Arusha.
Serikali inakusudia kupunguza au kuondoa kabisa kodi katika ving’amuzi
ili kuwezesha Watanzania wengi kumudu kununua vifaa hivyo na kupata
huduma ya matangazo ya runinga.
Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema jana kuwa
kwa sababu Serikali inatekeleza makubaliano ya kimataifa ya kuhamia
mfumo wa dijitali kutoka analojia, ni vyema kila Mtanzania akawa na
uhakika wa kupata huduma ya matangazo ya runinga na hilo haliwezi
kufanikiwa iwapo bei ya ving’amuzi itaendelea kuwa juu.
Akizungumza
kwenye mkutano wa 21 wa Umoja wa Taasisi za Utangazaji Kusini mwa Afrika
(Saba), Makamba alisema hivi sasa wizara yake inawasiliana na Wizara ya
Fedha pamoja na wadau wengine kuangalia njia bora na sahihi ya
kufanikisha lengo hilo.
“Tayari
serikali imepunguza viwango vya kodi kwenye ving’amuzi ili kuwapa nafuu
wananchi, lakini tunafikiria kuipunguza zaidi au kuondoa kabisa kodi ili
kuwezesha Watanzania wote wenye seti za televisheni kupata matangazo ya
runinga,” alisema Makamba.
Akizungumza
katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania,
Profesa John Mkoma alisema Tanzania inajivunia kufanikiwa kutekeleza
malengo ya kimataifa ya kuhamia mfumo wa dijitali kutoka analojia
kulinganisha na nchi zingine za SADC.
Alisema
matumizi ya king’amuzi imerahisisha gharama za matangazo ambapo hivi
sasa mtu anaweza kurekodi kipindi na kukipeleka kwenye kituo cha Tv au
redio kwa ajili ya kurushwa hewani.
Profesa Mkoma
alisema matumizi ya dijitali pia yameboresha usikivu wa sauti na
muonekano wa picha kwenye vituo vya televisheni nchini.
Tanzania
ilianza kuingia kwenye mfumo wa dijitali kwa kuzima mitambo ya analojia
kuanzia mwishoni mwa mwaka jana kwa kuanzia na mkoa wa Dar es Salaam
mpango ulioendelea kwa mikoa mingine ya Tanzania.
Tayari baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki yameanza kufuata hatua hiyo ya Tanzania.