Home » » RIPOTI: MATEJA WAPEANA ULEVI KWA NJIA YA DAMU...!! Soma hapa kwa habri kamili..

RIPOTI: MATEJA WAPEANA ULEVI KWA NJIA YA DAMU...!! Soma hapa kwa habri kamili..

Ukosefu wa fedha za kununulia dawa za kulevya, umewafanya walevi, ‘mateja,’ kubuni njia ya hatari, kwa kunyonya damu yenye kilevi toka kwa aliyetumia na kujidunga.
‘Mateja’ wamefikia hatua ya kuchangishana fedha na kununua kete moja ya dawa aina ya heroin yenye ubora, mmoja wao hutumia na akilewa wengine hupata ulevi huo kwa kumnyonya damu kwa kutumia sindano ya hospitali na kujidunga.
Reuben (si jina lake halisi) aliyenyong’onyea mwili mwenye midomo yenye rangi nyeusi anasema aliwahi kubadilishana damu na watu zaidi ya 20, damu anayoeleza kuwa alikuwa akibadilishana vijiweni, kwenye kumbi za starehe na maskani bila kuzingatia taratibu wala athari zake.
“Nimewahi kununua damu kwa watu waliotumia heroin halisi, pia ‘maskani’ (kijiweni) tulikuwa tukichanga fedha na kununua heroin halisi kisha mmoja anatumia na baadaye tulichukua damu kwake kwa njia ya bomba la sindano,” anasema Reuben akiwa kwenye foleni ya matibabu ya kliniki ya ‘Methadone’ iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Ukishatumia sana ile ya buku baadaye unakuwa huridhiki sana hata hivyo itakulazimu utumie zaidi ya moja kwa siku, kwani ile huchakachuliwa sana kwa kuchanganywa na vidonge aina ya ‘Valium’ ambavyo hutumiwa kama dawa za usingizi,” alisema Reuben. Heroin ambayo huuzwa kwa gharama ya kuanzia sh 1,000 kwa kete hasa ile ‘iliyochakachuliwa’, asilimia kubwa wamekuwa wakishindwa kununua heroin halisi ambayo huuzwa kwa bei ya juu, hivyo huishia kuomba au kununua damu kwa aliyetumia aina hiyo ili kupata ulevi.
Akizungumza na gazeti hili, Mtaalamu wa Afya ya Akili (psychiatric) na Mkuu wa Kliniki ya Matibabu ya Dawa za Kulevya ‘Methadone’ kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Frank Masao, anasema tatizo hilo wameligundua hivi sasa baada ya kuzungumza na waathirika wa dawa hizo.
“Baada ya kuzungumza na waathirika hawa tumegundua kuwa wamekuwa na mazoea ya kubadilishana damu, pindi mmoja anaposhindwa kununua heroin, wao hawazingatii makundi ya damu wanatoleana tu, vitendo hivi vimekuwa vikifanywa sana kwa mazoea bila kujali athari za mbeleni,” alisema Dk Masao.
Hata hivyo, Reuben anasema alianza kubadilishana damu mwaka 2009, wakati huo walikuwa wakinunua Kinondoni kwa Manyanya, jijini Dar es Salaam.
“Maskani ambayo nilikuwa nanunua unga ni Kinondoni kwa Manyanya, pale mpaka mara ya mwisho naachana na dawa za kulevya mwaka mmoja uliopita, nilikuwa nanunua hapo. Japokuwa nikisafiri nilikuwa natafuta hukohuko mkoani pia zipo ilimradi upewe ramani na watu wanaojua soko lilipo,” alisema Reuben.
Amina anayeishi Temeke jijini Dar es Salaam, naye ni mmoja kati ya waathirika wa zoezi la kubadilishana damu na hakumbuki idadi kamili ya watu aliokuwa akibadilishana damu japokuwa anasema si wengi.
“Nilikuwa natumia heroin nyeupe na ile ya brown miaka 14 iliyopita, wakati huo nilikuwa nafanya shughuli za biashara, nilikuwa vizuri kifedha lakini leo kama unavyoniona nimechoka,” anaanza kwa kusema mwanamke huyo aliyejichora ‘tatoo’ nyingi mwilini mwake.
“Nilifika hapa Muhimbili baada ya kuzidiwa na dawa hizi na uchumi wangu uliyumba, ilifikia hatua nilianza kubadilishana damu na wengine na hata niliiba na kupora ili tu nipate ‘unga’ kwani nikienda kuomba kazi walinikatalia na kuniita teja, sikuwa na sehemu ya kuniongezea kipato. Nawashukuru Asasi ya Blucose ambao walinileta hapa,” anasema Amina na kuwataka wanawake kutojiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya.
Hata hivyo, Dk Masao amefafanua kuwa matumizi ya dawa za kulevya humfanya mtu yoyote aliyeambukizwa Virusi vya Ukimwi CD4 zake kushuka haraka, huku akipoteza uwezo wake kiutendaji na hata akili yake kuathirika kwa kiwango kikubwa.
Alisema maambukizi ya virusi vya Ukimwi yapo juu sana kwa waathirika wa dawa za heroin waliofika katika kituo hicho kwa ajili ya matibabu ya methadone, lakini hata hivyo wapo walioambukizwa homa ya ini, hao hugundulika baada ya vipimo kwani mwathirika yeyote lazima afanyiwe vipimo vyote ili kupatiwa matibabu kwa urahisi,
“Asilimia 32 ya wagonjwa wanaotibiwa katika kliniki hii wana maambukizi ya virusi vya Ukimwi huku asilimia 60 wana maambukizi ya homa ya ini (hepatitis C) na asilimia 31 wana maambukizi ya homa ya ini aina ya pili (hepatitis B) huku asilimia 11 wakiwa na kifua kikuu,” anasema Masao huku akifafanua kuwa watu zaidi ya 25,000 nchini Tanzania wanajidunga dawa aina ya heroin huku 15,000 wakitokea jijini Dar es Salaam.
Dk Masao ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Afya ya Akili nchini, anasema Hospitali ya Taifa Muhimbili inahudumia wagonjwa 640 huku 50 kati yao ni wanawake na kufanya idadi yao kuwa asilimia saba.
Itaendelea Jumapili ijayo…..
“Kitengo chetu kilianza kutoa huduma hii Februari 2011 na tulianza kupokea wagonjwa wanne kwa siku na ilifikia hatua tulikuwa tukipokea hata 20 waliohitaji huduma kutoka kwetu na mpaka sasa tuna wagonjwa 640. Kati ya hawa 18 tuliwaondoa kutokana na matatizo mbalimbali. Wapo waliokuwa wakifika na silaha mbalimbali na hawa walikuwa tishio kwa kitengo hiki.”
Dk Masao anasema licha ya kuondolewa katika kitengo hicho walio wengi wamekuwa wakirudishwa tena; “Hata kama akifanya vurugu tutamwondoa lakini baadaye lazima tumfuate na kama akikiri kosa na kuahidi kubadilika tunamrudisha na anaendelea na dozi. Kila anayetibiwa hapa sharti la kwanza ni lazima makazi yake halisi yajulikane hivyo inakuwa rahisi kumfuatilia mgonjwa huyu iwapo atakatisha dozi ili kujua sababu ni nini.”
Akifafanua kuhusu dawa inayotumika kuondoa sumu ya dawa za kulevya katika mwili wa mwathirika, Dk Masau alisema methadone humwezesha mgonjwa kutosikia hamu ya kutumia dawa hizo, sambamba na kumwondolea maumivu mwilini.
“Dawa hii wanayopewa inawasaidia mwili kutokuwa na maumivu. Maana mtu anaposikia maumivu hapo ndipo anapoanza kuhangaika kutafuta heroin ili ajidunge. Lakini akipata methadone huwa salama na hawezi kupata tena hamu ila masharti ya dawa hii ukitumia hupaswi kurudi tena na kuanza kujidunga,” alisema Dk Masau na kuongeza; “Dawa hii yenye thamani ya dola 75,000 sawa na Sh124 milioni tumepewa na wafadhili kutoka Canada ambapo walitoa kiasi cha kilogramu 50 ambazo huweza kutumika kwa kipindi cha miaka miwili.”
Anafafanua kuwa dozi hiyo hutolewa kila siku katika hospitali hiyo kwa kiasi cha dozi ya mililita 1.5 kwa kila mwathirika kila siku huku wengine wakitunzwa wodini kutokana na kuathirika kwa kiwango kikubwa, hata hivyo aliweka wazi kuwa idadi kubwa wamekuwa wakishindwa kuhimili gharama za usafiri kila siku.
Alisema Tanzania ni nchi ya kwanza katika nchi za Jangwa la Sahara kuwa na kitengo cha methadone.
“Tanzania ni nchi ya kwanza katika nchi za Jangwa la Sahara kuanza kutoa matibabu ya methadone, lakini pia tunafundisha nchi nyingi kutoa huduma hii wakiwemo Nigeria, Msumbiji, Kenya, Uganda, Zambia na nchi nyinginezo ambao hufika hapa Muhimbili kwa ajili ya kupata utaalamu huu,” alisema Dk Masao.
Alisema utaalamu hasa kuhusu matumizi ya dawa hiyo sambamba na ujuzi wa kutoa matibabu hayo waliupata katika nchi ya Vietnam.
“Vietnam ndipo hasa tulipopata ujuzi huu na huko tumekuwa tukiwapeleka wataalamu wengi kujifunza. Moja kati ya changamoto zilizopo katika kitengo hiki ni ukosefu wa watoa huduma, wengi hawapo radhi kujitolea katika kutoa matibabu kwenye kitengo hiki. Hatuna wanasaikolojia wa kutosha, manesi na madaktari”
Dk Masao anasema kitengo hicho kimekuwa kikipokea pia wanandoa ambao wamekuwa wakifika kwa pamoja kwa nia ya kupata huduma hiyo ili waachane na matumizi ya dawa za kulevya.
“Tunapokea hapa wanandoa wanaohitaji kuacha na walio wengi huwa waaminifu. Mpaka sasa watu waliopona na kuacha kabisa tunawatumia katika kuhamasisha wengine kuachana na matumizi ya dawa hizi.”
Aliitaja mikoa inayoongoza kwa waathirika wa dawa za kulevya kuwa ni Mbeya, Dodoma, Arusha , Tanga na Morogoro.
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger