JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI
WIKIENDI hii miamba 10 ya soka barani Afrika
itaingia viwanjani kupambana kuwania nafasi tano za kuliwakilisha bara
hilo katika fainali za Kombe la Dunia zilizopangwa kuchezwa Brazil
mwakani.
Timu hizo ndizo zilizoingia raundi ya tatu ambayo
ni hatua ya mtoano. Kivumbi kitakuwa leo Jumamosi na kesho Jumapili
ambapo mechi za kwanza zitachezwa na marudiano yamepangwa kuwa kati ya
Novemba 15 na 19.
Kila timu sasa ipo katika hatua ya mwisho ya
maandalizi kwa ajili ya kujiandaa na mechi hizo ambazo zitachezwa
nyumbani na ugenini. Washindi wa mechi hizo ndiyo watakaoiwakilisha
Afrika katika fainali hizo maarufu duniani.
Wababe hao wanaowania fursa hiyo ni Ethiopia,
Tunisia, Ivory Coast, Ghana, Burkina Faso, Nigeria, Misri, Algeria,
Cameroon na Senegal.
Kati ya hizo, Ethiopia na Burkina Faso ndizo ambazo hazijawahi kupata nafasi ya kuiwakilisha Afrika katika Kombe la Dunia.
Makala haya. inaziangalia mechi hizo kwa mtazamo ufuatao;
Ivory Coast v Senegal
Ivory Coast ‘The Elephants’ itaingia uwanjani
Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny mjini Abidjan
kupambana na Senegal ‘Lions of Teranga’. Ivory Coast imewahi kufuzu
fainali hizo mara mbili wakati Senegal imewahi kufuzu mara moja tu.
Mechi baina ya timu hizo inatarajiwa kuwa na
upinzani mkubwa huku Ivory Coast ikipewa nafasi kwani kwa mara ya mwisho
timu hizi zilipokutana katika mechi za kuwania kufuzu kushiriki fainali
za Kombe la Mataifa la Afrika za mapema mwaka huu, Ivory Coast
ilishinda mabao 4-2 nyumbani.
Katika mechi ya marudiano jijini Dakar, Ivory
Coast ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-0 kabla ya mashabiki wa Senegal
kuanzisha vurugu kubwa na hivyo mechi kuvunjika.
Kutokana na vurugu hizo, Senegal ilifungiwa
kutumia uwanja wake wa nyumbani katika mechi za kuwania kufuzu kushiriki
fainali za Kombe la Dunia. Kwa hiyo hata mechi ya marudiano dhidi ya
Ivory Coast itachezwa kwenye uwanja huru.