baadhi yao wakipata shaka kama
wataendelea kubaki katika nyadhifa zao.
Ni
hatua hiyo pia inatajwa kumpatia nafasi ya kuwaondoa au kuwahamisha
wizara mawaziri wengine, wakiwamo wale waliopachikwa jina la mawaziri
mizigo pindi atakapofanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.
Mawaziri
wanaotajwa kuwa ni mizigo na ambao tayari wamekwishahojiwa na Kamati
Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Tamisemi), Hawa Ghasia.
Wengine
ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Waziri wa
Fedha, William Mgimwa, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah
Kigoda, na Waziri wa Nchi Menejimenti na Utumishi wa Umma, Celine
Kombani.
Katika
mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri yanayotarajiwa kufanywa ndani ya
muda mfupi, pia huenda yakatoa nafasi kwa baadhi ya mawaziri ama
kuondoka au kubaki, lakini pia kuwajumuisha wapya.
Miongoni
mwa wanaotajwa kujumuishwa katika baraza jipya la Mawaziri ni pamoja na
Dk. Asha Rose Migiro, ambaye hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alimteua
kwenye nafasi ya ubunge.