Askari mwenye cheo cha sajini katika Gereza la Ruanda na polisi mwenye cheo cha konstebo katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Mbeya, wamekamatwa kwa tuhuma za kushirikiana na watu wengine watatu, kwa kuteka gari na kupora fedha na mali katika eneo la Mlima wa Kawetere, Barabara ya Mbeya-Chunya, juzi jioni.
Inadaiwa kuwa katika tukio hilo, watuhumiwa walipora Sh3.5 milioni na mabegi yaliyokuwa na vitu mbalimbali.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kushiriki katika kupora
mali ya mfanyabiashara Sheedhar Paupeleti (38) baada ya kuteka gari
alilokuwa akisafiria akiwa na watu wengine wawili.
Habari zilisema katika tukio hilo, dereva wa gari hilo Ezekiah Matatira, alifungwa pingu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi,
alisema majambazi hayo yalikamatwa baada ya polisi kwenda katika eneo
la tukio, kutokana na taarifa zilizotolewa na wananchi kwa njia ya simu.
Kamanda Msangi alisema tukio hilo lilitokea saa
11.30 jioni na kwamba majambazi hayo walikuwa yanatumia magari mawili.
Alisema katika eneo hilo, gari moja lilizuia njia huku majambazi
wakidai kuwa wamepata pancha na kwamba lilipofika gari la
wafanyabiashara lilishindwa kupita na hivyo kulazimika kusimama.
“Waliposimama, majambazi walimkamata dereva na
kumfunga pingu wakidai wao ni polisi na walikuwa katika eneo hilo
kuwasubiri watu hao ambao wanatafutwa’,’ alisema.
Alisema majambazi hao walimfungua pingu dereva na
kuondoka na mfanyabiashara pamoja na funguo za gari lakini baadaye
walimtupa chini mfanyabiashara huyo.
Kamanda huyo alisema polisi walipopata taarifa
walikwenda katika eneo la tukio na kuweka kizuizi kimoja na baadaye
kurudi Mbeya na kwamba kikosi cha kwanza kilipishana na majambazi
waliokuwa wakirejea Mbeya, lakini kwa bahati nzuri kikosi cha pili
kilikuwa karibu na kizuizi ambapo majambazi walipofika walikamatwa na
askari wa pande zote.