Ametoa msimamo huo jana wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Malumba Jimbo la Kasulu Mjini kwenye mkutano wa hadhara.
“Kama ni kutishiwa maisha mimi si mara kwa kwanza, lakini hata ikitokea nimepigwa risasi Mwenyezi Mungu atakuwa ameridhia, binadamu hawezi kufa kama Mungu hajaruhusu, sasa unaogopa nini?,” Alisema na kuhoji Dk. Slaa.
Dk. Slaa ambaye alikuwa akijibu watu walioandamana juzi Kigoma Mjini na kumtisha asikanyage Kigoma, alisema hawezi kuacha kutetea wanyonge eti sababu kuna watu wanataka asikanyage Kigoma.
“Hao wanaofanya hivyo hawawatakii mema Watanzania wanyonge, naomba wajue Dk. Slaa haogopi, mlinzi wangu siyo hawa wenye bunduki mlinzi wangu ni Mungu ambaye yupo juu,” alisema.
Dk. Slaa alisema wanaodai asikanyage Kigoma mjini watambue nchi hii hakuna mwenye hakimiliki bali kila mtu ana haki ya kufika mahali popote.
Alisema toka mwaka 2011, amekuwa akitembea vijijini, wilaya, majimbo na mikoa na kwamba tatizo watu wanahisi amekwenda Kigoma kwa sababu ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ambaye mwezi uliopita alivuliwa nafasi ya Unaibu Katibu Mkuu wa Chadema kwa tuhuma za kukisaliti Chama.
Kwa upande wake, Ofisa wa Chadema wa Sera na Utafiti, Mwita Waitara, alisema Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kigoma, amtafute na kumkamata mtu aliyetangaza katika maandamano ya jana Kigoma mjini kwamba atamuua Dk. Slaa akikanyaga Kigoma mjini “OCD wa Kigoma asiseme viongozi wa Chadema makao makuu badala yake amtafute aliyetishia kumuua Dk. Slaa hadharani,” alisema.
Alisema Chadema inafahamu njama zote hizo zinafanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwamba vitisho hivyo haviwezi kumzuia Dk. Slaa kwenda Kigoma Mjini.
Dk. Slaa leo ataendelea na ziara yake katika Mkoa wa Kigoma kwa kutembelea Jimbo la Buhigwe, kesho atatembelea Jimbo la Kigoma Kaskazini na kesho kutwa Kigoma Mjini.
Credit: -NIPASHE.