Simba inaivaa Yanga katika Ligi Kuu ya soka Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Oktoba 20, mwaka huu.
KAZI nzuri imefanyika katika Ligi Kuu Bara ambayo sasa udhamini wake unafikia kiasi cha Sh 3.3 bilioni.
Hizi ni fedha nyingi na zinaleta matumaini kwa
mashabiki wa soka, lakini pia ni kielelezo cha kazi nzuri iliyofanywa
katika kushawishi wadhamini wakubali kuiunga mkono ligi hii ambayo ni
mhimili muhimu wa soka la Tanzania.
Wadhamini hao ni pamoja na Kampuni ya Simu ya
Vodacom Tanzania ambayo inatoa Sh 1.7 Bilioni pamoja na Azam Media ambao
wanatoa kiasi cha Sh 1.68 bilioni kwa msimu.
Kutokana na udhamini huo, kila klabu ya Ligi Kuu inajipatia kiasi cha Sh 165 Milioni kwa mwaka.
Kupatikana kwa fedha hizo kunaweza kumfanya
shabiki au kiongozi wa klabu ajiulize hali ingekuwaje bila ya udhamini?
Je, ligi yetu ingekuwa katika mazingira gani?
Swali la aina hiyo maana yake ni kwamba udhamini
uliopo sasa katika Ligi Kuu ni faraja ya kipekee kwa klabu, mashabiki,
wanasoka na maendeleo ya soka la Tanzania.
Hata hivyo pamoja na ukweli huo bado viongozi wa
klabu na wale wa TFF hawana sababu ya kubweteka na kuona kazi
waliyoifanya inatosha na kwamba ziada haihitajiki.
Ni kutokana na hilo ndiyo maana tunawahimiza
viongozi wa klabu wakishirikiana na wale wa TFF kuhakikisha kwamba
udhamini katika Ligi Kuu Bara unaongezwa na kuwa mkubwa zaidi ya huu
tunaojivunia sasa.
Kwamba badala ya klabu kupata Sh 165 milioni kwa msimu, ifikie zaidi ya Sh 300 milioni kwa msimu au hata zaidi.
Kuongezeka kwa ufadhili kuna maana kubwa katika
maendeleo ya mpira na hivyo kuwa na msaada mkubwa katika timu yetu ya
Taifa. Wachezaji watalipwa vizuri, waamuzi watalipwa vizuri, makocha
watalipwa vizuri na kila anayehusika katika soka na hivyo kuleta
ushindani wa kweli.
Tukitaka Ligi Kuu Bara iwe na ushindani ni lazima
tuwahamasishe wanaohusika kuanzia wachezaji kwa malipo mazuri, kuwaweka
katika kambi nzuri, vitu vitakavyowezekana tu pale tutakapoongeza
udhamini.
Tunaamini juhudi za dhati zikifanyika udhamini
unaweza kuongezeka tena kwa kiasi kikubwa tu. Bado kuna kampuni za
vinywaji kama vile soda ambazo zinaweza kudhamini ligi.
-MwanaSport
-MwanaSport