Siku chache baada ya kuanzisha ukaguzi wa magari na watu wanaoingia katika maduka ya Mlimani City, ukaguzi huo sasa umesitishwa.
Hatua
hiyo ilifuatia tishio la ugaidi baada ya duka la Westgate la Nairobi
nchini Kenya kushambuliwa na kikundi cha Al-shabab na kusababisha mauaji
ya watu 68 na wengi kujeruhiwa.
Mbali na Mlimani City lililopo Barabara ya Sam Nujoma, jijini Dar es
Salaam, maduka mengine makubwa kama vile Quality Plaza lililopo Barabara
ya Nyerere nalo lilianzisha ukaguzi kwa wateja wake.
Hata hivyo uchunguzi wa hivi karibuni umebainisha kuondolewa kwa
ukaguzi uliokuwa ukifanywa kwa wateja na magari yanayoingia dukani hapo,
kwa madai kuwa unapunguza wateja.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, askari wa kike wa kampuni ya
Omega Nitro inayolinda duka hilo, alisema kuwa hatua hiyo ilikuja Oktoba
16 mwaka huu.
“Nakumbuka Jumatano baada ya kumaliza ‘shift’ niliacha ukaguzi
ukiendelea, lakini niliporudi Ijumaa nikaambiwa umesitishwa mara moja,”
alisema na kuongeza:
“Kwa kweli ukaguzi wenyewe ulikuwa mgumu kwani hatukuwa na vifaa vya
kutosha na wateja ni wengi,” alisema na kuongeza: “Katika ukaguzi
tulikuta watu wengi na silaha hasa bastola wakimiliki kihalali.”
Jitihada
za kuupata uongozi wa Mlimani City hazikufanikiwa kwa kile
kilichoelezwa kuwa yuko likizo. Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kinondoni, Camilius Wambura alisema hana taarifa ya kusitishwa kwa
ukaguzi, lakini akasisitiza kuwa hilo ni suala lao binafsi.