Dar es Salaam.
Seleman Rajab (17) anaugua ugonjwa ambao mpaka sasa wazazi wake wanasema
hawaufahamu. Licha ya kuwa na maumivu na uvimbe kuongezeka, mara ya
mwisho kupelekwa hospitali ilikuwa mwaka 2010, zaidi amekuwa akipewa
vidonge vya kutuliza maumivu.
Mama yake anayemlea Khadija Ahmed anasimulia kuwa, alielezwa kwamba Rajab alizaliwa akiwa na uvimbe kwenye unyayo.
Akiwa na umri wa miaka miwili hakuweza kutembea, akapelekwa hospitali
kufanyishwa mazoezi ya viungo na alipotimiza umri wa miaka sita, uvimbe
huo ukaanza kututumka kidogo kidogo.
“Alikuwa akiishi na mama yake ambaye alifariki Agosti mwaka jana,
hakutuambia hospitalini aliambiwa mtoto anaugua nini, lakini mara ya
mwisho kumpeleka hospitali ya CCBRT ilikuwa mwaka 2010 na kwa sababu
ilipendekezwa akatwe mguu, mama yake hakumrejesha tena,” mama Seleman
Anasema tangu waanze kuishi na mtoto huyo, mwaka jana hawajampeleka
hospitali yoyote kutokana na kukosa fedha ya kugharamia vitu mbalimbali
ikiwamo kukodi gari la kumpeleka hospitali na kumrejesha nyumbani.
Baba Selemani anafanya kazi ya kutunza bustani kwenye kiwanda cha Kamal
Steel, kinachotengeneza nondo na mama yake ni mama wa nyumbani ambapo
familia yake ni yenye watoto watano, wa kike mmoja wa kiume. Wadogo zake
wanasoma shule.
Selemani anasema, “Naomba nisaidiwe angalau na mimi niwe na uwezo wa
kutoka nje au kujihudumia mwenyewe badala ya sasa ambapo ninaogeshwa,
nikitaka kutoka nje mpaka baba na mama waniweke kwenye blanketi,
wanibebe mmoja huku mwingine kule, inaniuma sana.”
Anasema huwa anapata maumivu mara moja, kwamba huhisi viungo hususan
mguu uliovimba kama vile ndani yake kuna moto unawaka na kwamba
inapotokea hali hiyo, hupewa vidonge vya kutuliza maumivu; mara nyingi
humsaidia kupunguza maumivu.
Tangu mwaka jana, mguu wa kushoto nao umeanza kuvimba. Hata sikio
linaonekana kuanza kuvimba. Pamoja na matatizo yote yanayomkabili tangu
utoto, Seleman anaweza kusoma na kuandika majina yake na ya wazazi wake.
Anasema alikuwa akifundishwa na marehemu mama yake, kwamba alinunua ubao
mdogo ambao alikuwa akiutumia kumfundishia kusoma na kuandika.
Hakuwahi kuingia darasani na anasema ikitokea Mungu akamponya, atasoma sana ili awe mwalimu au daktari.
Baba Seleman anasema katika familia yao hakuwahi kutokea mtu kuugua
ugonjwa wa aina hiyo, ila baba mzazi wa mama yake mguu wake mmoja una
ugonjwa wa tende, umevimba sana lakini anasema yeye hutembea na kufanya
shughuli zake kama kawaida.
Lakini ninapotazama sura ya Baba Selemani (Rajab) kwenye kidevu upande
wa kushoto ana uvimbe mkubwa kidogo, anasema umekuwapo kitambo sasa na
kwamba alienda hospitali ya Amana akaandikiwa dawa za kutumia na kwamba
huwa anazitumia ingawa haoni mabadiliko,“Hiki kipo siku nyingi tu, wala
hakiumi.”
Maisha ya Seleman
Baba yake anasema huwa anaoga mara moja kwa siku. Hii inatokana na
ukweli kwamba ni lazima amuogeshe mwenyewe (baba) na inatakiwa iwe usiku
kwa sababu kutokana na mazingira ya familia hiyo, ambayo inaishi katika
vyumba viwili yenye choo cha nje na cha shimo; anaogea nje- uwanjani.
“Umri wa miaka 17 siyo mdogo, ameishajitambua, hivyo siyo rahisi
tumuogeshee nje mchana, huwa tunasubiri giza liingie, tunamuweka kwenye
blanketi mimi nashika huku mama yake kule tunamtoa nje, tunatandika
turubai, namuogesha,” anaeleza baba Seleman
Anasema hata anapotaka kujisaidia, wanamtengea kifaa na kumsaidia
kuunyanyua mguu uliyojaa ili aweze kukaa vizuri kwenye chombo na
kujisaidia.
Hawezi kujihudumia kwa kitu chochote. Kuhusu kula inaelezwa na mama yake
kuwa anakula kila kitu isipokuwa viazi mviringo na uji wa ulezi;
vinamvuruga tumbo.
Wazazi hao wanaomba msaada ili mtoto huyu apelekwe hospitalini, afanyiwe
uchunguzi na ikiwezekana atibiwe, ili naye aishi kama watoto wengine.
Kwa atakayeguswa na mateso yake na kufikia uamuzi wa kumsaidia
awasiliane na gazeti hili, Mhariri wa Dawati la Ndani ya Habari (Dismas
Lyassa) kwa mpesa 0754498972 au tigo pesa 0712183282. Kutoa ni moyo na
huongeza baraka katika maisha, ni furaha ya Mungu kuona wanadamu
wanajaliana hasa wakati wa shida, ndivyo yanavyosema maandiko
matakatifu.
Je, ugonjwa huu hutokana na nini? Usikose toleo la jumatatu ili
kuufahamu kwa kina na kujua namna ya ili hata wewe usiupate, kwani
utafiti wa awali unaonyesha mtu yeyote anaweza kuupata.