Dar
es Salaam. Siku moja baada ya maudhui ya Ripoti ya Tume iliyoundwa
kuchunguza matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana kuwekwa wazi, wadau
wa elimu wamekiri na kusema kuwa mfumo wa elimu ya Tanzania upo katika
hali mbaya.
Akizungumza na
gazeti hili jana, Mbunge wa kuteuliwa na Rais, James Mbatia alisema
matokeo ya tume hiyo yanaonyesha udhaifu wa hali ya juu katika sekta ya
elimu jambo ambalo alishawahi kulisema katika hoja maalumu bungeni.
Mbatia, ambaye
pia ni Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, alisema alishawahi kuishauri
Serikali kuufumua mfumo wa elimu nchini na kuanza upya ili kunusuru
taifa la kesho ambalo ndilo linaloathirika na rasilimali watu zisizo na
ubora.
Matokeo ya
kidato cha nne ya mwaka jana yalionyesha kuwa asilimia 60.6 ya wanafunzi
Tanzania walipata alama sifuri na wanafunzi 23,520 sawa na asilimia
tano ndiyo waliofaulu jambo ambalo lilisababisha Waziri Mkuu Mizengo
Pinda kuunda tume ya kuchunguza matokeo hayo.
Baadaye, mitihani hiyo ilisahihishwa upya na Pinda kukabidhiwa matokeo Juni, mwaka huu.
“Nilishasema
katika hoja yangu bungeni Januari 31 na Februari 1, mwaka huu nikamwomba
waziri anionyeshe mitaala ya elimu ya sasa, lakini hakuitoa,” alisema
Mbatia.
Mbatia alisema
ili taifa hili liondokane na janga la elimu lililopo halina budi
kukubali kuwa ni kweli Tanzania ipo katika janga la elimu na kuunda dira
ya elimu itakayotuongoza katika safari ya elimu nchini.
Mbatia
aliongeza kuwa elimu ya Tanzania ipo mahututi na kuwa kila mwaka
wanafunzi wanaomaliza katika shule mbalimbali hawana sifa za kutosha za
kuweza kushindana katika masoko ya kimataifa.
“Tumeshaanza
kuona taifa linaangamia kwa sababu ya ubovu wa elimu, ni lazima tukiri
hilo kwa sababu hata Rais alikiri na kuikubali hoja yangu Aprili 30
mwaka huu alipokuwa mkoani Mbeya” alisema Mbatia
Mbunge huyu
ambaye awali aliteuliwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa tume ya uchunguzi
wa matokeo haya na kukataa kushiriki alisema, ili Serikali iondokane na
janga hili haina budi kuunda Kamati ya Bunge ambayo itaisimamia Serikali
na kutoa mawazo mapana kuhusu elimu.
Mbatia
alishauri Bunge lisiegemee itikadi za vyama au porojo za kutaka sifa za
kisiasa na badala yake suala la elimu lijadiliwe kwa maslahi ya taifa.
Mdau mwingine
wa elimu, Dk Method Samwel, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Elimu
cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUSE), alisema tatizo la elimu hapa
nchini lielekezwe zaidi kwenye mfumo uliopo kuliko laumu taasisi au mtu
mmoja mmoja.
Dk Samwel
alisema tangu zamani mfumo wa elimu umekuwa ni wa kudorora na haya ni
matokeo ya mfumo huo ambao haukuwa na misingi imara kwa muda mrefu.
Alitolea mfano
wanaokwenda kusomea ualimu wengi ni wale waliofeli kwa kupata daraja la
nne, jambo ambalo linasababisha wataalamu wa kada hiyo kuwa ni wale
waliofeli pekee.
“Yapo mambo
mengi yanayotakiwa kufanyiwa kazi katika sekta ya elimu Tanzania, suala
la kudai kuwa Baraza la Mitihani na Taasisi kuwa ndizo taasisi zenye
makosa, hazina ukweli,” alisema.
Hata hivyo, Dk
Samwel alisema, tume hiyo bado ina maswali mengi ya kujibu kulingana na
walichokisema katika sehemu ya ripoti yao.
“Nashindwa
kuelewa kwa sababu kila nikisoma majibu ya tume hiyo napata maswali
mengi zaidi. Kwa mfano, walimu waliofanya mtihani wakafeli walipewa muda
wa kujiandaa? “ alihoji na kuongeza:
“Na kuhusu
mitihani ya Tanzania kuonekana kuwa ni migumu zaidi, Je waliwapa
mitihani ya Tanzania wanafunzi wa nchi nyingine au walitumia mbinu gani
kupata matokeo hayo?”
Hata hivyo,
Mkuu wa Kitivo cha Elimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila
Mkumbo, alipinga ripoti ya tume hiyo na kusema kuwa wamepotosha taarifa
kwani tatizo halikuwa katika mtihani bali ni wanafunzi wenyewe wamefeli.
Dk Mkumbo
amesema tatizo si la walimu, wala baraza, wala mitihani yenyewe bali
ukweli utabaki kuwa wanafunzi walifeli mtihani wa Kidato cha Nne kwa
sababu ya mfumo mbovu wa elimu.
Mhadhiri huyo
alihoji tena kuwa tume hiyo ilitumia njia gani kujua kuwa mtihani wa
Sayansi ulihitaji saa sita kuufanya na ni kwa mbinu gani waliupima
mtihani wa Tanzania na kujua kuwa ni mgumu kuliko mitihani mingine.
“Nilipata
ripoti fulani iliyoonyesha kuwa mitihani ya Tanzania ni mizuri na haina
matatizo, ripoti ilionyesha kuwa haina chembe ya mashaka na inatungwa
kwa ustadi. Tusitafute sababu, tatizo si mitihani ni wanafunzi wenyewe
wamefeli,” alisema.
Pia, Dk Mkumbo
alisema kuwa ni dharau kubwa kusema kuwa baadhi ya wasahihishaji
hawakuwa na sifa kwani hilo ni tusi kubwa kwa walimu kwani wao ndiyo
wamekuwa wakisahihisha kila siku.
Naye Mwenyekiti
wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi nchini,(Tamongsco), Albert
Katagira alisema si kweli kuwa mtihani ulikuwa mgumu bali tatizo lipo
katika uandaaji wa wanafunzi.
Mtihani
ulikuwan sahihi kabisa, mbona wanafunzi wengine walifaulu. Ni wanafunzi
wenyewe, ambao nao hatuwezi kuwalaumu moja kwa moja,” alisema Katagira.
Alisema taifa
bado lina tatizo katika mfumo wa elimu na kuweka mkazo katika masomo ya
sayansi na hisabati ambayo yanaonekana kuwa magumu kwa wanafunzi wengi.
Mwanafunzi wa
Shule ya Sekondari ya Mafinga, Mustapha Mambea alisema, mtihani wa
Fizikia na Kemia haikuwa migumu, lakini kuna mada kadhaa ambazo
hawakufundishwa.
Profesa Mchome aongea
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alisema kuwa
wameshindwa kuiweka hadharani ripoti hiyo kwa kuwa bado inafanyiwa kazi
serikalini.
Profesa Mchome,
ambaye ndio aliongoza tume hiyo, alisema kuwa ripoti hiyo inatakiwa
kupelekwa kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kujadiliwa.
Alidokeza, hata
hivyo, tayari walikuwa wameanza kufanyia kazi baadhi ya vitu
vinavyotakiwa kufanyiwa kazi haraka kwenye ripoti hiyo.
Katibu Mkuu wa
Necta, Dk Joyce Ndalichako, ambaye ameomba likizo ya muda mrefu
ikitafsiriwa pengine ndio mwanzo wa utekelezaji wa ripoti hiyo.