Ikulu imesema Rais Jakaya Kikwete hatakubali kuidhinisha kama akipelekewa ombi la kuongeza kiinua mgongo cha wabunge kutoka Sh43 milioni hadi Sh160 milioni.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu
alisema jana kuwa Rais Kikwete hajapokea maombi hayo huku akipinga
maelezo kuwa Serikali ilishayakubali.
Gazeti la The Citizen wiki iliyopita,
lilimkariri Waziri wa Fedha, Saada Mkuya akisema Serikali ilikuwa
imepitisha kupandishwa kwa kiwango cha kiinua mgongo kutoka Sh43 milioni
hadi Sh160 milioni baada ya kumaliza kipindi cha miaka mitano.
Waziri huyo alikaririwa akisema kuwa kiwango hicho
kilipitishwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na tayari wabunge walishaanza
kuchukua fedha hiyo licha ya ukweli kuwa Bunge hili halijamaliza muda
wake.
Hata hivyo, Rweyemamu alisema nao wamelisoma suala
hilo kwenye magazeti na kwamba halijafika Ofisi ya Rais... “Suala hili
halijafika Ofisi ya Rais hata kama litaletwa, `I really doubt if the
President will endorse such matter’ (Nina shaka kama Rais ataidhinisha
suala hili).”
Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi katika Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi tayari
imekanusha vikali taarifa za kupandishwa kiwango hicho cha malipo kwa
wabunge.
Kashililah akanusha
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alikanusha kuwapo kwa mapendekezo ya wabunge kulipwa kiasi hicho cha fedha.
“Malipo ya wabunge yanalipwa kwa mujibu wa sheria
kwa Kiingereza inaitwa Political Service Retirement Benefits Act (Sheria
ya Malipo ya Utumishi kwa Viongozi wa Kisiasa) ni sheria namba 3 ya
1999, kwa hiyo hakuna malipo yoyote yanayoweza kufanyika nje ya sheria
hiyo,” alisema Dk Kashililah na kuongeza:
“Sheria inaelekeza kila kitu, kwa kuzingatia
uhalisi wa mishahara ya wabunge kwa sasa, malipo yao ya mwisho hayawezi
kufikia kiasi cha Sh160 milioni, hata kama mishahara itaongezwa
haitaweza kufikia kiwango ambacho kitamwezesha mbunge kulipwa kiasi
hicho cha fedha.”
Katibu huyo wa Bunge alisema malipo ya kiinua
mgongo kwa wabunge yanakokotolewa kutokana na kiwango chake cha mshahara
tu na siyo malipo ya posho za kuendesha shughuli za kibunge.
Licha ya Dk Kashililah kukataa kutaja kiwango cha
mshahara wa mbunge kwa mwezi, gazeti hili limebaini kuwa malipo hayo kwa
sasa ni Sh3.4 milioni.
Mbali ya mshahara, wabunge pia hulipwa fedha nyingine kiasi cha
Sh8.2 milioni kwa ajili posho ya jimbo, gharama za ofisi, mafuta, malipo
ya wasaidizi wao na dereva.
Matakwa ya sheria
Sehemu ya tano ya Sheria ya Malipo ya Utumishi kwa
Viongozi wa Kisiasa katika Kifugu cha 21 inasema mbunge atalipwa kiinua
mgongo ambacho ni asilimia 40 ya mshahara ya kila mwezi katika kipindi
chote cha utumishi wake.
Kadhalika, Kifungu 18 (3) Mbunge atalipwa malipo
ya nyongeza yanayoitwa posho ya ukomo wa Bunge (winding up allowance)
ambayo ni asilimia 20 ya jumla ya mishahara yake ya miezi 24 iliyopita.
Kwa tafsiri ya sheria hiyo na kwa kigezo cha
mshahara wa Sh3.4 milioni, wabunge wa sasa watalipwa kiasi cha Sh97.92
milioni watakapomaliza uongozi wao mwishoni mwa mwaka ujao.
Malipo hayo ni Sh81 milioni ambayo ni asilimia 40
ya jumla ya mishahara ya miezi 60 ya utumishi wa wabunge hao na Sh16.32
ambazo asilimia 20 ya mishahara ya miezi 24 kwa ajili ya malipo ya posho
ya ukomo wa ubunge.
Malipo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia zaidi
ya 100 ya kiinua mgongo cha Sh43 milioni walicholipwa wabunge
waliostaafu 2010.
Kabla ya kupandishwa kwa kiwango hicho kuwa Sh43
milioni mwaka 2010, kwa miaka kadhaa kiwango cha kiinua mgongo kwa
wabunge kilikuwa Sh20 milioni.
>>Mwananchi
>>Mwananchi