Mama mzazi wa Shaban Maulidi, Aziza Ramadhan. |
Inadaiwa watu hao kabla ya kufanya ukatili huo walizizingira nyumba za jirani pia na kuingia moja baada ya nyingine kwa kugonga milango kwa nguvu na kuwashambulia kwa mapanga na nondo wakazi wake huku wakiwalazimisha watoe pesa.
Maneno Sungura ambaye naye alijeruhiwa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mama, baada ya mwanaye kuruhusiwa kutoka Hospitali ya Wilaya Geita alikolazwa aliondoka na baba yake na kwenda kufichwa sehemu ili kuepusha msongamano wa watu ambao wangefurika nyumbani hapo kumtazama.
“Wakiwa wameshanijeruhi sehemu mbalimbali kwa mapanga na nondo, wakataka hela. Nilikuwa na shilingi elfu kumi nimeifungia kwenye nguo, nikafungua nikawapa, chini ya kitanda nilikuwa na shilingi laki mbili nilizochangiwa na ndugu na jamaa waliokuwa wanakuja kumwona mwanangu hospitali, nazo wakachukua,” alisema Aziza.
Alipoulizwa kama tukio hilo linahusiana na kufufuka kwa mwanaye kama ilivyoenezwa na baadhi ya watu kwamba mtoto huyo hatakiwi kuishi, mama huyo alijibu:
Aziza Ramadhan akiwa na jeraha kichwani.
“Yawezekana maana waliniambia wametumwa kutuua mimi na mtoto wangu lakini wakasema endapo nina pesa niwapatie wasiniue. Kwa hiyo sijui kama lengo lao lilikuwa ni mtoto au la!”
Wengine waliojeruhiwa katika tukio hilo ni Maneno Sungura (36), Peter Kulwa (23) na Doto Lucas ambaye umri wake haukujulikana mara moja.
Majirani Zachary Petro, Bahati Musa na Samuel Runguya licha ya kujeruhiwa, pia waliporwa zaidi ya Sh. 388,000 na simu moja ya mkononi yenye thamani ya Sh. 45,000. Majeruhi wote walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kupatiwa matibabu na baadaye kuruhusiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, ACP Leonard Paulo alipotafutwa kwa njia ya simu na kuulizwa kuhusu tukio hilo hakukiri wala kukanusha kutokea na badala yake alisema: ”Niko sehemu mbaya sana,” akakata simu