Home » » JE UNATAMBUA KUWA DAWA ZA HOSPITALI NDIZO ZINAGEUZWA KUWA DAWA ZA KULEVYA ..??

JE UNATAMBUA KUWA DAWA ZA HOSPITALI NDIZO ZINAGEUZWA KUWA DAWA ZA KULEVYA ..??


Matumizi ya dawa za kulevya nchini yamechukua sura mpya, baada ya kubainika kuwa watumiaji wengi wa dawa hizo aina ya heroin na cocaine sasa wanatumia dawa za hospitali zenye uwezo wa kulevya kuwa mbadala.
Matumizi hayo mabaya yamebainika kutokana na kuwapo ongezeko la matumizi ya dawa za hospitali zilizo na nguvu inayoelezwa kulingana na dawa za kulevya ikiwamo heroin, cocaine na amphetamine.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Uhalifu na Dawa za Kulevya (UNODC) ya mwaka 2013, inathibitisha ongezeko hilo la matumizi ya dawa hizo, ambazo kitaalamu zinaitwa ‘new psychoactive substances (NPS).
“Dawa mbadala za dawa za kulevya zimezua wasiwasi mkubwa siyo kwa sababu ya ongezeko la matumizi yake, bali hata ukosefu wa utafiti wa kisayansi na uelewa wa matumizi yake,” ilisema sehemu ya ripoti ya UNODC.

Katibu Mkuu UNODC, Yury Ferdotov alieleza katika ripoti hiyo ya hali ya dawa za kulevya mwaka 2013 kwamba, changamoto kubwa iliyopo katika kudhibiti dawa hizo duniani ni matumizi ya dawa za hospitali na kemikali zinazotumika kuzitengeneza kutumika kama dawa za kulevya.
Alisema nchi nyingi duniani hazina sheria wala uelewa kuhusu kemikali hizo, jambo linalosababisha wafanyabiashara wakubwa kuendelea kusafirisha kemikali hizo au kutumia teknolojia kulima mimea inayotumika kutengeneza dawa hizo.
UNODC limefafanua kuwa matumizi mabaya ya dawa hutokea wakati dawa za hospitali zinapotumika kwa malengo mengine kinyume na tiba.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa aina tisa ya dawa za hospitali ni miongoni mwa dawa zinzouzwa kwa njia ya panya kama mbadala wa heroin na cocaine.
Dawa hizo ni pamoja na mephedrone, ketamine, benzodiazepine, tramadol na dextromethorphan.
Nyingine ni piperazines, phencyclidines, trypitamines na aminoindance.
Uchunguzi huo umebainisha kwamba unaweza kuzipata dawa hizo kwa wafamasia wasio waaminifu katika hospitali kubwa ambapo huuzwa kwa bei nafuu na wakati mwingine katika maduka ya dawa muhimu.
Mwananchi Jumamosi lilipita katika baadhi ya maduka ya dawa na kufanikiwa kuzinunua dawa hizo zilizothibitishwa kutumika mbadala wa dawa za kulevya bila ya kuwa na cheti cha daktari.
Dawa zilizonunuliwa na gazeti hili ni pamoja na dawa aina ya Tramadol, morphene, phencyclidines na valium.
Pamoja na matumizi hayo pia, ilibainika kuwa dawa za kifua au za pumu ambazo zina kemikali aina ya codeine na zile zenye mchanganyiko wa dextromethorpen, pia zinatumiwa kama dawa za kulevya.
Pamoja na dawa hizo kutoruhusiwa kuuzwa bila cheti cha daktari, watu wengi wamekuwa wakizipata kwa urahisi na bei nafuu katika maduka ya dawa maeneo mbalimbali nchini hasa mijini.
Gazeti hili limebaini kuwa dozi moja ya dawa aina ya Tramadol inayotumika kutuliza maumivu lakini inatumika kama heroin, huuzwa katika maduka ya dawa bila cheti cha daktari na bei ndogo.
Kitaalamu dawa hiyo inaelezwa kumfanya mtu kupata kilevi kinachoweza kulingana na mtumiaji wa dawa za kulevya.
TFDA wazungumza
Msemaji wa Shirika la Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza alikiri dawa hizo kutumiwa vibaya na watumiaji wa dawa za kulevya jambo alilosema linakuzwa zaidi na ukosefu wa maadili.
“Kama wafamasia wanauza dawa hizo kwa siri basi watakuwa wanavunja ile Sheria ya Famasia ya Mwaka 2001 ya Dawa Muhimu,” alisema Simwanza.
Alisema TFDA inachunguza kwa umakini matumizi mabaya ya dawa hizo na endapo watabaini wafamasia wanaouza dawa hizo kinyume na taratibu, watachukuliwa hatua kali.
Hata hivyo, Simwanza alisema kuwa kuna changamoto kubwa katika usimamizi na udhibiti wa ununuzi wa dawa.
Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya
Mchambuzi wa Masuala ya Mifumo ya Kompyuta kutoka Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, January Nkisi naye alikiri kuwepo kwa dawa mpya za hospitali zinazotumika kama mbadala wa dawa za kulevya.
Nkisi aliongeza kuwa kutokana na kuwepo dawa hizo, tume hiyo kwa sasa inafanya kazi kwa ukaribu na TFDA, Ofisi ya Mkemia Mkuu na Jeshi la Polisi katika kuhakikisha kuwa kemikali hizo zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya zinajulikana na hazipitishwi katika mipaka ya nchi.
Nkisi alisema kuwa tume hiyo inaendelea kufanya kazi kwa kasi katika kupata taarifa kutoka vyombo vya kimataifa ili kujua namna dawa za kulevya zinavyopitishwa, pamoja na mbinu mpya zinazotumiwa na wasafirishaji wa dawa za kulevya.
Akitoa mfano wa vilevi aina ya pombe, sigara na mirungi alisema kuwa vyote hivyo vina madhara na athari za muda mrefu kama zilivyo dawa za kulevya na kwamba sheria hazina budi kuundwa kwa kuangalia mifumo ya matumizi ya vilevi hivyo.
Naye Asia Gregory ambaye ni mfamasia kutoka duka la dawa baridi Buguruni alisema kuwa mtu anayetumia dawa kama ketamine, tramadol na kundi la dawa aina ya benzodiazepine hupata matokeo sawa na anayetumia heroin au cocaine.
“Hata mtu wa kawaida akitumia dawa hizi kwa muda mrefu huanza kumfanya awe tegemezi. Akizikosa hupata athari kama kuwashwa, mate kumdondoka, kupata hali kama ya degedege, kutetemeka, kutokwa jasho jingi na ili aondokane na hali hiyo, basi huhitaji dawa hizo tu,” alisema.
Gregory alitoa mfano wa dawa aina ya morphene ambazo ni za maumivu makali akisema zina uwezo wa kulevya sawa na heroin.
Alizitaja pia dawa za usingizi aina ya ketamine ambazo hutumika katika upasuaji kuwa nazo hutumiwa na waathirika wa dawa za kulevya.
Alitoa angalizo kuwa hata wagonjwa ambao hawakuwa na nia ya kutumia dawa hizo kama mbadala wa dawa za kulevya huathirika, hivyo lazima utafiti wa kina ufanyike.
Utafiti uliofanywa Tanzania
Utafiti uliofanywa na Erasmus Mndeme wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), kuhusu matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana mkoani humo ulibaini kuwa, vijana wengi wanatumia dawa aina ya benzodiazep kuwa mbadala wa dawa za kulevya.
Utafiti mwingine uliochapishwa mwaka huu ulibaini kuwa, dawa mbadala wa dawa za kulevya zinazotumiwa zaidi ni zile dawa zenye codeine.
Dawa hizo hutumiwa na vijana kwa asilimia 59.6, huku valium na morphine zikitumika kwa asilimia 1.8 huku mbadala mwingine unaotumiwa na vijana ukitajwa kuwa ni glue na petroli.
Aidha, utafiti huo ulibaini kwamba vijana wengi wameanza kutumia dawa mbadala wa dawa za kulevya wakiwa na umri wa kuanzia miaka 12.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili na mtaalamu wa waathirika wa Dawa za Kulevya, Augustine Godman, alithibitisha kuwa watu wengi wamegundua matumizi ya dawa za hospitali kama dawa za kulevya.
Alisema kuwa chanzo kikubwa cha hali hiyo ni uuzaji holela wa dawa hizo katika maduka ya dawa.
“Sheria zingekuwa zinafuatwa vijana wasingeharibika kiasi hiki. Sasa wanauziwa dawa hizo katika maduka ya dawa bila kuhojiwa chochote,” alisema.
Dk Godman alisema kuwa amekuwa akitibu vijana wengi walioathirika kwa dawa za kulevya katika kliniki yake, chanzo kikubwa kikiwa ni dawa za kulevya ambazo ndani yake kuna chembechembe ya dawa aina ya benzodiazepine na morphine.
“Unajua watu wanadhani dawa za kulevya ni heroin na cocaine pekee, lakini vijana wanavuta petroli, gundi, dawa za maumivu na za kifua ambazo zina codeine, vyote hivi vinaathiri,” alisema.
Aliongeza kuwa ulevi wa aina yoyote ni sawa na dawa za kulevya ikiwemo bangi, mirungi na mimea yoyote inayolevya.
“Hili ni janga. Unawaacha watu wanaathirika kwa kutumia Sh2,000 au 3,000, lakini unapata kazi ya kuwatibu ya zaidi ya Sh100 milioni,”alisema akisikitika Dk Godman.
Mfamasia Charles Lymo wa Hospitali ya Amana wilayani Ilala alisema kuwa mtu anapokunywa dawa ya benzodiazep hujisikia hali ya raha na maisha mazuri.
“Mtu anaweza kujisikia ana mali nyingi, amani humwingia moyoni, yaani anapata faraja ya kina na anasinzia,” alieleza Lymo.
Alisema kuwa dawa nyingine ambazo huweza kufanya kazi kama mbadala wa dawa za kulevya ni amephetamine na phenobabiton.
Joshua Joseph (siyo jina halisi), ambaye ni mwathirika wa dawa za kulevya, mkazi wa Tabata Dar es Salaam alisema kuwa anapokosa cocaine, hununua dawa aina ya tramadol na kuchanganya na valium, kisha kuzisaga na kuvuta kama wanavyovuta dawa nyingine za kulevya.
“Unakuwa ‘high’ kama kawaida lakini tunazitumia zaidi kama tumekosa unga wa kawaida,”alisema.
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Imeeleza kuwa idadi kubwa ya watu wanaougua maradhi ya akili wanaofika katika hospitali hiyo huonyesha historia ya kutibiwa kimakosa au kutumia dawa aina ya benzodiazepine kabla ya kupelekwa hospitali.


 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. BONGONEWS TZ - All Rights Reserved
Template Modify by Creating Website
Proudly powered by Blogger