MMHHH...!!! DAKTARI MWENYE MATATIZO YA AKILI ATIBU WATU NA KUFUNDISHA MASUALA YA TIBA...
Huwezi
kuamini lakini huu ndio ukweli, kwamba watu kadhaa wamekuwa
wakimiminika kupata msaada wa tiba, ushauri wa kitabibu na wengine
masomo ya udaktari kwa mtu ambaye imethibitika kwamba hivi sasa ana
matatizo ya akili.
Huyu si
mwingine bali ni Mark Paulo Kishiwa ambaye kitaaluma ni daktari,
aliyewahi kufanya kazi Hospitali za Kasulu, mkoani Kigoma na Bugando
mkoani Mwanza, lakini sasa mvua na jua humwishia akiwa maeneo ya
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Ukimwona
mara kadhaa utamkuta akiimba nyimbo zisizo rahisi kuzielewa kutokana na
hali anayonekana kuwa nayo ya matatizo ya akili, lakini anapokuwa sawa,
hugeuka kuwa msaada kwa wengi; madaktari wa MNH ambao huomba ushauri
kwake, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba Muhimbili (MUHAS) na
wagonjwa ambao hutaka ushauri pia.
Dk
Kishiwa anasema: “Naikumbuka Aprili 26, 1981, ilikuwa Jumatatu ya
Pasaka, ndipo nilianza kuugua. Nilijikuta nikifanya vitu visivyo vya
kawaida.
Nilimwaga
maji ovyo ndani, nilimwaga nguo na vitu mbalimbali, kila kitu kilikuwa
ovyo. Baada ya muda niligundua kufanya vitu siyo vya kawaida…Hivyo
ndivyo nilivyoanza kuchanganyikiwa na hali hii imenitokea mara kwa
mara.”
Aliongeza:
“Yaliponitokea hayo, nilikuwa nikifanya kazi mkoani Kigoma katika
hospitali iliyopo wilayani Kasulu (hakuitaja jina) ndipo kilikuwa kituo
changu cha kazi.”
Pamoja
na Dk Kishiwa kuwa na matatizo ya akili, imethibitika kuwa baadhi ya
madaktari wa MNH wamekuwa wakikimbilia kwake kupata ushauri, lakini
kubwa ni lile la kufundisha masomo ya ziada kwa baadhi ya wanafunzi
MUHAS.
Pia
amekuwa akifuatwa na watu wanaomfahamu hasa wanawake wakimwomba ushauri
hata kuwaandikia dawa kutokana na maradhi waliyonayo. Mwandishi wa
habari hii ni mmoja wa waliopata ushauri wa kitabibu kutoka kwa Dk
Kishiwa.
Tiba na ushauri
Uchunguzi
wa wiki kadhaa katika eneo la MNH, nyumbani kwake Chamazi na hata
katika familia yake, umethibitisha kwamba Dk Kishiwa licha ya kuwa
mgonjwa wa akili bado ni msaada mkubwa kwa watu wengi.
Gazeti
hili lilishuhudia daktari huyo akimwelekeza mmoja wa madaktari wa MNH
namna ya kumsaidia mgonjwa wake. Kwa mujibu wa mazungumzo yao, hali ya
mgonjwa husika ilimchanganya daktari huyo, hivyo kutaka kupata msaada
kwa Dk Kishiwa.
Uchunguzi
pia ulibaini kuwa wakati fulani, Dk Kishiwa anakuwa katika hali ya
kawaida na kuweza kutoa ushauri, hata kutibu kwa kuwaandikia dawa
wagonjwa akiwa eneo hilo la Muhimbili.
Jioni
moja gazeti hili lilishuhudia wanawake wawili waliobeba watoto mgongoni
wakiwa na Dk Kishiwa, aliyekuwa akiwaandikia kitu kwenye karatasi. Baada
ya tukio hilo mwandishi aliwauliza iwapo wanamfahamu, na walijibu;
“Tunamfahamu, ni daktari alikuwa akituandikia dawa.”
Hata
hivyo, uchunguzi ulibaini kuwa mambo yanapobadilika, Dk Kishiwa huwa
mkali asiyetaka kuwa karibu na mtu au kuzungumza naye, huku akifanya
vioja vinavyothibitisha hali yake ya matatizo ya akili. Hali hiyo
ilimlazimisha mwandishi kuendelea kumfuatilia kwa siku kadhaa katika
eneo hilo la MNH na kufanikiwa kuzungumza naye.
Kwa
mujibu wa watu wanaomfahamu hasa madereva teksi wa eneo hilo, walisema
Dk Kishiwa hushinda hapo na kwamba pamoja na kuwepo kwa wafanyabiasha na
madereva wengi, daktari huyo humsikiliza dereva mmoja anayepatana naye
na mara nyingi hutekeleza anayomweleza.
Kwa
msaada wa dereva huyo, Dk Kishiwa anaeleza historia ya maisha yake kuwa
alizaliwa Desemba 25, 1954, alipata elimu katika Shule ya Msingi Tumbi
mkoani Tabora hadi darasa la nane na kuendelea na masomo kupitia shule
kadhaa ikiwemo Sekondari ya Busonga na Sekondari ya St Mary’s ya
Tabora.kwamba katika elimu ya sekondari alipata daraja A kwa masomo yote
11.
“Sikuwahi
kufeli, nilipata daraja A katika masomo yote 11 niliyosoma yakiwemo
kemia, baolojia, hisabati na civics. Baada ya hapo nilijiunga na jeshi
kwa mujibu wa sheria kwa miezi sita katika kambi ya Mafinga,” anasema
Kishiwa bila kutaja miaka aliyosoma.
Anakumbuka
kuwa 1974 ndipo alijiunga na Chuo cha Tiba Muhimbili, ambapo alisoma
kwa miaka mitano na kumaliza 1979, bila kufeli somo hata moja na baada
ya hapo alipangwa kwenda Hospitali ya Bugando, Mwanza kikiwa ni kituo
chake cha kazi cha kwanza.
Anasema
alikaa Bugando kwa mwaka mmoja tu na mwaka uliofuata akapelekwa Wilaya
ya Kasulu, Kigoma kama Mganga Mfawidhi na huko ndipo lilipoanzia tatizo
alilonalo hadi sasa.
Kuugua akili
Anaeleza
kuwa tangu Aprili 26, 1981 alipopatwa na tatizo la akili, amekuwa
akipelekwa hospitali mara kadhaa na tatizo hilo kutulia, lakini bado
hali haikuwa nzuri ingawa bado aliendelea kufanya kazi.
Anasema kuugua kwake kunahusishwa na imani za kishirikina, jambo ambalo si kweli na hajui nani aliyezusha.
Dk
Kishiwa anasimulia kuwa baada hali yake kuwa nzuri hakuendelea kukaa
Kigoma bali alirudishwa Bugando, Mwanza na anadai kwamba kati ya 1986 na
1994 alifanya kazi Muhimbili, lakini alisimamishwa kwa sababu ambazo
hadi leo hazifahamu.
“Nililipwa Sh3.4 milioni ambazo nilizitumia kununua shamba eneo la Chamazi na kujenga nyumba ninayoishi sasa,” anabainisha.
Anaendelea
kueleza kuwa licha ya kufanya kazi Muhimbili, pia aliwahi kufanya
katika Hospitali ya Vikuruti na Chamazi wilayani Ilala, Mkoa wa Dar es
Salaam, ambapo alikuwa akilipwa posho na Wizara ya Afya.
“Nilipokuwa
nikifanya kazi Vikuruti, nilitakiwa nipewe maharage na unga na vitu
muhimu bure, lakini nilipewa mara moja tu,”analalamika Kishiwa.
Kauli ya MHN
Hata
hivyo, Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Aminiel
Eligaesha, anasema Kishiwa hakuwahi kufanya kazi katika hospitali hiyo
licha ya kusikia kuwa aliwahi kuwa daktari.
“Kwenye
kumbukumbu za hapa Muhimbili hakuna daktari kama huyo ingawa kuna
habari kuwa aliwahi kuwa daktari na kuna maprofesa ambao alisoma nao
darasa moja. Niliwahi kusikia kuwa anawafundisha masomo ya ziada
wanafunzi wa MUHAS,”anasema Eligaesha.
Profesa
Victor Mwafongo MNH anathibitisha kwamba alisoma darasa moja na Dk
Kishiwa, lakini hakuwahi kufanya naye kazi hospitalini hapo.
Anasema
kuwa alipotezana na Kishiwa kwa muda na hakufuatilia alipo, lakini
baadaye alipata taarifa kuwa ana matatizo ya akili na kufikishwa MNH kwa
ajili ya matibabu.
“Namafahamu
Kishiwa na nimesoma naye katika Chuo Kikuu cha Muhimbili, lakini
sikuwahi kufanya naye kazi hapa Muhimbili. Kwa sasa humwona mara nyingi
akizunguka hapa MNH, hukutana na kuzungumza naye kwa kuwa ananikumbuka
vizuri na mimi namkumbuka,”anasema Mwafongo.
Anafafanua kuwa anachofahamu kuhusu Kishiwa ni kwamba anapata tiba hospitalini hapo inayomsaidia hata kuwa kama alivyo sasa.