Tukio hilo la aibu lilijiri Jumatatu iliyopita saa 5:10 asubuhi kwenye Mtaa wa Uhindini mjini Iringa jirani kabisa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kanisa Kuu.
Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya mashuhuda waliliambia gazeti hili kwamba, siku ya tukio, mwanamke huyo akiwa na wenzake watano walifika katika duka hilo la Elizabeth Mlowe kama wateja wa jumla wa nguo.
“Walimkuta binti muuzaji, wakaanza kumsumbua kwa kuagiza nguo bila mpangilio, yule anaagiza aina ile huku mwingine akiomba kusogezewa vitenge na kanga. Hali hiyo ilimchanganya muuzaji na kujikuta akiibiwa kirahisi na Angel,” alisema shuhuda mmoja.
Akihojiwa na paparazi wetu, mwanamke huyo mwenyeji wa Mbeya aliyeolewa Iringa alisema kuwa alijiunga na mtandao wa wizi kwa kuzunguka madukani siku mbili zilizopita (Jumamosi).
Alisema kuwa mtandao huo unajulikana kwa jina la Zubaa Tutajirike (Zutu), upo Ipogolo kwa sasa lakini ulianzishwa jijini Mbeya ila baada ya kugundulika mbinu yao walihamia Iringa na kuendelea na wizi huo.
“Kwa kweli najuta sana, ni mara yangu ya kwanza kuingia katika kazi hii hapa Iringa, wenzangu ambao wamenikimbia wao ni wenyeji. Mume wangu alinikataza kutembea nao, ila leo nimemtoroka,” alisema kisha kupelekwa polisi mjini hapa.