Wananchi
wa Kenya wameshangazwa na taarifa ya mwanamume mmoja aliyezinduka akiwa
katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali moja mjini Naivasha
umbali wa kilomita tisini kutoka mji mkuu Nairobi.
Mwanamume
huyo Paul Mburu mwenye umri wa miaka 24, alipelekwa hospitalini kwa
matibabu baada ya kunywa sumu kwa lengo la kujitoa uhai,kutokana na
ugomvi wa kinyumbani na babake ingawa alisemekana kufariki Jumatano
usiku wakati akipokea matibabu.
Wafanyakazi
wa hospitali hiyo walipigwa na butwaa na hata kutoroka walipoona mwili
wa mtu waliyedhani ni maiti ukisonga na kuonyesha dalili za kuwa hai
katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Afisa
mkuu wa matibabu katika hospitali hiyo ya wilaya, Dokta Joseph Mburu,
alisema kuwa dawa iliyotumiwa kumtibu Mburu hufanya moyo kupiga polepole
hali ambayo huenda ilimfanya muuguzi kudhani kuwa mgonjwa alikua
amefariki.
Mwanamume
huyo alisikika akimtaka mmoja wa wafanyakazi katika chumba cha
kuhifadhia maiti kumsaidia kwani alikuwa anahisi baridi kali na hapo
ndipo mmoja wa wafanyakazi alipotimua mbio kwa hofu.
Nusura Mburu awekwe kwenye jokovu la kuhifadhia maiti.
Jamaa
za mwanamume huyo akiwemo babake walikuwa wametembelea chumba cha maiti
siku ya Alhamisi ili kujiandaa kwa mazishi , lakini baadaye mchana
walifahamishwa kuwa Mburu alikuwa hai.
CHANZO; BBC