Ufoo Peter Saro akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. |
Akizungumza na Uwazi, juzi nyumbani kwao Kibamba Dar, mdogo wa Ufoo aitwaye Goodluck Saro alisema ugomvi anaoujua yeye ni kitendo cha dada yake huyo kukataa kuhamia kwenye nyumba ya Kimara, Dar ambayo Anther aliipanga.
Alisema hajui kwa undani ni kwa nini dada yake alikuwa akigoma kuhamia makazi hayo mapya lakini kitendo hicho kilikuwa kikimfanya shemeji yake kubadilika.
“Siku za hivi karibuni shemeji alibadilika hata tabia. Zamani alikuwa akija anatuchangamkia sana, siku za hivi karibuni alikuwa akija, baada ya salamu haongei,” alisema Goodluck.
Wakizungumza na gazeti hili juzi, saa chache baada ya tukio hilo, baadhi ya majirani wa nyumbani kwa akina Ufoo walisema walishtushwa na milio ya risasi kutoka kwenye nyumba ya mama Ufoo, Anastazia Peter Saro wakidhani amevamiwa na majambazi.
“Ilikuwa saa kumi na moja alfajiri, mimi nilikuwa nimeshtuka kutoka usingizini lakini sijatoka kitandani, nilisikia milio ya risasi, nilijua mama Ufoo amevamiwa na majambazi.
“Lakini nikiwa najipanga jinsi ya kutoka nikasikia sauti ya mama Ufoo akisema jamani nakufa huku Ufoo akipiga kelele za kuomba msaada, nikashangaa maana najua haishi hapo, kwenda nikamuona Ufoo yupo nje akikimbia hovyo na damu chapachapa maeneo ya kifuani na mgongoni.
“Nilimuuliza kuna nini, kabla hajanijibu nikamwona mwanaume wake anatoka nje akiwa peku. Akasimama na kupiga risasi nyingine hewani kisha akaingia ndani.
“Muda huohuo nikasikia mlio mwingine wa risasi, nikajua kuna mauaji makubwa sana,” alisema jirani huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Jirani mwingine alisema alishtushwa sana na milio ya risasi, akaminya ndani akijua ni majambazi mpaka baadaye aliposikia watu wakilia huku wakisema mama Ufoo ameuawa kwa risasi na mkwe wake.
Habari nyingine zinadai kuwa Anther kabla ya kujiua, alikaa kwenye kochi kwanza na kujiandaa ambapo alisema: “Nimezaliwa siku moja nitakufa siku moja.” Akajilipua!
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura, marehemu Anther alikuwa akifanya kazi katika Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) nchini Sudan.
Habari za ndani zinadai kuwa usiku wa kuamkia siku ya tukio, mwanaume huyo akiwa nyumbani kwa Ufoo, Mbezi, Dar hawakulala kwa ugomvi ambapo marehemu alisikika akimshutumu mchumba wake huyo mambo ambayo hakuyaweka wazi.
Ikadaiwa kuwa ili kumaliza mgogoro, saa kumi na nusu alfajiri waliondoka kwenda Kibamba kwa mama wa Ufoo ili akasaidie kurejesha amani.
Katika kurudisha amani, mama Ufoo alikuwa mstari wa katikati, akiwa hapendelei lakini marehemu Anther alimshutumu mama mkwe wake huyo kwamba anampendelea mwanaye.
Ndipo alipotoa bastola na kuielekeza kwa mama Ufoo na kumpiga risasi ya kifuani. Mama huyo alianguka na kukata roho papo hapo.
Aliielekeza bastola kwa Ufoo na kumfyatulia risasi nne, mbili kifuani, moja begani na nyingine tumboni ambapo damu zilimtoka kwa wingi.
Ufoo alikimbizwa katika Hospitali Teule ya Tumbi (Kibaha) na baadaye kukimbizwa Muhimbili.