TATIZO la ujangili ambalo limekuwa sugu nchini kwa muda mrefu sasa linaanza kupata dawa, baada ya Serikali kutangaza ‘Operesheni Tokomeza’ itakayotumia mbinu za kijeshi.
Katika operesheni hiyo inayotekelezwa kwa awamu, ndege za kivita zisizokuwa na marubani (Drones), zitatumika katika kufanikisha vita hiyo, iliyolenga kunusuru wimbi la wanyama kuuawa.
Akizungumza na RAI katika mahojiano maalumu jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alisema operesheni hiyo itatokomeza ujangili hususan wa tembo ambao umekuwa ukishika kasi kutokana na ukubwa wa soko.
Balozi Kagasheki alisema operesheni hiyo imepata nguvu, baada ya silaha za kupambana na ujangili zilizokuwa zimezuiliwa bandarini kutolewa kwa agizo la Rais Jakaya Kikwete.
Kagasheki aliendelea kueleza mbali ya askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), operesheni hiyo pia itahusisha askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), katika kukabiliana na mtandao huo.
“Ninachotaka kusema katika hii vita, Serikali haitashindwa na kazi ambayo tumekuwa tukiifanya, kila mmoja wetu anajua nini kinachoendelea, nawaomba wananchi waendelee kutupa ushirikiano,” alisema.
Kwa mujibu wa Kagasheki awali oparesheni hiyo ilikuwa ni kukusanya taarifa mbalimbali, ambapo wizara yake imebaini kuwa baadhi ya vigogo wa Serikali wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo.
“Ninawaambia katika hili yeyote atakayekutwa hatasalimika, kwani siwezi kukaa kimya huku wanyama ambao ndiyo urithi wa Taifa wakiendelea kumalizwa na majangili ambao wana nia ovu na Tanzania yetu,” alisema Balozi Kagasheki.
Kuhusu ndege za kivita, Balozi Kagasheki alisema hiyo ni mbinu nyingine katika operesheni hiyo ambapo ndege maalumu ambazo hazina rubani zitakuwa zikizunguka katika maeneo yote ya hifadhi za Taifa na mapori ya akiba.
“Hizi ndege tutazitumia kwa lengo la kuzidisha mapambano na maharamia hawa ambao hivi sasa tunawaambia popote walipo wajue sasa Serikali ipo kazini hasa katika kulinda rasilimali za nchi,” alisema.
Akizungumzia hatua ya Rais Kikwete kuagiza kutolewa kwa silaha zilizokuwa zimekwama bandarini, Balozi Kagasheki alimpongeza rais kwa hatua hiyo ambayo alisema inalenga kujali maslahi ya taifa zaidi.
Hatua hiyo imekuja miezi kadhaa baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kudai kodi ya uingizaji wa silaha hizo zilizonunuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kuimarisha vita hiyo.
Kagasheki, alisema hatua ya TRA hapo awali haikuwa sahihi kwani silaha hizo hazikuingizwa kwa ajili ya kumlinda yeye na familia yake, isipokuwa ni kwa ajili ya kulinda rasilimali za nchi.
“Uamuzi wa TRA ulimshangaza Rais Kikwete, baada ya kupata maelezo ya kina kuhusu hali hii alitoa agizo ili sihala hizo zitolewe bandarini mara moja.
“Ni vema jamii ikatambua kuwa tunachofanya ni kuimarisha ulinzi dhidi ya rasilimali za nchi yetu ambayo si mali ya mtu mmoja wala mali ya Kagasheki.
“Katika hili ni lazima kila mmoja atambue kuwa ana jukumu la kutoa taarifa juu ya ujangili huu unaofanywa dhidi ya tembo wetu waliopo katika hifadhi za Taifa pamoja na mapori yote ya akiba.
Waziri Kagasheki pia alilaumu hatua ya Ofisa Upelelezi Mkoa wa Arusha (RCO), Duwan Nyanda, kwa kuruhusu kuachiwa kinyume cha sheria majangili wawili kutoka nchini Saud Arabia.
“RCO huyo wa Arusha akaona haitoshi akaamuru watu hawa ambao walikuwa wamefanya vitendo vya ujangili watolewe na wakabidhiwe na hati zao za kusafiria, kwa hili hapana na wala siwezi kukubaliana nalo hata kidogo.
“Nitafanya mawasiliano na waziri mwenye dhamana ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ili kumweleza kwa kina jambo hili kuhusu kitendo hiki ambacho si cha kuungwa mkono hata kidogo kutokana na vita hii ya ujangili,” alisema.
Kwa mujibu wa takwimu kumekuwa na ongezeko la biashara ya meno ya tembo, ambapo kati ya mwaka 2008 hadi 2009 bei ya Kilo moja ya meno ya tembo ilikuwa ikiuzwa dola 10 na sasa imepanda hadi kufikia Dola za Marekani 1500 hadi 2000.
Kwa mujibu wa Kagasheki, soko kubwa la biashara hiyo hivi sasa lipo katika nchi za China, Vetnam na Thailand.
Aprili 29, mwaka huu katika Mkutano wa Bunge la Bajeti Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli alitaka TRA iachie silaha hizo ili kurahisisha vita dhidi ya ujangili.
“Kamati inaona kwamba japokuwa Wizara ya Maliasili na Utalii, imeonesha nia ya wazi ya kukabiliana na ujangili, na kununua silaha za kufanikisha azma hiyo, Serikali hiyo kupitia TRA imezuia silaha hizo bandarini ikidai kodi,” alisema.
Alisema kuzuiwa kwa silaha hizo za kisasa ni jambo la kushangaza kwani pamoja na wanyamapori ambao ni mali ya Serikali inayoiingizia mapato, bado taasisi kama TRA haioni jitihada za mkono mwingine wa Serikali wa kuokoa rasilimali ya taifa.
Kwa mujibu wa Lembeli tembo wasiopungua 30 huuawa kila siku, huku takwimu za Taasisi ya Utafiti wa Wanyama (TAWIRI ), zikibainisha wazi tishio kubwa na tembo kumalizika.
-Mtanzania