Katika
ajali ya kwanza, watu sita walifariki baada ya boti ya Kilimanjaro II
ilipokumbwa na dhuruba kali katika mkondo wa Nungwi, Zanzibar wakati
ikitokea Pemba kwenda kisiwani Unguja jana asubuhi.
Mkuu
wa Wilaya ya Kaskazini A, Riziki Juma, alisema jana jioni kuwa maiti
sita zilipatikana na kwamba abiria watatu waliokolewa wakiwa hai huku
uokoaji ukiendelea.
Hata
hivyo, wakati mkuu huyo wa wilaya akisema hayo, Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Kaskazini Unguja, Khalfan Mohamed Mshangi, alisema baadaye kuwa
zimepatikana maiti tano na tatu zimetambuliwa.
Aliwataja
waliofariki kuwa ni Akram Khamis issa (11), mkazi wa Mwanakwerekwe;
Masoud Hamad Abdallah (30), mkazi wa Wete na Nashra Khamis (9), mkazi wa
Mombasa, Zanzibar.
Aliongeza kuwa boti hiyo ilikuwa na abiria 396 wakiwamo watoto 60 na kwamba abiria ambao hawajapatikana ni 18.
Awali,
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Yusuph
Ilembo, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa kazi ya
kuwatafuta watu wanaohofiwa kupotea imeanza kufanywa na mabaharia kwa
kushirikiana na wananchi.
Alisema
boti hiyo ilipofika katika mkondo wa Nungwi ilipigwa na wimbi moja
kubwa na injini kuzimika na watu waliokuwa wamekaa juu wakiwamo watoto
waliteleza na kuhofiwa kutumbukia ndani ya bahari.
Alisema
kuwa boti hiyo baada ya injini zake kuzimika ilibakia ikielea baharini
na kwamba Nahodha wake alifanikiwa kuziwasha tena na kuendelea na safari
na abiria waliobakia walifika salama.
Mkurugenzi
wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Abdi Omar Maalim,
alisema wazamiaji waliondoka jana mchana kuungana na baadhi ya wananchi
huko Nungwi kufanya kazi ya kutafuta watu wanaohofia kupotea baada ya
ajali hiyo.
Hata
hivyo, alisema ZMA itatoa taarifa baada ya kukamilika uhakiki wa majina
ya abiria kwa meli zote zilizosafiri jana kutoka kisiwani Pemba pamoja
na wazamiaji kufika katika eneo la tukio na kufanya kazi ya kutafuta
watu hao.
MASHUHUDA WANENA
Baadhi
ya mashuhuda waliozungumzia tukio hilo walisema mkasa huo ulitokea sasa
2:30 asubuhi wakati boti hiyo ilipofika eneo la Nungwi na kupigwa wimbi
kali na kuelemea upande mmoja.
Suleiman
Muhammed Said, abiria katika boti hiyo, alisema baada ya boti hiyo
kuelemea upande mmoja, baadhi ya watu walidondoka baharini pamoja na
mizigo na kwamba boti iliendelea na safari baada ya kukaa sawa.
Alisema
boti hiyo iliondoka Pemba majira ya saa 2:00 asubuhi na kwa mujibu wa
ratiba, boti ilitarajiwa kufika Unguja saa 4:00 asubuhi, lakini kutokana
na hitilafu hiyo, ilifika saa 6:00 mchana.
Alisema
boti ilipoondoka Pemba, hali ya bahari haikuwa nzuri na ilipofika
Nungwi hali ya bahari ilizidi kuchafuka na boti kuyumba.
Alisema hadi boti inafika bandarini, ndugu zake wawili hawakuonekana pamoja na mizigo waliyokuwa nayo katika boti hiyo.
“Nilikuwa
na ndugu zangu wawili na mizigo, baada ya meli kutaka kuzama mizigo na
baadhi ya watu walidondokea baharini, lakini meli ilipoibuka iliendelea
na safari bila ya kuwatafuta,” alisema Suleiman huku akitokwa machozi.
Baadhi ya watu walifika bandarini Malindi waliangua vilio na sura zao kujaa na huzuni kutokana na kutowaona ndugu na jamaa zao.
Abdallah
Mohammed Abdallah, aliyefika bandarini kumtafuta mtoto wake ambaye bado
hakuwa na taarifa zake, alisema alipokea simu ya mtoto wake aliyekuwamo
katika boti saa 2:30 asubuhi kuwa boti inazama.
“Nilipokea
simu ya mtoto wangu, alikuwa akilia na kuniambia baba baba tunakufa,
meli huku inazama, baada ya hapo simu yake ikawa haipatikani” alisema
Abdallah.
Aidha
alisema alifika bandarini kupata taarifa sahihi, lakini hakupewa jibu
linaloridhisha kutokana na boti kufika bila kumuona mtoto wake. Mmoja wa
abiria aliyekuwa anasafiri na boti, Salama Husseni alisema:
“Tulianza
safari vizuri ila tulipofika Nungwi mawimbi yalikuwa makali sana, boti
yetu ilizidiwa ndipo hali ya wasiwasi ikatujaa abiria wote ila
tunamshukuru Mungu hali ilikaa sawa baada ya muda na amani ikarejea.”
AZAM MARINE KIMYA
Hata
hivyo, waandishi wa habari walifika katika ofisi za Kampuni ya Azam
Marine inayomiliki boti hiyo ili kupata taarifa sahihi, uongozi ulikataa
kuzungumza badala yake ukawafukuza.
Wanne wafa Rufiji
Wakati
huo huo, watu wanne wamekufa maji na wengine 12 kuokolewa baada ya boti
ya Mv Nyaulele waliyokuwa wakisafiria kutoka wilayani Rufiji kwenda
Mafia mkoani Pwani kupinduka na kuzama majini katika Bahari ya Hindi
usiku wa manane kuamkia jana.
Kamanda
wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei, alidhibitisha tukio hilo na
kusema boti hiyo ilikuwa ikitoka Rufiji kwenda Mafia juzi saa 11:00
jioni na ilipofika katikati ya safari ilikumbana na dhoruba kisha
kupinduka na kuzama baharini.
Matei
alisema kwa kujibu wa taarifa zilizopo polisi, boti hiyo ilikuwa na
abiria 16 na mizigo kadhaa midogo midogo ya kawaida ya abiria.
Aliwataja
abiria waliofariki kuwa ni Swaumu Muhidin, Tano Shaban ambaye
amegundulika kuwa ni mwalimu wa shule moja wapo ya msingi Rufiji, Hadija
Ntayala na mtoto mdogo mwenye umri kati ya miezi minne na sita, Najma
Yusufu.
Imeandikwa na Rahma Suleiman, Beatrice Shayo, Zanzibar; Kamili Mmbando, Dar na Julieta Samson, Pwani.
CHANZO: NIPASHE