Kamati ndogo ya Maadili ya CCM imeendelea kuwahoji wanachama wake walioonyesha nia ya kuwania urais, jana ilikuwa zamu ya mawaziri watatu.
Waliotarajiwa kuhojiwa jana ni Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira na Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.
Makamba alikuwa wa kwanza kufika mbele ya kamati hiyo jana asubuhi, huku Wassira akifuatia. Hata hivyo, Membe hakuonekana.
Makamba alikuwa wa kwanza kufika mbele ya kamati hiyo jana asubuhi, huku Wassira akifuatia. Hata hivyo, Membe hakuonekana.
Hata hivyo, kanuni za uongozi wa maadili za CCM
kifungu cha 7 (i) kinaeleza kuwa wanachama wenye nia ya kugombea nafasi
za uongozi katika muhula unaofuata, yaani ubunge, uwakilishi, udiwani na
nafasi nyingine katika chama wanaweza kutangaza nia zao, lakini
hawaruhusiwi kufanya kampeni kabla ya muda uliowekwa rasmi, muda wa
kampeni unaanza baada ya majina ya wagombea kuteuliwa na kikao
kinachohusika.
Makamba
Baada ya kuhojiwa Makamba, alisema siyo vibaya kwa
wanaotaka kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kutangaza
nia mapema, kwa sababu inawapa nafasi wananchi kuwapima.
Mbali na hilo Makamba alisema siyo dhambi kwa mtu
kuonyesha nia, bali ni dhambi kwa mtu kutoa fedha kwa nia ya kutaka
uongozi na kuvitaka vyombo vya dola kuchukua hatua za kisheria kwa watu
wa aina hiyo.
Kikao hicho kinachoongozwa na Makamu Mwenyekiti
Bara, Philip Mangula, juzi kiliwahoji mawaziri wakuu wa zamani Edward
Lowassa na Fredrick Sumaye pamoja na Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja, ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
“Ipo faida ya kuwajua mapema wanaotaka uongozi
kuliko kuwajua mwishoni, kwa sababu mnapata faida ya kuwachambua na
kuwauliza maswali, mbaya ni mtu kutoa pesa ama kutumia pesa.
“Hata katika maoni yangu na ushauri (ndani ya
kikao hicho cha maadili), nimesema kwamba hilo ndilo kubwa na la msingi,
kwa sababu linawaweka pembeni watu wenye vipaji vya uongozi kama huna
fedha basi huwezi kuwa kiongozi,” alisema Makamba.
Alisisitiza matumizi ya fedha katika kutafuta
uongozi yanakatazwa kwa mujibu wa kanuni za chama chao na sheria za nchi
na kwamba ushahidi unapopatikana chama kifanye kazi yake na Serikali
ichukue hatua dhidi yao.
Makamba alisema ipo sheria ya Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ambazo
zote zinakataza matumizi ya fedha.
“Kwa hiyo hawa wanaotajwa wanatumia fedha vilevile vyombo vya dola viwachukulie hatua, siyo tu kwenye chama,” alisema Makamba.
Makamba alisema kuwa mazungumzo yao ndani ya kikao hicho
yalikwenda vizuri, akidai yeye hakuitwa kwa ajili ya kugawa fedha kwa
wananchi na wala hakukuwa na shitaka lolote, isipokuwa ilikuwa ni kutoa
ushauri na kukumbushana kuhusiana na misingi muhimu ya chama chao ya
namna ya kupata uongozi.
“Kwa hiyo nilipata fursa nzuri ya mimi kutoa
ushauri wangu kuhusiana na namna ambavyo tunaweza kuyafanya mambo haya
vizuri zaidi, na namna ambayo tunaweza kutafuta uongozi kwa namna nzuri
zaidi badala ya kukigawa,”alisema.
Makamba alisema kuwa mazungumzo yao yalikuwa
mazuri sana na kwamba hakukuwa na jambo baya, wala hakuwa ameshitakiwa
bali walikuwa katika majadiliano ya kawaida ya ndani ya chama na kuwa
aliitwa kutokana na kutajwatajwa na wanachama.
Wassira
Kwa upande wake Wassira alisema hana mpango wa kutangaza kugombea urais leo wala kesho, lakini muda ukifika ataamua.
Alisema: “Kutamani nafasi ya urais siyo dhambi.”
Wassira alisema yeye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hawezi kutoboa mtumbwi ndani ya chama, halafu waangamie wote.
Alisema hajafanya vurugu zozote ndania ya chama na
kwamba katika kikao cha jana aliitwa kwa ajili ya kujitathimini na
kuangalia mustakbali wa chama katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Ripoti ya kamati hiyo ya maadili ya chama huenda
ikawasilishwa kwenye mkutano Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC),
unaotarajiwa kufanyika leo mjini Dodoma.
Akizungumzia suala hilo mwishoni mwa wiki
iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Philip Mangula
alisema mwanachama yeyote wa chama hicho hatakiwi kutoa michango,
misaada, zawadi kwa mtu au katika shughuli yoyote bila kupata ridhaa ya
uongozi.
“Kufanya jambo hilo ni kwenda kinyume na kanuni za
chama. Ndani ya chama kila ngazi ina Kamati ya Maadili, wote ambao
wameanza kwenda kinyume na kanuni za chama watahojiwa katika kamati
hizo,” alisema Mangula na kuongeza:
“Hairuhusiwi kuwasafirisha wajumbe, kuwapa malazi,
chakula, vinywaji na ukifanya hivyo utakuwa unakwenda kinyume na
utaratibu uliowekwa na Kamati ya Sheria, Katiba na Kampeni.”
Akihutubia kilele cha maadhimisho ya miaka 37 tangu kuzaliwa kwa
chama hicho, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete aliziagiza
Kamati za Maadili na Usalama, kuwachukulia hatua stahiki viongozi na
wanachama wake wanaomwaga fedha ili kupata uongozi.
Kadhalika, Rais Kikwete alipozungumza na wajumbe
wa Halmashauri ya CCM ya Mkoa wa Mbeya, alisema kuanza kwa kampeni kabla
ya wakati wake ni moja ya mambo yanayosikitisha na kwamba suala hilo
limekabidhiwa kwa Mangula kwa hatua zaidi za kinidhamu.
>>Gazeti la Mwananchi.
>>Gazeti la Mwananchi.