Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna wa Polisi Hamdani Omari Makame, alisema tukio la kwanza lilitokea Februari 23 mwaka huu, saa saba mchana eneo la Pangawe.
Alisema mlipuko huo ulitokea baada ya waumini wa dhehebu la Evengilistic kumaliza ibada na haukuleta madhara yoyote.
Aliongeza kuwa, wakati polisi wakishughulikia tukio hilo, saa 6:36 mchana ikatokea milipuko mingine mitatu katika maeneo mawili tofauti.
"Mlipuko wa kwanza ulitokea eneo la Malindi mjini Zanzibar kwenye Mkahawa wa Mercury unaomilikiwa na Bw. Simai Mohammed Saidi (45) lakini haukuwa na madhara.
"Ilipofika saa 8:35 na 8:40 kwenye mtaro mmoja uliopo karibu na Mkunazini, eneo la Mji Mkongwe, Mjini Zanzibar ilitokea milipuko miwili iliyopishana kwa muda wa dakika chache," alisema.
Alisema milipuko hiyo pia haikuleta madhara kwa binadamu isipokuwa gari moja lenye namba Z.355 ET Harrier mali ya Bw. Mohammed Ibrahim Ali, lililoegeshwa karibu ya mtaro lilipata madhara kidogo kwa kutoboka bati upande wa nyuma kulia.
Kamishna Makame alisema milipuko yote ilitengenezwa kienyeji na Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wamechukua mabaki ya milipuko hiyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kitaalamu.
Aliongeza kuwa, polisi wameimarisha doria katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Zanzibar ili kuhakikisha matukio kama hayo hayatokei tena na kuweza kuwakamata wahalifu hao.
"Tayari timu ya Makachero wakiwemo Wataalamu wa Uchunguzi wa Kisayansi kutoka Makao Makuu ya Upelelezi, Dar es Salaam, wamewasili mjini Zanzibar kuungana na Makachero wenzao wa Zanzibar kuendelea na uchunguzi huu," alisema.
Alisema katika hali isiyo ya kawaida, Mkoa wa Kusini Unguja, juzi saa nane mchana katika Kijiji cha Unguja Ukuu, eneo la Kae Pwani, kulikuwa na wavuvi wakivua vyuma ili kwenda kutengeneza nanga ya boti lao, lakini wakati wakiendelea na kazi hiyo chuma walichokuwa wakikitengeneza kililipuka na kujeruhi watuwanne.
Waliojeruhiwa na kukimbizwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ni Juma Abdallah Juma (32), Shabani Khamisi Ibarahim (32) Haji Khamisi(35) na Sumai Hussein Hassan (38).
Wakati majeruhi hao wakiendelea na matibabu, majeruhi mmoja Juma Abdallah Juma (32) alifariki dunia saa 11 jioni na mmoja kati yao Sumai Hussein Hassani (38) alitibiwa na kuruhusiwa ambapo wengine wawili wanaendelea na matibabu.