Ukosefu wa
fedha za kununulia dawa za kulevya, umewafanya walevi, ‘mateja,’ kubuni
njia ya hatari, kwa kunyonya damu yenye kilevi toka kwa aliyetumia na
kujidunga.
‘Mateja’
wamefikia hatua ya kuchangishana fedha na kununua kete moja ya dawa aina
ya heroin yenye ubora, mmoja wao hutumia na akilewa wengine hupata
ulevi huo kwa kumnyonya damu kwa kutumia sindano ya hospitali na
kujidunga.
Reuben (si
jina lake halisi) aliyenyong’onyea mwili mwenye midomo yenye rangi
nyeusi anasema aliwahi kubadilishana damu na watu zaidi ya 20, damu
anayoeleza kuwa alikuwa akibadilishana vijiweni, kwenye kumbi za starehe
na maskani bila kuzingatia taratibu wala athari zake.
“Nimewahi
kununua damu kwa watu waliotumia heroin halisi, pia ‘maskani’ (kijiweni)
tulikuwa tukichanga fedha na kununua heroin halisi kisha mmoja anatumia
na baadaye tulichukua damu kwake kwa njia ya bomba la sindano,” anasema
Reuben akiwa kwenye foleni ya matibabu ya kliniki ya ‘Methadone’
iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Ukishatumia
sana ile ya buku baadaye unakuwa huridhiki sana hata hivyo itakulazimu
utumie zaidi ya moja kwa siku, kwani ile huchakachuliwa sana kwa
kuchanganywa na vidonge aina ya ‘Valium’ ambavyo hutumiwa kama dawa za
usingizi,” alisema Reuben. Heroin ambayo huuzwa kwa gharama ya kuanzia
sh 1,000 kwa kete hasa ile ‘iliyochakachuliwa’, asilimia kubwa wamekuwa
wakishindwa kununua heroin halisi ambayo huuzwa kwa bei ya juu, hivyo
huishia kuomba au kununua damu kwa aliyetumia aina hiyo ili kupata
ulevi.
Akizungumza
na gazeti hili, Mtaalamu wa Afya ya Akili (psychiatric) na Mkuu wa
Kliniki ya Matibabu ya Dawa za Kulevya ‘Methadone’ kutoka Hospitali ya
Taifa Muhimbili, Dk Frank Masao, anasema tatizo hilo wameligundua hivi
sasa baada ya kuzungumza na waathirika wa dawa hizo.
“Baada ya
kuzungumza na waathirika hawa tumegundua kuwa wamekuwa na mazoea ya
kubadilishana damu, pindi mmoja anaposhindwa kununua heroin, wao
hawazingatii makundi ya damu wanatoleana tu, vitendo hivi vimekuwa
vikifanywa sana kwa mazoea bila kujali athari za mbeleni,” alisema Dk
Masao.
Hata
hivyo, Reuben anasema alianza kubadilishana damu mwaka 2009, wakati huo
walikuwa wakinunua Kinondoni kwa Manyanya, jijini Dar es Salaam.
“Maskani
ambayo nilikuwa nanunua unga ni Kinondoni kwa Manyanya, pale mpaka mara
ya mwisho naachana na dawa za kulevya mwaka mmoja uliopita, nilikuwa
nanunua hapo. Japokuwa nikisafiri nilikuwa natafuta hukohuko mkoani pia
zipo ilimradi upewe ramani na watu wanaojua soko lilipo,” alisema
Reuben.
Amina
anayeishi Temeke jijini Dar es Salaam, naye ni mmoja kati ya waathirika
wa zoezi la kubadilishana damu na hakumbuki idadi kamili ya watu
aliokuwa akibadilishana damu japokuwa anasema si wengi.
“Nilikuwa
natumia heroin nyeupe na ile ya brown miaka 14 iliyopita, wakati huo
nilikuwa nafanya shughuli za biashara, nilikuwa vizuri kifedha lakini
leo kama unavyoniona nimechoka,” anaanza kwa kusema mwanamke huyo
aliyejichora ‘tatoo’ nyingi mwilini mwake.
“Nilifika
hapa Muhimbili baada ya kuzidiwa na dawa hizi na uchumi wangu uliyumba,
ilifikia hatua nilianza kubadilishana damu na wengine na hata niliiba na
kupora ili tu nipate ‘unga’ kwani nikienda kuomba kazi walinikatalia na
kuniita teja, sikuwa na sehemu ya kuniongezea kipato. Nawashukuru Asasi
ya Blucose ambao walinileta hapa,” anasema Amina na kuwataka wanawake
kutojiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya.
Hata
hivyo, Dk Masao amefafanua kuwa matumizi ya dawa za kulevya humfanya mtu
yoyote aliyeambukizwa Virusi vya Ukimwi CD4 zake kushuka haraka, huku
akipoteza uwezo wake kiutendaji na hata akili yake kuathirika kwa
kiwango kikubwa.
Alisema
maambukizi ya virusi vya Ukimwi yapo juu sana kwa waathirika wa dawa za
heroin waliofika katika kituo hicho kwa ajili ya matibabu ya methadone,
lakini hata hivyo wapo walioambukizwa homa ya ini, hao hugundulika baada
ya vipimo kwani mwathirika yeyote lazima afanyiwe vipimo vyote ili
kupatiwa matibabu kwa urahisi,
“Asilimia
32 ya wagonjwa wanaotibiwa katika kliniki hii wana maambukizi ya virusi
vya Ukimwi huku asilimia 60 wana maambukizi ya homa ya ini (hepatitis C)
na asilimia 31 wana maambukizi ya homa ya ini aina ya pili (hepatitis
B) huku asilimia 11 wakiwa na kifua kikuu,” anasema Masao huku
akifafanua kuwa watu zaidi ya 25,000 nchini Tanzania wanajidunga dawa
aina ya heroin huku 15,000 wakitokea jijini Dar es Salaam.
Dk Masao
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Afya ya Akili nchini, anasema
Hospitali ya Taifa Muhimbili inahudumia wagonjwa 640 huku 50 kati yao ni
wanawake na kufanya idadi yao kuwa asilimia saba.
Itaendelea Jumapili ijayo…..
“Kitengo
chetu kilianza kutoa huduma hii Februari 2011 na tulianza kupokea
wagonjwa wanne kwa siku na ilifikia hatua tulikuwa tukipokea hata 20
waliohitaji huduma kutoka kwetu na mpaka sasa tuna wagonjwa 640. Kati ya
hawa 18 tuliwaondoa kutokana na matatizo mbalimbali. Wapo waliokuwa
wakifika na silaha mbalimbali na hawa walikuwa tishio kwa kitengo hiki.”
Dk Masao
anasema licha ya kuondolewa katika kitengo hicho walio wengi wamekuwa
wakirudishwa tena; “Hata kama akifanya vurugu tutamwondoa lakini baadaye
lazima tumfuate na kama akikiri kosa na kuahidi kubadilika tunamrudisha
na anaendelea na dozi. Kila anayetibiwa hapa sharti la kwanza ni lazima
makazi yake halisi yajulikane hivyo inakuwa rahisi kumfuatilia mgonjwa
huyu iwapo atakatisha dozi ili kujua sababu ni nini.”
Akifafanua
kuhusu dawa inayotumika kuondoa sumu ya dawa za kulevya katika mwili wa
mwathirika, Dk Masau alisema methadone humwezesha mgonjwa kutosikia
hamu ya kutumia dawa hizo, sambamba na kumwondolea maumivu mwilini.
“Dawa hii
wanayopewa inawasaidia mwili kutokuwa na maumivu. Maana mtu anaposikia
maumivu hapo ndipo anapoanza kuhangaika kutafuta heroin ili ajidunge.
Lakini akipata methadone huwa salama na hawezi kupata tena hamu ila
masharti ya dawa hii ukitumia hupaswi kurudi tena na kuanza kujidunga,”
alisema Dk Masau na kuongeza; “Dawa hii yenye thamani ya dola 75,000
sawa na Sh124 milioni tumepewa na wafadhili kutoka Canada ambapo walitoa
kiasi cha kilogramu 50 ambazo huweza kutumika kwa kipindi cha miaka
miwili.”
Anafafanua
kuwa dozi hiyo hutolewa kila siku katika hospitali hiyo kwa kiasi cha
dozi ya mililita 1.5 kwa kila mwathirika kila siku huku wengine
wakitunzwa wodini kutokana na kuathirika kwa kiwango kikubwa, hata hivyo
aliweka wazi kuwa idadi kubwa wamekuwa wakishindwa kuhimili gharama za
usafiri kila siku.
Alisema Tanzania ni nchi ya kwanza katika nchi za Jangwa la Sahara kuwa na kitengo cha methadone.
“Tanzania
ni nchi ya kwanza katika nchi za Jangwa la Sahara kuanza kutoa matibabu
ya methadone, lakini pia tunafundisha nchi nyingi kutoa huduma hii
wakiwemo Nigeria, Msumbiji, Kenya, Uganda, Zambia na nchi nyinginezo
ambao hufika hapa Muhimbili kwa ajili ya kupata utaalamu huu,” alisema
Dk Masao.
Alisema utaalamu hasa kuhusu matumizi ya dawa hiyo sambamba na ujuzi wa kutoa matibabu hayo waliupata katika nchi ya Vietnam.
“Vietnam
ndipo hasa tulipopata ujuzi huu na huko tumekuwa tukiwapeleka wataalamu
wengi kujifunza. Moja kati ya changamoto zilizopo katika kitengo hiki ni
ukosefu wa watoa huduma, wengi hawapo radhi kujitolea katika kutoa
matibabu kwenye kitengo hiki. Hatuna wanasaikolojia wa kutosha, manesi
na madaktari”
Dk Masao
anasema kitengo hicho kimekuwa kikipokea pia wanandoa ambao wamekuwa
wakifika kwa pamoja kwa nia ya kupata huduma hiyo ili waachane na
matumizi ya dawa za kulevya.
“Tunapokea
hapa wanandoa wanaohitaji kuacha na walio wengi huwa waaminifu. Mpaka
sasa watu waliopona na kuacha kabisa tunawatumia katika kuhamasisha
wengine kuachana na matumizi ya dawa hizi.”
Aliitaja mikoa inayoongoza kwa waathirika wa dawa za kulevya kuwa ni Mbeya, Dodoma, Arusha , Tanga na Morogoro.